Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Monday, September 29, 2014

Funga kazi Bunge la Katiba leo

Na Daniel Mjema, Mwananchi
Dodoma. Wiki ya kufa au kupona kwa Bunge la Katiba, inaanza leo mjini Dodoma wakati wajumbe watakapoanza kuzipigia kura ibara na sura za Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

Shughuli hiyo itaanza huku kukiwa na hofu ya kutopatikana kwa theluthi mbili ya kura kwa wajumbe kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar inayotakiwa kwa mujibu wa kanuni, sheria na Katiba ya nchi.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, upigaji kura utafanyika kwa siku nne kuanzia leo hadi Oktoba 2, mwaka huu na iwapo itapitishwa, atakabidhiwa Rais kusubiri kupigiwa kura ya maoni mwaka 2016.

Habari kutoka bungeni zinadai kuwa wasiwasi wa kutopatikana kwa theluthi mbili uko zaidi upande wa Zanzibar hasa baada ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia Bunge hilo.

Hofu nyingine inatokana na suala la Mahakama ya Kadhi kutoingizwa, jambo ambalo limewagawa wajumbe huku kundi moja likiapa kupiga kura ya hapana iwapo haitaingizwa
Baadhi ya wajumbe wanataka Ibara ya 40 iingize vifungu vinavyotamka kuwapo kwa mahakama hiyo ili uamuzi wake kuhusu masuala ya ndoa, mirathi na talaka utambuliwe na sheria za nchi.

Hata hivyo, wajumbe wengine wanapinga suala hilo wakitaka ibara hiyo ibaki kama ilivyo ili Serikali isijihusishe na masuala ya uendeshaji wa jumuiya za dini.

Vilevile, Kifungu cha 22 (d) cha Rasimu kinachompa mwanamke haki sawa na mwanamume kumiliki ardhi kinapingwa vikali na baadhi ya wajumbe.

Pia baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar wanaona kuwa pamoja na kwamba karibu asilimia 90 ya mambo waliyokuwa wakiyalilia yameingizwa kwenye Katiba, bado Zanzibar haijapewa mamlaka kamili.

Hali hiyo imeifanya Kamati ya Uongozi chini ya Sitta kufanya vikao vya mashauriano mfululizo baina yao na wajumbe wa Kamati ya Uandishi ili kujaribu kuokoa jahazi.
Jana, vikao vya kamati 12 za Bunge ambavyo vilikuwa vianze saa 8:00 mchana vililazimika kusogezwa mbele kusubiri maelekezo kutoka Kamati ya Uongozi ambayo ilikuwa inakutana saa 9:00 alasiri.

« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment