Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Saturday, November 30, 2013


MAKAMU WA RAIS DKT.BILAL Aendesha Zoezi la Harambee ya Kuchangia Madawati Mfuko wa Maendeleo ya Elimu JIMBO la Nkenge

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza wakati wa hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Elimu Jimbo la Nkenge kununua madawati ili kusadia shule za msingi za Jimbo hilo. Harambee hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam, jana usiku. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Asumta Mshana na (kushoto kwa Makamu) ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanal Fabian Masawe
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi cheti, Mkurugeniz wa Kagera Sugar, Hamadi Yahya, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake wa kuchangia maendeleo ya Elimu ya Jimbo la Nkenge mkoa wa Kagera,wakati wa hafla ya harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Elimu Jimbo la Nkenge kununua madawati ili kusadia shule za msingi za Jimbo hilo. Harambee hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam, jana usiku. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Asumta Mshana na (kushoto kwa Makamu) ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanal Fabian Masawe
Meza Kuu wakijumuika kuimba wimbo maalumu wa mkoa wa Kagera wa kuhamasisha maendeleo ya mkoa huo, hususan katika suala la elimu na kuchangia madawati.

  Mbunge wa Jimbo la Nkenge, ambaye ni mratibu wa Harambee hiyo, Asumta Mshana, akizungumza kutoa ushuhuda wa matatizo ya Elimu katika jimbo lake
 Msanii wa Sanaa ya Ngoma akitumbuiza katika hafla hiyo ya harambee ya kuchangia madawati kwa skuli za Jimbo la Nkenge. Picha na OMR

Dkt Shein, azungumza na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria Daniel Ole Njooley.

  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Balozi wa Tanzania Nchini Nigeria Daniel Ole Njooley,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kumuaga Rais leo,baada ya kuteuliwa  kushika nafasi hiyo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akiagana  na  Balozi wa Tanzania Nchini Nigeria Daniel Ole Njooley,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar  leo,baada ya kuteuliwa  kushika nafasi hiyo,[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

Ndege iliyopotea Msumbiji yapatikana


Ndege iliyopotea tangu jana baada ya kuruka kwenye anga ya Msumbuji kuelekea Angola ikiwa na watu 34 imepatikana katika mbuga za wanyama Kaskazini Magharibi mwa Namibia.
Ndege hiyo ilitakiwa kutua kwenye uwanja wa Luanda.
Msemaji wa Polisi nchini Namibia amesema ndege hiyo iliteketea yote huku kukiwa hakuna aliyenusurika.
Ndege hiyo namba TM470 iliondoka Maputo nchini msumbiji tangu siku ya ijumaa na ilikuwa ikielekea Luanda nchini Angola.
mabaki ya ndege hiyo iliyoteketea kabisa yamepatika kwenye mbuga ya wanyama Bwabwata karibu na mpaka wa Angola na Botswana.
"Ndege imeteketea yote yamebaki majivu tu hakuna hata mtu mmoja aliyenusurika," Naibu Kamishna wa Polisi nchini Namibia Willy Bampton amenukuliwa na shirika la habari la Reuters.
Inaelezwa kuwa masiliano ya mwisho na ndege hiyo yalikuwa ni wakati ndege hiiyo ilipofika kaskazini mwa Namibia.
Kwa mujibu wa shirika la ndege la Msumbiji abiria walipanda ndege hiyo ni raia 10 wa Msumbiji, Angola 9, Wareno 5, Mfaransa 1 , Mbrazili 1 na Mchina 1.
Jopo la watu waliokuwa akifanya kazi ya kuitafuta ndege hiyo walishindwa kuingia kwenye mbuga hiyo hapo jana baada ya mvua kubwa kunyesha kufanya barabara kushindwa kupitika.
Abiria 28 na wafanyakazi sita walikuwa kwenye ndege hiyo wakitoka Maputo kuelekea Luanda.

Mchakato wa sarafu moja EAC kuendelea kujadiliwa


Umoja wa sarafu ni moja kati ya mambo makuu manne yaliyoainishwa katika mkataba wa EAC. PICHA | AFP 
Na Peter Saramba, Mwananchi
Kampala. Wakuu wa Nchi Tano Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), leo Novemba 30, wanatarajiwa kutia saini mkataba wa kuwa na sarafu moja.
Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Mawasiliano wa EAC, Richard Owora aliwaambia waandishi wa habari jijini hapa kuwa sherehe za kutia saini mkataba huo utakaoanzisha mchakato wa miaka kumi hadi kufikia lengo la kuwa na sarafu moja ya EAC, zitafanyika katika Viwanja vya Kololo jijini Kampala.
Marais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Yoweri Mseveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Nkuruzinza wa Burundi na Uhuru Kenyatta wa Kenya wanatarajiwa kuwa jijini hapa kuhudhuria mkutano wa mwaka wa wakuu wa nchi za EAC.
Umoja wa sarafu ni moja kati ya mambo makuu manne yaliyoainishwa katika mkataba wa EAC. Masuala mengine ni soko la pamoja na umoja wa forodha ambayo tayari mikataba yake imesainiwa na kuanza kutekelezwa, ingawa kwa kasi isiyotosheleza kutokana na vikwazo kadhaa.
Hatua ya mwisho na juu kabisa katika ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni shirikisho la kisiasa linalolenga kuwa na nchi moja, hatua itakayozihakikishia nchi za ukanda huo nguvu ya soko, biashara, majadiliano na uamuzi katika ngazi ya ndani na kimataifa.
Huu ni mkutano wa kwanza kuwakutanisha wakuu wote wa EAC tangu kuibuka kwa migongano ya kimawazo na mtazamo miongoni mwao kuhusu utekelezaji wa makubaliano na miradi iliyo katika mipango ya EAC pamoja na njia bora na sahihi ya kumaliza vita na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe ndani ya baadhi ya nchi wanachama.
Katikati ya migongano hiyo, nchi za Kenya, Uganda na Rwanda zilishuhudiwa zikifanya vikao vitatu na kufikia uamuzi kutekeleza baadhi ya miradi bila kuzishirikisha nchi za Burundi na Tanzania, hali iliyozua malalamiko kutoka kwa nchi zilizotengwa na hivyo kuibuka hofu juu ya hatima ya Jumuiya.
Wakati huohuo, Boniface Meena anaripoti kutoka Nairobi kuwa, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema uanzishwaji wa sarafu ya pamoja Afrika Mashariki utaimarisha ushindani katika masoko ya ndani ya nchi wanachama.
Rais Kenyatta alisema hayo jana alipokuwa akiwahutubia wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), lililokutana jijini Nairobi, Kenya.
“Hii itasaidia pia kupunguza gharama za shughuli za fedha ya utumiaji wa sarafu tofauti katika nchi zote tano,” alisema Rais Kenyatta na kuongeza:
“Kwa njia tofauti, muungano wa fedha ni moja ya jitihada za kuunganisha nchi, vitu vyote tunavyovitafuta katika shirikisho vitafanikiwa kupitia muungano wa fedha.”
Rais Kenyatta alisema hiyo pia itawahakikishia wawekezaji kuwa Afrika Mashariki ni soko moja la uhakika na sehemu bora ya kufanya biashara.
Alisema kutiwa saini kwa itifaki hiyo kutafungua njia ya kuufanikisha ndani ya kipindi cha miaka kumi.

Ushahidi wa umiliki wa Ziwa Nyasa watolewa


Watu wa viunga vinavyolizunguka Ziwa Nyasa /Ziwa Malawi wakiendelea na shughuli za uvuvi. Tafiti mbalimbali zimeonyesha wengi wao hawaelewi hasa chanzo cha mtafaruku huu wa mipaka ya Ziwa ulioibuka kati ya Tanzania na Malawi. PICHA | PLATOURS (KWA HISANI) 
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi 
Dar es Salaam. Malawi na Tanzania zimewasilisha ushahidi na majibu ya maswali kuhusu umiliki wa maeneo kwenye Ziwa Nyasa, kwa jopo la wasuluhishi linaloongozwa na Rais mstaafu wa Msumbiji Joachim Chissano.
Wasuluhishi hao walizitaka Malawi na Tanzania kutoa majibu ya maswali manne muhimu, wakati wakiwasilisha ushahidi wao kuhusu umiliki wa ziwa hilo wenye mgogoro.
Mgogoro huo uliibuka baada ya Serikali ya Malawi bila kushauriana na Tanzania kutoa leseni kwa kampuni mbili za kigeni, kutafuta mafuta katika eneo la ziwa ambalo linamilikiwa na Tanzania.
Kwa mujibu wa gazeti la mtandaoni la Malawi la  Nyasa Times, msemaji wa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa Malawi, Quent Kalichero alithibitisha Jumatano wiki hii kwamba nchi hiyo imewasilisha majibu ya maswali hayo na ushahidi uliohitajika.
“Waziri wetu amewasilisha taarifa maalumu ya maandishi kwa wasuluhishi na kwa sasa yuko nchini Msumbiji, kwa ajili ya suala hilo,” alisema Kalichero juzi.
Makabidhiano hayo yalifanyika mjini Maputo, Msumbiji ikiwa ni siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kufanya mazungumzo na wasuluhishi, marais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chissano na wa Botswana, Festus Mogae jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mkutano huo wa Jumatatu mjini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe aliwaeleza wanahabari kwamba mazungumzo baina ya Rais Kikwete na wasuluhishi hao yalihusu zaidi ushahidi wa Tanzania katika suala la umiliki wa Ziwa Nyasa.
Pia alithibitisha kwamba Tanzania ilikuwa tayari  kuwasilisha ushahidi wake kwa sekretarieti ya ofisi ya waliokuwa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) inayoongozwa na Chissano, Jumatano iliyopita.
Baada ya mkutano huo wa Jumatatu, Membe alieleza kwamba nchi zote husika, yaani Tanzania na Malawi zinatakiwa kuheshimu maagizo na kuwasilisha ushahidi huo kwa wakati, na kuwaachia wasuluhishi kazi ya kupitia na kutekeleza wajibu wao wakiwa wamepewa muda unaofikia mwaka mmoja kupata suluhu.
Wasuluhishi hao wa Sadc, Chissano na Mogae waliwasili jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita kwa ajili ya mazungumzo kuhusu mgogoro huo, kama walivyofanya kwa Malawi Julai mwaka huu.
Julai mwaka huu, Rais Joyce Banda wa Malawi alinukuliwa akisema kuwa nchi yake haina nia ya kulegeza kamba katika mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa na Tanzania.
 Alitoa msimamo huo baada ya kukutana na Chissano wa Msumbiji na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini ambao ni wajumbe maalumu wa Jumuiya ya Sadc katika mgogoro huo.Alisema kwamba madai ya Tanzania kuwa inamiliki sehemu ya Ziwa Nyasa, siyo ya kweli na kwamba mpaka uko ufukweni mwa ziwa hilo upande wa Tanzania.
Rais Banda alidai kuwa nchi yake inafuatilia kwa karibu upatanishi wa SADC na kwamba isiporidhishwa na uamuzi ya jumuiya hiyo italiwasilisha suala hilo Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ).
Kabla ya hatua hiyo ya Malawi,  Aprili mwaka huu Serikali ya Tanzania iliitaka nchi hiyo kuacha kutapatapa na kuonya kuwa kamwe isithubutu kugusa eneo hilo la mpaka.
Akitoa kauli ya Serikali ya Tanzania Membe alisema: “Nadhani watasikia na kuelewa, Serikali ya Malawi iache kutapatapa, nchi zote ilikoenda kulalamika kuhusu mgogoro huu, Tanzania tumekuwa tukielezwa na hata hao wanaotueleza wanaishangaa sana Malawi.” Kauli hiyo ya Serikali ilifuatia Rais Banda kusema kuwa mgogoro huo sasa utapelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), kwa madai kwamba juhudi za usuluhishi wa kidiplomasia zimeshindikana.
Hata hivyo, uamuzi huo wa Malawi ni kinyume na makubaliano baina ya nchi hizo mbili yaliyofanyika Novemba 7 mwaka jana, jijini Dar es Salaam ambapo zilikubaliana kwamba jopo hilo ndiyo sehemu ya mwisho ya makubaliano.
Katika maelezo yake, Rais Banda alisema nchi yake imejitoa katika mazungumzo ya usuluhishi kwa madai ya kuhujumiwa na katibu wa jopo hilo ambaye ni Mtanzania, John Tesha kwa maelezo kuwa anavujisha taarifa muhimu za Malawi kwa Tanzania kabla ya Tanzania haijawasilisha taarifa zake kwa jopo hilo. Alisema kuwa tangu kuibuka kwa mgogoro huo, Malawi imekwenda kulalamika katika nchi za Uingereza, Marekani, Umoja wa Afrika (AU) na katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc).
Hata hivyo, baadaye Julai mwaka huu, Serikali ya Malawi ilitangaza kuwa itaendelea na mazungumzo na Tanzania kuhusu mpaka huku ikieleza kuwa viongozi wa Tanzania hawaelewi mipaka ndiyo maana wanapigania kuwa wao ni sehemu ya ziwa.
Waziri wa Habari wa Malawi, Moses Kunkuyu aliliambia Shirika la Utangazaji la Malawi (MBC) kuwa viongozi wote wa Tanzania wanadhani wanamiliki Ziwa Malawi (Nyasa) lakini watakuja kubaini baadaye kuwa hawana hata tone la umiliki.

Kilimo chaporomoka, gesi, madini zashika chati katika Ripoti ya Uwekezaji


Jitihada za makusudi zinahitajika ili kuwavutia zaidi wawekezaji ili kuwekeza katika kilimo nchini kwani kwa sasa hali ya sekta hii nyeti si njema. PICHA | AFP 
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Dar es Salaam. Taarifa ya Uwekezaji Tanzania mwaka 2012 imetaja kuporomoka kwa kilimo huku madini na nishati zikiongezeka kwa kiasi kikubwa.
Kwa miaka mingi Tanzania imetaja kilimo kuwa ndiyo uti wa mgongo wa taifa ambapo zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wake hukitegemea, huku ikipanga na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukikuza, ikiwamo Kilimo Kwanza.
Hata hivyo, taarifa hiyo iliyozinduliwa jana na Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu jijini Dar es Salaam ilieleza kuwa, jitihada za makusudi zinahitajika ili kuwavutia zaidi wawekezaji ili kuwekeza katika kilimo nchini.
Pia taarifa hiyo inasema kwamba, mikakati inayoendelea kwenye sekta ya gesi na umeme inahitaji kufuatiliwa zaidi ili kutatua tatizo la upatikanaji wa nishati hiyo kwa uhakika na kwa bei nafuu.
Pia taarifa hiyo inasema kwamba, mikakati inayoendelea kwenye sekta ya gesi na umeme inahitaji kufuatiliwa zaidi ili kutatua tatizo la upatikanaji wa nishati hiyo kwa uhakika na kwa bei nafuu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dk Natu Mwamba alisema kwamba, utafiti huo  walioufanya Tanzania Bara na Visiwani ulibaini kuwa shughuli za umeme na gesi asilia ambao uwekezaji wake ulikuwa chini ya Dola za Marekani 3 milioni  kati ya mwaka 2008 na 2009 uliongezeka na hadi kufikia Dola 290.5 milioni,  mwaka 2010 na Dola 290.4 milioni mwaka 2011.
Kwa upande wa kilimo, alisema kuwa uwekezaji binafsi ulioingia uliongezeka kutoka Dola za Marekani 21milioni mwaka 2008  hadi kufikia 31 milioni, mwaka 2011.
“Uwekezaji katika sekta ya kilimo uliendelea kuwa mdogo ukilinganisha na sekta nyingine hususan madini na viwanda,” alisema Dk Mwamba aliyekuwa akimwakilisha Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu na kuongeza:
“Jitihada za makusudi zinahitajika hasa kuwekeza kwenye miundombinu vijijini, miradi ya umwagiliaji, upatikanaji wa umeme vijijini kwa ajili ya kuwezesha usindikaji wa mazao pamoja na uchoraji wa ramani zenye utambuzi na mgawanyo wa matumizi ya ardhi nchi nzima.”
Akizindua ripoti hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu alisema kuwa ili kuongeza sekta ya uwekezaji hasa kilimo ni lazima kuboresha miundombinu mbalimbali ili kuendelea kuwavutia wawekezaji.
Alitaja moja ya mambo yanayokwamisha wawekezaji nchini kuwa ni ufanisi wa bandari za hapa nchini kutokutoa huduma kwa ufanisi kutokana na kuchelewa kutoa mizigo inayoingia nchini.
Dk Nagu alisema suala la wananchi kudai fedha ili kutoa ardhi au jambo lolote la uwekezaji ndani ya eneo lao ni miongoni mwa mambo yanayorudisha nyuma maendeleo na kuwafanya wawekezaji kutokuvutiwa kwenda  kuwekeza katika maeneo yao.
Taarifa hiyo iliandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Rais Kabila azuru mashariki mwa Congo

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,Joseph Kabila, anatembelea eneo la mashariki mwa Congo ambalo awali lilidhibitiwa na kikundi cha waasi wa M23, ambacho kilishindwa katika mapigano dhidi ya majeshi ya Congo yakisaidiwa na yale ya Umoja wa Mataifa, mwezi mmoja uliopita.
Rais Joseph Kabila wa DR Congo
Anatarajiwa kuwasili eneo la Rutshuru -- eneo ambalo lilikuwa ngome kuu ya waasi karibu na mpaka wa Uganda.
Bwana Kabila amefanya safari ya urefu wa kilomita mia tisa kwa njia ya gari mashariki mwa Congo kuonyesha imani yake kuhusu kuimarika kwa usalama katika eneo hilo.
Amevitaka vikundi vingine vyenye silaha nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kujisalimisha, la sivyo vitashughulikiwa kama ilivyotokea kwa kikundi cha M23.
Eneo la Rutshuru lilikuwa chini ya udhibiti wa M23 kwa zaidi ya mwaka mmoja na wakaazi wa eneo hilo wameiambia BBC kuwa waasi hao waliwaua na kuwateka watu wengi.

Vita nchini Syria vyaathiri watoto

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeonya kuwa vita nchini Syria vimesababisha kuharibu watoto kimwili na kisaikolojia.
Watoto wakiwa mbele ya jengo lililoteketezwa Syria
Wakimbizi watoto walio katika umri wa kwenda shule ambao wamekimbilia katika nchi jirani wameendelea kukosa elimu na wanalazimika kufanyakazi ili kujikimu.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi limesema watoto wapatao 300,000 wanaoishi nchini Lebanon na Jordan huenda wakakosa masomo ifikapo mwishoni mwa mwaka 2013.
Wengi wa ambao hawaendi shuleni wanakwenda kufanyakazi kwa muda mrefu wakipata malipo kidogo, wakiwa na umri mdogo wa hata miaka saba.
Zaidi ya nusu ya wakimbizi wa Syria milioni 2.2 ni watoto, wengi wakikabiliwa na hatari kubwa na hata nje ya eneo la vita.
Hatari hizo ni pamoja na athari za kimwili na kisaikolojia.
Akizindua ripoti hiyo, Kamishina wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, Antonio Guterres alisema: "Kama hatutachukua hatua haraka, kizazi cha watu wasio na hatia kitaishia kufa kutokana na vita."
Utafiti huu ni mpya kabisa na unajaribu kuonyesha madhara makubwa kwa watoto kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vilivyodumu kwa miaka mitatu. Madhara hayo ni kwa watoto walio ndani na nje ya mipaka ya Syria.

Friday, November 29, 2013

KWA TAARIFA YAKO : JE WAJUA KWANINI JACKSON BENTY ANAJIITA MTAKATIFU?

Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa karibu katika kipengele chetu maalumu ''KWA TAARIFA YAKO'' ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutukia lakini yawezekana huijui pia yawezekana ilitukia ukawa unaijua lakini GK ikawa imesahau mahali au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuweka comment yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu

Jackson Benty akiimba katika mkutano wa Injili wa Ufufuo jijini Arusha hivi karibuni.
KWA TAARIFA YAKO leo hii ni kuhusu mwimbaji nyota wa injili nchini anayeitwa Jackson Benty kutoka jijini Arusha, ni mwimbaji ambaye amekuwepo kwa muda mrefu sasa katika tasnia ya kueneza neno la Mungu kwa njia ya uimbaji na amefanyika baraka kwa watu wengi wanaosikiliza nyimbo zake.KWA TAARIFA YAKO je unajua mwimbaji huyu kwasasa anamtumikia Mungu katika kanisa la Ufufuo na Uzima la mchungaji Josephat Gwajima jijini Arusha?

Jackson ambaye amekuwa akipata mialiko ya kihuduma katika kanisa hilo hasa makao makuu yake Kawe jijini Dar es salaam, alianza rasmi ndani ya kanisa hilo mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa injili ulioandaliwa na kanisa hilo huko jijini Arusha.KWA TAARIFA YAKO kama ilivyo makanisa mengi yanavyojipangia utaratibu wao ndivyo ilivyo kwa kanisa la Ufufuo na Uzima ambao mafundisho ya neno la Mungu ni kipaumbele cha kwanza unapojiunga, ambapo waumini wake wako katika madaraja mbalimbali ya utumishi kuanzia cheo cha potential shepherd cheo cha chini kabisa ambacho ndio ameanza nacho mwimbaji huyo.

Jackson Benty akimsifu Mungu katika kanisa la Ufufuo Arusha.
KWA TAARIFA YAKO Benty ana nyimbo nyingi zinazopendwa na watu kama uninyanyue, saa sita mchana, Ndiwe Mungu, Nipe raha na nyingine nyingi lakini pia ukiangalia katika baadhi ya makasha ya album zake Jackson amejiita St.Jackson Benty akimaanisaha Mtakatifu Jackson Benty alipoulizwa imekuwaje kujiita hivyo, Jackson amesema Mungu anapendezwa na watakatifu waliopo duniani ambao kat yao naye ni mmoja wapo. KWA TAARIFA YAKO Jackson Benty anajiandaa kutoa album mpya ikimpendeza Mungu hivi karibuni.

Habari na Gospel kitaa blog

KWAYA YA KWETU PAZURI WAKO NCHINI ZAMBIA

Ambassadors of Christ wakiimba katika tamasha la pasaka jijini Mbeya mapema mwaka huu.

Kwaya ya Ambassadors of Christ kutoka Kigali nchini Rwanda maarufu kama Kwetu Pazuri wapo nchini Zambia kwa ziara ya siku tano ukiwa ni mwaliko wa kanisa la Wasabato Libala la jijini Lusaka ambapo kwaya hiyo itashiriki katika maonyesho makubwa matatu nchini humo yanayotarajiwa kuanza siku ya jumamosi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kundi hilo matamasha hayo ambayo yatakuwa na viingilio ili kusaidia ujenzi na huduma ya kanisa la Libala yatafanyika katika ukumbi wa Blessing centre kisha uwanja wa mpira wa Levy Mwanawasa uliopo Ndola na kumalizia katika ukumbi wa New Government complex siku ya tarehe 2. Kwaya hiyo ambayo ilipata umaarufu sana nchini Tanzania mwaka 2011 kutokana na album yao ya Kwetu pazuri, imekuwa ikipata mialiko katika nchi mbalimbali za Afrika ambako wameonyesha kiu ya kuwaona waimbaji hao.

Ambapo kwa mwaka huu Ambassadors walishiriki tamasha la pasaka nchini Tanzania, tamasha ambalo hata hivyo liliwaweka katika wakati mgumu na makanisa ya kisabato nchini kutokana na kukubali kushiriki tamasha hilo, lakini pia walikuwa nchini Uganda pamoja na Goma nchini Kongo ambako wameshiriki katika matamasha mbalimbali ya kusaidia huduma za makanisa ya Kisabato.

Uwanja wa Levy Mwanawasa ulipo Ndola nchini Zambia,ambapo Ambassadors of Christ wataimba siku ya jumapili.

Habari na Gospel kitaa blog

Waandamanaji Thailand wavamia jeshi

Mamia ya waandamanaji nchini Thailand waliingia kwa nguvu katika makao makuu ya jeshi mjini Bangkok, ikiwa ni siku ya sita tangu kuanza kwa maandamano dhidi ya serikali.
Waandamanaji Thailand
Msemaji wa jeshi amesema waandamanaji walivunja kufuli la mlango mkuu na kuingia katika eneo la makao makuu hayo ya jeshi. Baadaye waliondoka.
Alhamisi, Waziri Mkuu Yingluck Shinawatra aliwataka waandamanaji kuacha maandamano mitaani, ikiwa ni baada ya waziri mkuu huyo kushinda kura ya kutokuwa na imani naye iliyopigwa bungeni.
Lakini kiongozi wa waandamanaji Suthep Thaugsuban amekataa ombi hilo.
"Hatutaacha waendelee na kazi," mbunge mwandamizi wa zamani wa upinzani alisema hayo katika hotuba yake, Alhamisi.
Waandamanaji wapatao 1,000 waliingia kwa nguvu katika viwanja vya makao makuu ya jeshi mjini Bangkok.
Msemaji wa jeshi Kanali Sansern Kaewkamnerd amesema waandamanaji hawakuingia katika majengo.
Mwandishi wa BBC, Jonah Fisher, ambaye yupo katika eneo la tukio, amesema waandamanaji walikusanyika nje ya jengo wakisikiliza hotuba za viongozi wao waliokuwa katika jukwaa walilojenga.
Walikuwa wakiomba jeshi liwaunge mkono waandamanaji. "Tunataka kujua jeshi liko upande gani," Shirika la Habari la Uingereza, Reuters lilimkariri mmoja wa waandamanaji akisema hivyo.
Serikali imewataka waandamanaji kufanya mazungumzo-lakini ombi hilo limekataliwa.
Mwandishi wetu ameelezea hali hiyo kuwa nzuri na kusema serikali inaonekana kuepuka malumbano.

JK auzindua Mkoa wa Simiyu

Rais Jakaya Kikwete.PICHA|MAKTABA 
Na Frederick Katulanda na Faustine Fabian, Mwananchi
Simiyu. Rais Jakaya Kikwete amezindua Mkoa mpya wa Simiyu na wilaya zake huku akisimikwa kuwa Mtemi wa Kisukuma na kupewa jina la MunguBhanu lenye maana ya Mungu watu.
  Katika uzinduzi  huo uliofanyika juzi jioni kwenye Uwanja wa Mashujaa wa Bariadi Mjini na kuahirishwa baada ya  mvua kunyesha, Rais alieleza kuwa lengo la Serikali katika uanzishaji mikoa hiyo na wilaya zake ni kusogeza huduma karibu na wananchi.
  Hata hivyo, sherehe hizo ziliendelea jana asubuhi ambapo Rais Kikwete alisimikwa kuwa Mtemi wa Kisukuma, shughuli zilizoambatana  na maombi ya kuomba baraka ya mvua, hekima, utajiri na neema kwa ushirikiano wa wazee wa jadi ambao ni watemi wa Kabila la Kisukuma mkoani humo.
Zoezi la kuuombea baraka Mkoa wa Simiyu pamoja na kuusimika kijadi, liliendeshwa na Watemi Charles Doto Itale wa Bujashi akiwa pamoja na Mtemi Andrew Chenge (Itilima) Mbunge wa Bariadi Mashariki, Wenseslaus Seni (Kanadi), John Ngemela (Magu) waliomvisha joho na kumkabidhi Utemi  Rais Kikwete.
Mkoa wa Simiyu ulianzishwa rasmi mwaka jana na kuwa mkoa wa nne kati ya mikoa iliyogawanywa katika maeneo mbalimbali ikiwamo mikoa ya  Geita, Njombe pamoja na Katavi hivyo kuifanya Kanda ya Ziwa kuwa na jumla ya mikoa sita.
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia alieleza kuwa Serikali imetenga Sh17 bilioni kwa ajili ya mkoa huo fedha ambazo amedaiwa ni kwa ajili ya kujenga miundombinu pamoja na nyumba za watumishi hivyo alitoa wito wa matumizi yaliyokusudiwa.

Njia mpya ya Reli Afrika Mashariki

Njia hii ya reli itaunganisha Kenya na kanda nzima ya Afrika Mashariki na eneo la maziwa makuu
Kenya imezindua rasmi ujenzi wa njia ya Reli itakayounganisha kanda ya Afrika Mashariki na eneo la maziwa makuu ujenzi utakaofadhiliwa na serikali ya China.
Reli hiyo itaunganisha Kenya na Sudan Kusini, DR Congo na Burundi.
Sehemu ya kwanza ya njia hiyo ya reli , itaunganisha bandari ya Mombasa na Mji mkuu Nairobi na kupunguza muda wa safari kati ya miji hiyo kutoka masaa 15 hadi masaa manne tu.
Huu bila shaka ndio utakuwa mradi mkubwa Zaidi kuwahi kujengwa tangu nchi hiyo kujipatia uhuru miaka 50 iliyopita.
Mradi huo utagharimu dola bilioni 5.2 kiasi kikubwa cha pesa hizo kikitolewa na Uchina.
Baadhi ya wakenya wanalalamika kuwa tenda hiyo imetolewa kwa kampuni ya kichina kwa njia isiyofaa.
Rais Uhuru Kenyatta katika hafla ya uzinduzi huo amesema kuwa mradi huu ndio utakuwa kumbukumbu kubwa ya utawala wake Kenya.
Mkataba wa ujenzi wa njia hiyo ya reli, ulifikiwa kati ya Rais Kenyatta na mwenzake wa China Xi Jinping mnamo mwezi Agosti mjini Beijing.
Pia kuna matumaini kuwa njia hiyo ya reli itapunguza msongamano mjini Mombasa moja ya bandari yenye shughuli chungu nzima barani Afrika.
Njia ya reli iliyoko sasa, ni ile iliyojengwa enzi za ukoloni.
Baada ya kukamilika kwa sehemu ya kwanza ya reli hiyo mjini Nairobi, mwaka 2017, itaendelezwa hadi Magharibi mwa DRC hususan mjini Kisangani, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.
"Tunachokifanya hapa leo, kitaleta mageuzi makubwa sio nchini Kenya tu bali katika kanda nzima ya Afrika Mashariki,’’ alisema Rais Kenyatta akitaja mradi huo kama jambo la kihistoria.

Aliongeza kusema kuwa mradi huu ni moja ya miradi mikubwa katika maono yake ya maendeleo itimiapo mwaka 2030 kuboresha hali ya miundo msingi nchini humo.

Baregu aitahadharisha Chadema kuhusu Zitto

“Tuhuma zinazotolewa dhidi ya Zitto na wenzake kwamba wamenunuliwa na chama fulani cha siasa zinahitaji maelezo na vielelezo vya kina ili kuwaaminisha wengi. Nasema hivi kwa sababu historia yao inadhihirisha kuwa wana uchungu na chama chao. Chama kinachoongozwa kwa demokrasia na kinachotarajiwa kushika madaraka ya kuongoza nchi, lazima kionyeshe uwezo mkubwa wa kuvumiliana, kutafakari, kusamehe, kuaminiana na kujenga umoja wenye lengo la kuelekea kusudio lake.” Baregu  
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu amewataka viongozi wa chama hicho kutafakari na kudhibiti madhara yanayoweza kukikumba hasa baada ya hatua yake ya hivi karibuni ya kumvua nyadhifa zote, Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na wenzake wawili.
“Bahati nzuri wamevuliwa uongozi siyo uanachama, binafsi nadhani  viongozi wanatakiwa kutafakari na kudhibiti madhara zaidi kwa chama, wakishupaza shingo, lolote litakalotokea watakuwa ni sehemu ya lawama,” Profesa Baregu alisema Dar es Salaam jana.
Zitto, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba walivuliwa uongozi Novemba 22 mwaka huu, kwa tuhuma za kuandaa waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013, uliolenga kufanya mabadiliko makubwa ya kiuongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho kinyume na katiba, sheria na itifaki za chama.
Profesa Baregu alisema pamoja na viongozi hao kuvuliwa madaraka, mema waliyokifanyia chama hicho hayawezi kuyeyuka na kwamba makosa yao yasikuzwe kiasi cha kufuta mazuri yao katika kujenga chama hicho.
“Ni vigumu kuamini kwamba makosa ya Zitto, Dk Kitila na Samson Mwigamba yanaweza kuyeyusha mema waliyokifanyia chama kama barafu inavyoyeyuka juani.”
Profesa Baregu ambaye alikuwapo katika kikao kilichowavua uongozi Zitto na wenzake alisema kinachotakiwa kufanyika sasa ni kujenga uhusiano ndani ya chama na hasa kipindi hiki cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu wa ndani ambao umeanza Novemba 22 na unatarajiwa kumalizika Juni mwakani.
Alitaka hatua dhidi yao zizingatie Katiba ya chama hicho ili kuhakikisha kuwa hazivurugwi na mamlaka nyingine zilizopo ndani ya Chadema akisema mkutano wa Baraza Kuu unaweza kubadili uamuzi wa Kamati Kuu.
“Kinachotakiwa kufanywa ni kuwatangazia wanachama misingi, taratibu na kanuni za kuzingatia katika harakati zao  ili kuondoa hali ya watu kufanya mambo kwa kificho,” alisema na kuongeza:
“Ni wazi wengi wapo katika kampeni, ichukuliwe kuwa walioshughulikiwa wamebambwa na iwe njia ya kuonyesha ukomavu katika kustahamiliana.”
Alisema asingependa kuona siasa za kulipizana visasi na kusisitiza kwamba hata kama mwanachama ana chuki binafsi na mwenzake, hatakiwi kutumia chuki hiyo kumhukumu.
“Tuhuma zinazotolewa dhidi ya Zitto na wenzake kwamba wamenunuliwa na chama fulani cha siasa zinahitaji maelezo na vielelezo vya kina ili kuwaaminisha wengi. Nasema hivi kwa sababu historia yao inadhihirisha kuwa wana uchungu na chama chao. Chama kinachoongozwa kwa demokrasia na kinachotarajiwa kushika madaraka ya kuongoza nchi, lazima kionyeshe uwezo mkubwa wa kuvumiliana, kutafakari, kusamehe, kuaminiana na kujenga umoja wenye lengo la kuelekea kusudio lake.”
LwakatareMkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare alisema chama hicho kipo imara na hakiwezi kuyumba kwa sababu ya uamuzi huo.
Lwakatale ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho alisema: “Mfumo wa ulinzi ndani ya chama upo imara, yakitolewa maelezo na ngazi za juu kinachofuata baada ya hapo ni utekelezaji.”
Alisema kilichotokea ni kitu cha kawaida na ni mwanzo wa chama kujiimarisha.
Temeke wapinga
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu na Baraza Kuu la Chadema hicho Wilaya ya Temeke wamepinga hatua iliyochukuliwa na Kamati Kuu ya kuwavua nyadhifa viongozi hao.
Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Temeke, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu, Joseph Patrick aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mgogoro huo haulengi kujenga chama, bali unakibomoa.
“Chama chetu kimekuwa na tabia ya kuingia kwenye migogoro kila panapokaribia uchaguzi wa ndani. Hii inasababisha kuchafuana na kutukanana miongoni mwetu kiasi cha kuitana wahaini, wasaliti na wengine kuwaita wenzao wanatumika kwa lengo la kuwadhoofisha mbele ya wanachama,” alisema na kuongheza:
“Tumeona mifano mingi ya namna hii. Wakati Chacha Wangwe akiwa hai alipotangaza kuwania uenyekiti, mgogoro wa namna hii ulijitokeza, aliitwa majina yote na hakuwahi kusemwa vizuri kwenye chama, hakuchafuliwa na watu walio nje ya chama, bali viongozi wenzake waliotofautiana kimsimamo.”
Alisema hali hiyo ilijitokeza pia kwa Zitto alipotangaza kuwania uenyekiti kama ilivyokuwa wakati wa chaguzi za viti maalumu na mabaraza ya chama.
Alisema ni vyema viongozi wakaitisha mkutano mkuu wa dharura na kuwaeleza wanachama mambo mbalimbali ikiwamo ni kwa nini wameamua kusambaza waraka ambao alisema unakidhalilisha chama badala ya waliouandika.
Katibu Chadema ahojiwa
Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Herry Kilewo amehojiwa na Polisi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kutokana na madai ya Zitto kutishiwa kuuawa.Katika mahojiano hayo, Kilewo aliongozwa na Mwanasheria wake, Mussa Mfinanga, Mwanasheria wa Chadema John Malya na pia alikuwapo Diwani wa Ubungo, Boniface Jacob. Mfinanga alisema Novemba 11 mwaka huu, chombo kimoja cha habari kiliripoti kuwa Zitto ametishiwa kuuawa na mteja wake Kilewo.
Mfinanga alisema baada ya madai hayo, Jeshi hilo lilimwita Zitto kutoa maelezo yake na kisha kuona haja ya kumhoji Kilewo shutuma hizo. Alisema mteja wake amejidhanini mwenyewe na yupo nje kwa dhamana bila ya masharti yeyote.
Msemaji wa Polisi, Advera Senso alikiri kuhojiwa kwa Kilewo akisema ni kawaida kwa jeshi hilo kumuita mtu na kumhoji kwa mujibu wa taratibu na sheria zake.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Beatrice Moses, Pamela Chilongola na Editha Majura.

Julius Malema ana kesi ya kujibu

Mwanasiasa wa upinzani nchini Afrika Kusini, Julius Malema ameshindwa katika juhudi zake za kutaka kesi ya ufisadi dhidi yake itupiliwe mbali huku akikabiliwa na tisho la kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo mwaka ujao.
Melema akiwa mahakamani
Kiongozi huyo wa zamani wa tawi la vijana la chama tawala ANC ameshitakiwa kwa makosa ya kutengeza pesa kwa njia haramu , udanganyifu na kujihusisha na mitandao ya uhalifu.
Jaji Ephraim Makgoba alisema kuwa kesi itaanza kusikilizwa tarehe 30 mwezi Septemba mwaka 2014.
Anadaiwa kupokea dola za kimarekani, 392,000 kutokana na mikataba na maafisa wa serikali , madai anayoyakanusha.
Mamia ya wafuasi wa chama kipya cha Malema, (Economic Freedom Fighters), walikusanyika katika mahakama kuu ya Polokwane mjini Limpopo kusikiliza uamuzi wa jaji.
Wafuasi hao waliokuwa wamebeba vuvuzela na virungu, waliimba nyimbo za kumpinga Rais Jacob Zuma.
Jaji alisema kuwa Melema atafikishwa mahakamani pamoja na washtakiwa wenza wanne hadi labda kiongozi wa mashitaka atakapoamua kumwondolea kesi hio.
Serikali inadai kuwa Malema na wenzake wajiwakilisha ili waweze kupata kandarasi ya serikali ya thamani ya dola milioni 5.
Lakini Malema anasema kuwa mashitaka dhidi yake ni njama ya kisiasa kumponza.
Kucheleweshwa kwa kesi hiyo ina maana kuwa Melema hatajihusisha na kampeini za uchaguzi mkuu mwaka ujao.
Malema anasema ikiwa atachaguliwa atahakikisha kuwa mali ya Afrika Kusini itawafikia watu masikini na vijana wengi wasio na ajira wamevutiwa zaidi ya wito huu.
Alifurushwa kutoka chama tawala ANC mwaka 2012 kwa madai ya kuchochea migawanyiko chamani.

Wanaharakati nchini Misri wapinga adhabu

Makundi ya kutea haki za Binaadam nchini Misri yamekosoa uamuzi wa mamlaka kuhukumu kifungo cha miaka kumi na mmoja dhidi ya kundi Waandamanaji wa kike kutoka chama cha kiislamu nchini humo.
mamlaka imekuwa ikipambana na Waaandamanaji wa Misri
Wanawake 21 na wasichana walikamatwa mwezi uliopita baada ya kutokea maandamano mjini Alexandria yaliyokuwa yakimuunga mkono Kiongozi aliyeondolewa madarakani, Mohamed Morsi , huku Familia moja ikidai binti wa familia hiyo alikamatwa alipokuwa akipita eneo lenye maandamano akielekea shuleni.
Walithibitishwa kuwa na makosa ya kutumia nguvu na hujuma, lakini washtakiwa walikana wakidai kuwa maandamano hayo yalikuwa ya amani.
Mwandishi wa BBC jijini Cairo amesema kuwa hukumu iliyotolewa imedaiwa kudhihirika kwa kuwepo kwa utawala wa mabavu nchini humo

Mbunge wa Jimbola Kikwajuni azindua Nembo ya Chama cha Michezo cha Watu wenye Ulemavu Zanzibar













habari picha na Zanzibar news

MKUTANO WA KINANA TUNDUMA WAFUNIKA, MAELFU WAJITOKEZA, NAPE ABEBWA
















Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akihutumia maelfu ya wananchi katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mwaka, mjini Tunduma, wilayani Momba, jioni hii, Nov 28, 2013, akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM, kusikiliza kero za wananchi na kuzungumza nao njia ya kuzitatua, katika mkoa wa Mbeya.







Wananchi wakiwa wamembeba Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye wakati wa mkutano mkubwa wa hadhara uliohudhuria na maelfu ya wananchi katika uwanja wa shule ya msingi Mwaka mjini Tunduma wilayani Momba mkoani Mbeya, leo















Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye 'akihutoa dozi' alipohutubia katika mkubwa wa hadhara uliohudhuria na maelfu ya wananchi katika uwanja wa shule ya msingi Mwaka mjini Tunduma wilayani Momba mkoani Mbeya, leo














Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akitoa 'dozi' katika mkutano mkubwa wa hadhara uliohudhuria na maelfu ya wananchi katika uwanja wa shule ya msingi Mwaka mjini Tunduma wilayani Momba mkoani Mbeya, leo














Dk. Asha-Rose Migiro akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano uliofanyika  Uanja wa shule ya  Mwaka, Tunduma,leo




















Katibu wa NEC, Siasa na Uhisiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro (katikati mwenye  miwani) akiselebuka na wananchi kwenye mkutano, Uwanja wa shule ya  Mwaka, Tunduma leo