Licha ya Manchester United kupanda hadi nafasi ya tano, Kocha wa Chelsea, Antonio Conte amesema kwamba timu hiyo inaweza kumaliza katika nafasi nne za juu.
Conte alisema kwamba anaamini Manchester United bado ina nafasi kubwa ya kumaliza katika nafasi ya nne za juu kwenye Ligi Kuu England.
Timu hiyo ina tofauti ya pointi nne ikiwa nyuma ya Manchester City, lakini ina mchezo mmoja mkononi ikilinganisha na timu zilizo juu yake kwenye msimamo.
Conte alisema licha ya klabu hiyo kukabiliwa na mashindano mengine muhimu ya Ligi ya Europa mchezo wa robo fainali, lakini inatakiwa pia kufikiria kuhusu kumaliza katika nafasi nne za juu.
“Ninafikiri Manchester United wana nafasi kumaliza nafasi nne za juu,” alisema Conte alipokuwa akizungumza na gazeti la UK.
“Hata hivyo nina uhakika Manchester United wanajua hali hii. Wanatakiwa kupambana kuwemo kwenye nafasi hiyo muhimu ili waweze kushiriki mashindano ya Ulaya mwakani.”
Chelsea inakabiliwa na mechi ngumu za mwisho na leo watakutana na Manchester United, pia wana michezo ijayo na Manchester City, Arsenal na Tottenham.
Mchezo huu wa leo utakuwa wa historia kutokana na Kocha Jose Mourinho kukutana na timu yake aliyokuwa anaifundisha msimu uliopita.
“Sina tatizo na Manchester United. Ni katika tu hali ya mashindano kati yangu na Mourinho. Huu ni mchezo tu.”
Conte alisema, “Nitahakikisha kikosi changu kinaibuka na ushindi.”
No comments
Post a Comment