Writen by
sadataley
12:47 PM
-
0
Comments
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
linawaalika kutafakari juu ya “Ufalme wa Mungu” katika kipindi cha Kwaresima
cha mwaka huu wa 2020. Baada ya kupokea baraka na mwanga wa Jubilei ya miaka
150 ya Ukristo Tanzania na Maadhimisho ya Mwezi Maalum wa Kimisionari Oktoba
2019, ni vema sasa tukaweka mkazo juu ya maana ya Ufalme wa Mungu kwa kutamka
na kueleza bayana.
Na
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, - Dar es Salaam.
UTANGULIZI:
Wapendwa wanafamilia ya Mungu:
Mapadre, Watawa, Waamini Walei na watu wote wenye mapenzi mema: “Neema na iwe
kwenu, na Amani zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo.” (2
Thes. 1: 2). Tunafurahi kuwaandikia ujumbe huu katika kipindi hiki maalum cha
Kwaresima, kipindi cha Neema na Baraka nyingi. Ujumbe wetu wa Kwaresima wa Mwaka
2019 ulilenga kuamsha roho, moyo, tabia, desturi na mila zetu za Kikristo za
kuthamini utu katika maisha ya kifamilia. Maisha ya familia yasipojengwa vyema
yanaweza kuwa kikwazo kwa Ufalme wa Mungu kufika katika maisha yetu. Tangu
mwanzo maisha na mahusiano katika familia yanahitaji mahusiano mazuri ili
ufalme wa Mungu ufike katika familia zetu.
Tunapomaliza
kutafakari juu ya familia, ambayo ni kiini cha kwanza cha uhai wa jamii na
kituo cha kawaida ambamo mtu anaweza kupata maendeleo ya kiroho na kimwili
(rej. Ecclesia in Africa, No. 85), tunawaalikeni kwa mara nyingine tena
kutafakari kwa pamoja ujumbe wa mwaka huu usemao “Ufalme wako Ufike.” Kwa
kuzingatia hayo, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linawaalika kutafakari
juu ya “Ufalme wa Mungu” katika kipindi cha Kwaresima cha mwaka huu wa 2020.
Baada ya kupokea neema, baraka na mwanga wa Jubilei ya miaka 150 ya Ukristo
Tanzania na Maadhimisho ya Mwezi Maalum wa Kimisionari Oktoba 2019, ni vema
sasa tukaweka mkazo juu ya maana ya Ufalme wa Mungu kwa kutamka na kueleza
bayana.
Siku
zote tutilie maanani kuwa Yesu mwenyewe aliishi katika jamii halisi kijijini
Nazareti, na akakubali hali, tabia na maisha ya jamii, huku akihubiri Ufalme wa
Mungu. Hivyo katika kipindi hiki tuendelee kutafakari kwa kina juu ya “Ukuu wa
Mungu”, na namna Neno la Mungu linavyokuza Ufalme wa Mungu na Mamlaka ya Watu;
na jinsi mazoezi ya kiroho yanavyoimarisha Ufalme huo. Tuombe tuendelee kukua
katika Kristo, kwa kuifanya mioyo yetu iwake mapendo yake. Aidha tuendelee
kuomba kwa ajili ya uongofu wa mioyo yetu ili iwe na hofu ya Mungu adumuye
milele, ambaye ufalme wake ni ufalme usihoharibika na mamlaka yake hudumu hata
mwisho.
SURA
YA KWANZA UFALME WAKO UFIKE Katika
Maandiko Matakatifu, Maneno “Ufalme wa Mungu” yanatoa tafsiri iliyojijenga juu
ya imani ya Kibiblia kuwa Mungu ndiye Mkuu, Bwana wa mabwana na Mtawala wa vitu
vyote (rej. Zab 103:19, 145:13). Hii ilitokana na ukweli kwamba, sura za kwanza
za kitabu cha Mwanzo zinaweka wazi mpango wa Mungu wa kuanzisha ufalme wake
ulimwenguni. Baada ya juhudi za shetani za kuvuruga mpango huo wa Mungu kwa
njia ya Adam na Eva (rej. Mwa 3:15), na baada ya vizazi vingi kupita, Mungu
alimwahidi Baba yetu wa imani Ibrahim, kuwa kwa njia yake mataifa yote
ulimwenguni yatabarikiwa; na kupitia yeye watapatikana wafalme (rej Mwa 12:1-3,
17:6). Kwa zaidi ya miaka 400 baadaye, Mungu aliwakomboa wana wa Israeli kutoka
utumwani Misri na kuwafanya “taifa teule”, “ufalme wa makuhani” na “taifa
takatifu” (Kut. 19:6).
AGANO
LA KALE: Mungu alikusudia kulifanya Taifa
la Israeli kuwa mfano wa Ufalme wake ujao kwa ulimwengu mzima. Kabla wana wa
Israeli hawajaingia nchi ya ahadi ya Kanaani, Musa aliwaambia kuwa watapata
mfalme ambaye atateuliwa na Mungu (rej. Kum 17:14-20). Kufuatia kuingia kwao
nchi ya Kanaani chini ya uongozi wa Joshua, na kipindi kirefu cha Waamuzi (1400
– 1050 K. K.), wana wa Israeli walimpata Sauli ili awatawale kama mfalme wao wa
kwanza (rej 1Sam 10:24). Hata hivyo, Sauli hakumtii Mungu na kwa sababu hiyo
Mungu aliamua kumwinua Daudi badala yake (rej. 1 Sam. 16). Baada ya Daudi
kuteuliwa kuwa mfalme wa Waisraeli (rej. 2Sam. 5:3-4), aliutwaa mji wa
Yerusalemu uliokuwa umetekwa na maadui na kulirudisha sanduku la Agano na Mungu
wao kwenye mji huo. Daudi alitamani kumjengea Mungu nyumba, yaani hekalu la
kudumu badala ya tabernakulo pekee (rej. 2Sam. 7:1-3).
Kama
jibu kwa matamanio hayo, Mungu aliahidi kumjengea Daudi “nyumba” na kuanzisha
ufalme wa uzao wa Daudi milele (rej. 2Sam. 7:4-16). Basi, mpango wa Mungu wa
kuanzisha ufalme ulimwenguni ulifikia hatua hiyo mpya kwa njia ya Agano hilo la
milele na Daudi. 1.1.3 Hata utawala wa kifalme wa Waisraeli ulipoanza
kutetereka, bado manabii walisimamia Agano la Mungu na Daudi. Manabii hao
waliwatangazia wana wa Israeli matumaini ya wakati ujao ya ujio mpya wa Mfalme
wa uzao wa Daudi, yaani Masiya, ambaye angeanzisha utawala wa Haki, Amani na
Furaha (rej. Isa 9:6-7, 11:1-10, 40:9-10, 52:7, Dn. 7:13-14, Zek 9:9). Agano la
Mungu na Daudi linatimia kwa kuzaliwa kwake Yesu (rej. Isa 9:2-7, Lk. 2:1-14,
Mt. 1:1- 25). Yesu ndiye Mfalme ambaye Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi
baba yake (rej. Lk 1:32).
AGANO
JIPYA.: Katika Agano Jipya, neno “UFALME”
laweza kufasiriwa kama “milki” au “utawala”. Ni Ufalme wa Mungu ambao uko mbele
yetu. Umeletwa karibu na Neno aliyemwilishwa (rej. Yn. 1:14); unatangazwa
katika Injili zote na umedhihirika katika kifo na ufufuko wa Kristo. Utume wa
Yesu unaanza kwa tangazo la ufalme wa Mungu kuwa umekaribia (rej. Mk. 1:15, Mt.
3:2, 4:17, 23, 9:35, Lk. 4:18-19.) Tangazo hili ni kiini cha ujumbe wa mahubiri
ya Yesu na ni nukuu kutoka kwa Nabii Isaya (rej. Isa. 61:1-2). Ujio wa ufalme
wa Mungu umekuwa pia ujumbe mkuu katika mahubiri ya wafuasi wa Yesu (rej. Mt.
10:7, Lk. 9:2, 10:9).
Sala
ya Baba yetu ambayo Yesu anawafundisha wafuasi wake imebeba ombi la msingi,
“ufalme wako ufike…. duniani kama mbinguni” (rej. Mt. 6:20, Lk. 11:2). Sala hii
inadokeza kuwa ufalme huo bado haujafika kikamilifu duniani; ni ufalme ujao
katika utimilifu wake siku zijazo. Maneno “mapenzi yako yatimizwe” yanadokeza
kuwa ufalme ni Mapenzi ya Mungu yanayopaswa kutimizwa na wanadamu. 1.2.3 Ombi
hili pia linamaanisha ufalme wa Mungu tayari upo katika ukamilifu wake huko
mbinguni, hata kama bado haujakamilika duniani. Hata mafundisho ya Yesu mlimani
(rej. Mt. 5:2-12) yanaonyesha ufalme wa Mungu kama jambo ambalo bado lipo
mbali, na muda wake haujatimia. Lakini, katika utume wa Yesu wa uponyaji,
ufalme wa Mungu upo tayari na umeanza kuonekana (rej. Mt. 12:28, Lk. 11:20).
Kwa maneno mengine, ufalme wa Mungu umeshafika kwa ujio wa Yesu Kristo. Yeye
amepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Lakini inatupasa kuendelea kusali
“ufalme wako ufike” kwa sababu hapa duniani wapo watu ambao bado hawamwamini
Yesu Kristo na hivyo hawajajiweka chini ya utawala wake, yaani utawala wa haki,
amani na maridhiano!
Yesu
alitumia neno “Ufalme wa Mungu” kama dhana msingi ya mafundisho yake. Tunasoma,
“Yesu alikuwa anakwenda kila mahali mkoani Galilaya akifundisha katika
masinagogi na kuhubiri Habari Njema juu ya ufalme wa Mungu. Aliponya kila namna
ya maradhi na magonjwa waliyokuwa nayo watu.” (Mt.4:23). Ufalme wa mbinguni ni
sehemu ya heri katika hotuba ya Yesu mlimani; “Heri walio maskini rohoni, maana
ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wanaoteswa kwa sababu ya kufanya atakavyo
Mungu, maana ufalme wa mbinguni ni wao.” (Mt. 5:3, 10). 6
Yesu
analitumia neno “ufalme” mara nyingi katika mafundisho yake ili kuelezea
utawala wa Mungu na mapenzi yake. Mara nyingi Yesu alitumia picha ya sherehe au
mlo wa pamoja au tafrija ili kufundisha juu ya ufalme wa mbinguni. Yesu
anasema, “Basi, nawaambieni kwamba watu wengi watakuja kutoka mashariki na
magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika
ufalme wa mbinguni” (Mt. 8:11). Ufalme wa Mungu unaonekana wazi katika
mafundisho na matendo ya Yesu. Maandiko Matakatifu yanaonyesha vigezo vya
Ufalme wa Mbinguni kwa kadiri vinavyodhihirika katika maisha ya Kristo. Kwa
mfano, pale Msalabani ni mtu aliyewapenda maadui zake; mtu ambaye haki yake ni
zaidi ya ile haki ya Mafarisayo; anayetoa nira yake kwa wale wote wanaobeba
mzigo wake na anayewaombea wote wanaomdhihaki (rej. Lk. 23:34). Anaonyesha
kwamba msalaba sio kikwazo au pingamizi katika njia ya kwenda mbinguni, bali ni
mwaliko wa ufalme wake.
Maisha
na mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo kwa kujumuishwa na Sala ya Bwana,
vyatualika sisi kujumuika naye kama watumishi katika Ufalme wa mbinguni.
Hatimaye, tuweze kufanya kazi naye katika kusaidia mapenzi ya Mungu kufanyika
duniani, kama ambavyo tayari yanafanyika mbinguni. Yesu anatufundisha njia ya
kuuendea ufalme wa Mungu bila kujali tofauti zetu za kikabila, kitaifa, rangi,
kidini, kiitikadi na kijinsia (rej. Gal. 3:28; 1 Kor 1:10-13).
KWA
NINI TUNASALI “UFALME WAKO UFIKE?” Katika
kipindi hiki cha Kwaresima, Tunasali “ufalme wako ufike” kwa ajili ya
mwendelezo wa kueneza ufalme wa Mungu duniani, ili watu wote wajiweke kwa hiari
yao chini ya utawala wa Yesu Kristo (rej. Flp. 2:6-11), na hivyo watimize
mapenzi ya Mungu hapa duniani kama yanavyotimizwa katika ukamilifu wake wote
huko mbinguni. Tunamwomba Mungu ili abadili mioyo ya maadui wake na kuwaleta
kwake ili wamkiri Yesu Kristo na kumwamini kuwa ni Bwana wao (rej. Zab. 110) na
kujiweka chini ya maongozi yake. Tunaomba kwa ajili ya ujio wa siku ambapo
uovu, dhambi na uasi wote dhidi ya Mungu katika maisha ya mwanadamu katika
nyanja zote utakoma; na hivyo haki, upendo, amani na maridhiano vitatawala.
Tunasali
Ufalme wa Mungu ufike, ili kila mtu aishi kadiri Mungu apendavyo. Wakristo
lazima kwa moyo radhi watafiti namna ya kuupokea utawala wa Kristo katika
maisha yao ya kila siku na huo utakuwa mwanzo wa kutimiza sala ya Bwana “Ufalme
wako ufike, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni.” Kwa mfano, makazi yetu
lazima yawe kimbilio la wakosefu, maskini, wenye maradhi, wanaoonewa,
wakimbizi, n.k. Urafiki wetu ukolezwe na neema, na shughuli zetu zote zifanyike
kwa ajili ya utukufu wa Kristo (rej. Kol. 3:17, 23).
Tunaposali
“Ufalme wako ufike, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni”, tunamwomba Mungu
atutumie sisi kuonyesha nguvu ya ufalme wake leo, na jinsi mambo yatakavyokuwa
hapo siku za usoni. Tukizingatia hilo, kutakuwa na jamii yenye kufuata sheria
na amri za Mungu; yenye umoja na mshikamano; inayozingatia haki na amani; na
hivyo kuwa na jamii yenye upendo isiyokuwa na migawanyiko. Kwa namna hiyo
tutaishi vizuri kama atakavyo Mungu (rej. Ufu 11:15). Ili kufikia hapo ni
lazima yaanzishwe mapambano thabiti kati ya “mwili na roho” (rej. Gal. 5:
16-25). Ni moyo ulio safi tu unaoweza kusema kwa ujasiri: “Ufalme wako uje.”
Yeye anayetenda haki, katika matendo yake, mawazo yake na maneno yake, anaweza
kumwambia Mungu: “Ufalme wako ufike.” (rej. Rum. 6: 12).
Sisi
ambao tayari ni wana wa Ufalme na tumejiweka chini ya utawala wa Kristo
tunaalikwa kuufanyia kazi ufalme wa Mungu ili kuwapa wengine mwanga wa Ufalme
huo. Kwa upande mwingine tunaalikwa kufanya kazi tukiwa na matumaini makubwa
kwamba juhudi zetu zitaleta mabadiliko, tukifahamu kuwa Bwana wetu atakuja
kuyaweka mambo yote sawa. Kwa kuwa pale ufalme wa Mungu unapoongezeka, watu wa
Mungu huwa “chumvi na mwanga” katika ulimwengu unaowazunguka (rej. Mt. 5:13-
16).
Katika
kipindi hiki cha Kwaresima, tunaomba “Ufalme wa Mungu” uzidi kudhihirika wazi
ulimwenguni ili kile anachotaka Mwenyezi Mungu
kiwe kile kinachopaswa kutokea. Tunaombea mapenzi ya Mungu yatimizwe
ulimwenguni, kwa nguvu ya Roho wa Mungu anayefanya kazi pamoja nasi na ndani
yetu; na hii inatudai ushiriki wetu na kujitoa kikamilifu. Tunaposali, “Ufalme
wako ufike,” tunasali kwa ajili ya ufalme (utawala) unaolinda daima uhuru
kamili wa mwanadamu na unaopinga nguvu zinazoenda kinyume na mapenzi ya Mungu
ulimwenguni. Uhuru wa mwanadamu unaotokana na ubinafsi, dhambi na uovu,
huletwao na tamaa za kibinadamu, huzalisha matendo na tabia ambazo ziko nje ya
mapenzi ya Mungu. Kwa mfano, kamwe si mapenzi ya Mungu kuwadhalilisha watoto,
yatima na wajane. Mambo hayo yanapotokea ni kwa sababu ya msukumo wa dhambi za
mwanadamu, kunakotokana na kutotii amri za Mungu, na si kwa sababu ya mapenzi
ya Mungu.
Tunasali
pia kwa ajili ya ufalme wenye nguvu kubwa ya kuzibadilisha nguvu ovu za mtu
mmoja mmoja, taasisi, na ulimwengu kwa kuanza na sisi wenyewe. Tunasali “Ufalme
wako ufike, utakalo lifanyike,” ili utawala wa hapa duniani na utumishi wa kila
namna uondokane na unyanyasaji; na msamaha umalize kabisa chuki; na kwamba
upendo wa ufalme wa Mungu, usambaze mwanga wa Kristo ili neema, usawa na huruma
vitawale katika kila eneo la maisha ya mwanadamu. Matokeo yake ni kuwa na jamii
inayolinda utu wa mwanadamu mwenye sura na mfano wa Mungu (rej. Mwa 1:26-27).
HITIMISHO
Tunaposali ili ufalme wa Mungu ufike
tunaomba ili ufalme wa shetani utokomezwe. Tunapenda kuona kwamba shetani na
nguvu zake, ujanja wake wote, ushawishi wake wa kiovu, uongo wake na uharibifu
wake wote unatokomezwa. Vitu vyote vya ulimwengu na tamaa zake mbaya havitoki
kwa Baba, bali vyatoka kwa yule mwovu. Ulimwengu pamoja na vitu vyake vyote
vyenye kutamanika unapita; lakini mtu atendaye mapenzi ya Mungu, ataishi
milele. (rej. 1Yoh. 2:15-17
SURA
YA PILI: NENO LA MUNGU LINAKUZA UFALME WA MBINGUNI: Lengo kuu la mahubiri na utume wa uchungaji katika Kanisa,
daima lilikuwa, linabaki, na litabaki kuwa lile ambalo Mtume Paulo analitamka
akisema:” Kwa hiyo navumilia yote kwa ajili ya wateule, ili nao wapate wokovu
katika Kristo Yesu, ndio utukufu wa milele” (2 Tim 2:10). Kuupokea wokovu na
utukufu wa milele, ndiko kuufanya Ufalme wa Mungu ufike. Mtume Paulo
anamwandikia Timotheo waraka huu akiwa gerezani jijini Roma wakati ambapo
anaonekana ameachwa na wengi wa marafiki zake (rej. 2Tim.1:15-18; 4:9-18) na
anakabiliwa na kifo (rej. 2Tim. 3:6-8). Hivyo Mtume Paulo anamtia moyo Timotheo
akimwambia “Nami katika hiyo (Injili) nimeteswa hata kufungwa kama mtenda
mabaya; Kwa ajili yake (Injili) navumilia mateso, hata nikifungwa minyororo
kama mvunja sheria. Neno la Mungu halikufungwa” (2 Tim. 2:9).
Neno
la Mungu ni tofauti na neno la mwanadamu. Mungu ndiye muumba wa mbingu na nchi
na kila kilichomo; hata mwanadamu aliumbwa na Mungu mwenyewe. Mungu aliumba
vitu vyote kwa Neno (rej. Mwa. 1:3-29). Hivyo, ni wazi kwamba Neno lake lina
nguvu ajabu kiasi cha kutoweza kuzuiliwa na kitu chochote; ni kwa Neno hilo
vyote vilifanyika na pasipo Neno kitu chochote kisingekuwepo ila Mungu mwenyewe
(rej. Yn. 1:2-3). Neno linapaswa kutangazwa kadiri ya amri ya Mungu mwenyewe
(rej. Mk. 16:15). Hivyo kwa Mkristo aliyepewa jukumu la kuhubiri Injili kwa
ujasiri na kuimarishwa na paji la Roho Mtakatifu katika Ubatizo na Kipaimara
(rej. Rum. 8:35- 37), ana jukumu la kuona kwamba ufalme wa Mungu unaenezwa bila
kukata tamaa, licha ya changamoto anazokutana nazo.
AGANO
LA KALE Katika agano la kale kuna mifano ya
kutosha ya manabii waliohubiri Neno la Mungu kwa ujasiri bila kujali dhuluma na
mateso waliyokutana nayo katika vifungo. Mungu aliponena na Musa na kumwambia
aende nchini Misri kuwakomboa watu wake na kuwapeleka Nchi ya Ahadi (rej. Kut
3:10), Musa katika hali ya kibinadamu alijaribu kuweka mnyororo juu ya Neno
hilo (rej. Kut 4:10). Pamoja na sababu alizozitoa mwishowe Musa alikwenda
nchini Misri kadiri ya Neno la Mungu kwani hakuna kinachoweza kulifunga Neno la
Mungu. Huko Musa alikutana na vikwazo vingi vilivyokuwa na lengo la kumkatisha
tamaa ili ujumbe wa Mungu aliopeleka usitimie na lengo lisifikiwe. Lakini
pamoja na hayo yote, wana wa Israeli walitoka nchini Misri na kuelekea katika
Nchi ya Ahadi; na kila aliyejaribu kulizuia Neno la Mungu kutimia alipata
mapigo makali (rej. Kut 7:8-11:1-9). 2.1.2 Ingawa hatuambiwi iwapo Nabii Isaya
aliwahi kuhubiri akiwa mfungwa lakini mazingira hatarishi ya kisiasa ya wakati
wake yalikuwa ni kama kifungo kwake.
Nabii
Isaya alihubiri katika kipindi kigumu ambapo yeye pamoja na taifa zima la
Israeli lilipitia shida za kisiasa hasa
zile zilizosababishwa na uvamizi na ukandamizaji wa Waashuru wakati wa utawala
wa Ahazi na Hezekia, wafalme wa Israeli na Yuda (736-700 K.K). Lakini pia Nabii
Isaya hakuogopa hata kidogo kuwakemea wafalme na makuhani ambao walikosa
uaminifu kwa Mungu, na alitamka waziwazi hukumu ya Mungu juu ya ukaidi wao bila
kujali mateso ambayo yangempata mtu yeyote aliyemdhalilisha mtu wa cheo cha juu
kama vile mfalme. Aidha Nabii Isaya kwa ujasiri mkubwa alilionya taifa la
Israeli kwamba kwa sababu ya kukosa uaminifu kwa Mungu lingeadhibiwa vikali na
Mungu mwenyewe (rej. Isa. 6:1-13). 2.1.3 Mfalme Ahazi kwa mfano, alikuwa hana
imani ya kutosha kwa Mungu. Hivyo alifanya mikataba ya kivita na mataifa jirani
ili kuwashinda maadui wa Israeli. Lakini Nabii Isaya alimwambia mfalme Ahazi
asiwaogope Waashuru na kwamba aombe ishara ya Imanueli, mfalme Masiya, ambayo
nabii alitabiri kutimia kwake (rej. Isa. 6:6-12) ila mfalme alikaidi na alipata
madhara makubwa.
Mfalme
Ahazi alikosa imani na uaminifu kwa Mungu, akategemea nguvu za muungano na
mapatano ya kijeshi zaidi na matokeo yake alipata madhara makubwa baadaye.
Lakini pia taifa lote la Israeli lilikosa imani na uaminifu kwa Mungu na hivyo
lilistahili adhabu na toba. Nabii Isaya alisisitiza kuwa Mungu mtukufu ni
“Mtakatifu wa Israeli” aliyejiunga na Israeli katika Agano ili amkomboe. Njia
ya kukombolewa kwake Israeli ni kumwamini Mungu, Mungu peke yake, katika haki
na ukweli. Na kwa sababu Israeli hakumwamini Mungu atahukumiwa na ataangamizwa.
Lakini waliobaki watamrudia Mungu na kuokoka (rej. Isa 4:3). Mfalme wao atakuwa
Masiya mwana wa Daudi, atakayeweka duniani ufalme wa amani na haki, na “dunia
itajawa na kumjua Mungu”, yaani watu wote watampenda na kumtii Mungu. Katika
unabii wake, Isaya hakuuma maneno! Alihubiri Neno la Mungu bila kuogopa hatari
zilizoonekana kumzonga au kumfunga asihubiri Neno la Mungu kwa ufasaha na
uwazi.
Nabii
Yeremia alijiona kuwa na umri mdogo hivyo hangeweza kutangaza Neno la Mungu (rej. Yer. 1:6). Pale nabii Yeremia alipojaribu kuweka
mnyororo ili asifanye kazi hiyo ya Mungu, Mungu alimthibitishia kuwa umri siyo
sababu ya kutotangaza Neno lake (rej. Yer. 1:7). Neno la Mungu halifungwi na
chochote hata umri mdogo. Lakini pia nabii Yeremia alikutana na mazingira ya
kifungo katika kuhubiri Neno la Mungu (rej. Yer. 32). Uaminifu na imani yake
kwa Mungu vilimtia nguvu. “Tazama, mimi ni Bwana, Mungu wa wote wenye mwili;
je, kuna neno gumu lolote nisiloliweza?” (rej. Yer. 32:27). Kwa maneno mengine,
“Neno la Mungu halifungwi minyororo.”
Katika
Mwaka wa kumi wa Zedekia, mfalme wa Yuda, ambao pia ulikuwa mwaka wa kumi na
nane wa Nebukadreza, nabii Yeremia alitabiri kuchukuliwa mateka kwa mji wa Yuda
na mfalme Nebukadreza. Jambo hili halikumpendeza mfalme Zedekia, hivyo nabii
Yeremia alifungwa gerezani ndani ya uwanda wa walinzi uliokuwa katika nyumba ya
mfalme wa Yuda. Hata hivyo nabii Yeremia aliendelea kuhubiri Neno la Mungu
angali kifungoni; kifungo hakikumzuia kuendelea na kazi yake (rej. Yer. 33).
Kama ilivyokuwa kwa Nabii Isaya vivyo hivyo na nabii Yeremia naye alikuwa na
ujasiri mkubwa katika kuutangaza ukweli wa Neno la Mungu. Mara kadhaa
alilumbana na wafalme Zedekia na Jehoiakimu katika kutetea Ukweli wa Neno la
Mungu. Hii inadhihirisha kuwa Neno la Mungu halifungwi minyororo, linavuma
katika mazingira yoyote kadiri ya mapenzi ya Mungu na si kwa matakwa dhaifu ya
wanadamu.
Nabii
mwingine aliyehubiri akiwa kifungoni ni Ezekieli. Nabii Ezekieli anadhaniwa kuwa mhubiri aliyewalenga
Waisraeli waliokuwa uhamishoni Babeli (593-571 K.K). Lakini inasemekana pia
kuwa kuna ujumbe aliutoa akiwa Palestina (rej. Eze. 2:1-3:9) na mwingine akiwa
utumwani Babeli (rej. Eze. 1:4-28, 3:10-15). “Haya! Enenda uwafikie watu hao
waliohamishwa, kwa watu wako, ukaseme nao, na kuwaambia, ‘Bwana Mungu asema
hivi’; kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia (rej. Eze. 3:11).” “Enenda
ukajifungie nyumbani mwako. Lakini wewe, mwanadamu, tazama, watakutia pingu,
nao watakufunga kwazo, wala hutakwenda nje kati yao. Nami nitaufanya ulimi wako
ugandamane na kaakaa lako, hata utakuwa bubu, wala hutakuwa mwonyaji kwao, kwa
kuwa wao ni nyumba yenye kuasi. Lakini hapo nitakaposema nawe, nitafumbua
kinywa chako, nawe utawaambia, ‘Bwana Mungu asema hivi, Yeye asikiaye na
asikie, naye akataaye na akatae’; maana wao ni nyumba yenye kuasi (rej. Eze.
3:24-27).” Hivyo, Neno la Mungu linawafikia watu wake hata kama wako kifungoni
au latokea kifungoni, lenyewe linapenya tu.
Pia
tundu la simba ambamo nabii Danieli alifungiwa jiwe kubwa, utukufu wa Neno la
Mungu ulidhihirika kwa Waisraeli. Baada ya kuamka asubuhi mfalme alikwenda nje
ya pango alimokuwa Danieli akalia na kuuliza kama Mungu wa Danieli alimwokoa.
Ndipo Danieli alipothibitisha kwa kusema kuwa Mungu alimtuma malaika ayafumbe
makanwa ya simba wasiweze kumdhuru hata kidogo. Mungu alinena na malaika,
akatenda muujiza wa kumwokoa Danieli uliosababisha ongezeko la imani ya Mfalme
Dario pamoja na watu wake (rej. Dan. 6). Hivyo Neno la Mungu halizuiliwi na
chochote kilichoumbwa naye. 2.1.8 Nabii Amosi alishindana na kuhani Amazia
ambaye alimkataza kuhubiri, ya kwamba hakuwa na haki ya kufanya hivyo. Amazia
aliyafanya haya kwa sababu Amosi alitabiri kuwa Mfalme Yeroboamu ataangamia kwa
upanga na Waisraeli watapelekwa utumwani. Utabiri huu haukumpendeza Amazia
hivyo aliamuru nabii Amosi aondoke Betheli na aende kuwatabiria watu wa Israeli
(rej. Am. 7:10-17). Lakini Amosi alimthibitishia Amazia kuwa yeye ni nabii
halali na kwamba ndiye aliyeteuliwa na Mungu alipokuwa mchungaji na mtunza
mikuyu kuwahubiria nyumba ya Israeli. Na papo hapo alimtangazia Neno la
Mwenyezi Mungu (rej.Am. 7: 16-17). Maandiko hayo yanaonyesha jinsi gani Neno la
Mungu haliwezi kuzuiliwa na yeyote au chochote.
AGANO
JIPYA: Yohane Mbatizaji alielewa umuhimu
wa kuupata Ufalme wa Mungu alipotoa mwaliko, “Tubuni kwa maana ufalme wa Mungu
umekaribia “(Mt. 3: 2)”. Yohane Mbatizaji akiwa gerezani alitafuta faraja ya
Neno la Mwenyezi Mungu. Aliamini kuwa Neno hilo litamfikia hata akiwa kifungoni
katika mateso na kwalo angepata amani. Hivyo, Yohane Mbatizaji aliwatuma
wanafunzi (rej. Mt. 11:2-6) kumwuliza Yesu ili apate kujua iwapo Yeye ndiye
yule ajae au wamtarajie mwingine. Jibu lililorudi ni ushuhuda wa Neno la Mungu
linavyoendelea kufanya kazi kati ya watu. Hivyo hakuna sababu ya kuwa na
mashaka nalo. Neno la Mungu linavunja mipaka ya kifungo na kusafiri kwa urahisi
bila ya pingamizi. Neno hilo halifungwi minyororo hata kama wale wanaolipokea
wamefungwa minyororo. Aidha kilichompeleka Yohane Mbatizaji kifungoni na kuuawa
ni Neno la Mungu ili asiendelee kulitangaza (rej. Mt. 14:1-12). Hata hivyo,
akiwa kifungoni Neno la Mungu liliendelea kutangazwa na wengine (rej. Mk.
6:6-29).
Yesu
alifungua Hotuba ya Mlimani kwa Heri nane. Heri hizo zinaunganisha tabia
anayokuwa nayo mtu muda uliopo sasa na maisha yajayo. Heri ya kwanza na ile ya
mwisho (Mt. 5: 3, 10), zote hueleza kuwa ufalme wa Mungu tayari upo hivi sasa
miongoni mwetu na kati yetu. Heri sita ambazo zimo (Mt. 5: 4-9) huonyesha
Ufalme utafikia ukamilifu wake siku ya mwisho. Heri za mwisho, (Mt. 5: 10-11)
ni juu ya ulazima wa kuteseka kwa ajili ya Injili na baraka na utukufu wenye
nguvu ya pekee tunavyovipata katika maisha yetu. Hakuna heri ambayo wanadamu
wanaweza kuifikia inayokwepa mateso.
Katika
Karamu ya Mwisho Yesu alisema,
“Sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa upya katika
ufalme wa Mungu” (Mk. 14: 25). Yesu Kristo mwenyewe akiwa katika praitorio
anazungumza ukweli wa Neno la Mungu kwa ujasiri mkubwa (rej. Yn. 18-19:1-15).
Kwa mfano, baada ya kuulizwa habari za mafundisho yake, Yesu Kristo anasema
waziwazi kwamba hakuficha chochote. Alihubiri Neno la Mungu kwa uwazi hivyo
hakuna sababu ya kuendelea kumhoji. Kwa hili Bwana wetu Yesu Kristo anapigwa
kofi lakini naye anamjibu aliyempiga kwamba, aliyoyazungumza ni ukweli mtupu na
kulikuwa hakuna sababu ya Yeye kupigwa kofi. Alisema haya bila kujali hatari ya
kupigwa kofi tena. Neno la Mungu halifungwi kwa kupigwa kofi, au mijeledi, au
kutemewa mate. Aidha Neno la Mungu alilolifundisha Bwana wetu Yesu Kristo na
ukweli alioutangaza ndio uliomfikisha kwenye mateso makali na kifo cha Msalaba.
Hata hivyo, siku ya tatu alifufuka na Neno la Mungu linaendelea kutangazwa
(rej. Mt. 28:1-10).
Mitume
Petro na Yohane na wengine wengi walianza kulitangaza Neno la Mungu baada ya
Pentekoste; lakini walipelekwa gerezani kwa kuwa walilihubiri Neno la Uzima la
Bwana wetu Yesu Kristo. Wangali bado gerezani, walipelekwa mbele ya baraza
kuhojiwa. Kwamba ni kwa nguvu ya nani wanatenda? Mtume Petro kwa ujasiri mkubwa
anazungumza juu ya habari za Yesu ambaye Wayahudi na viongozi wao
walimsulubisha kuwa ndiye chanzo cha nguvu na mamlaka yao. Kristo ni jiwe
walilolikataa waashi na limekuwa jiwe kuu la pembeni (rej. Mdo. 4:1-22). Neno
la Mungu halifungwi minyororo!
Shemasi
Stefano naye anapelekwa mbele ya baraza la Wayahudi kwa kuwa alitenda maajabu
na ishara kwa jina la Yesu Kristo. Akiwa mbele ya baraza la Wayahudi anaendelea
kutoa hotuba inayoshuhudia ukweli wa Neno la Mungu (rej. Mdo. 6:1-7:1-60).
Stephano anaonyesha ujasiri wa hali ya juu kabisa. Anaonyesha imani yake kwa
Bwana wetu Yesu Kristo bila kuogopa macho ya watesi wake. Anazungumza ukweli
bila kuficha lolote. Mwishowe anauawa kwa sababu ya kusema ukweli uliowachoma
Wayahudi. Kuuawa kwake hakuzuii Neno la Mungu kuendelea kutangazwa. Neno la
Mungu halifungwi na minyororo ya mateso au kifo.
Mtume
Paulo naye anafungwa gerezani mara kadhaa kwa sababu ya Neno la Mungu.
Alipelekwa mbele ya baraza la Wayahudi na aliwaambia ukweli wa Neno la Mungu
wajumbe wa baraza lote la makuhani na Wayahudi (rej. Mdo. 22:30-23:1-11,
24:24-26:32). Neno ambalo Mtume Paulo analihubiri akiwa kifungoni linaonyesha
wazi kabisa kwamba Neno la Mungu halifungwi minyororo (rej. 2 Tim. 2:9). Fundisho
hili linajirudiarudia sana katika maandishi ya Mtume Paulo katika barua zake
(rej. Flm. 1:7-17, 9-13). Lakini zaidi katika Waraka wake kwa Wafilipi (rej.
Flp. 1:13-17) na katika waraka kwa Waefeso (rej. Efe. 3:1-13). Neno la Mungu
haliwezi kuzuiliwa na kitu chochote kuhubiriwa na kupenya katika mioyo ya watu.
Kwa
njia ya haya yote, tunajifunza ujumbe mahususi kwamba Neno la Mungu hupenya
sehemu yoyote. Mungu katika haya yote anatufunulia asili yake Mwenyewe kuwa ni
Roho halisi na ukamilifu wake hauna mipaka. Yeye ni wa mahali pote. Bwana wetu
Yesu Kristo anaushuhudia ukweli huu, “…watu hawa wakinyamaza, hata mawe
yatasifu” (rej. Lk. 19:40). Hivyo, watu wakizuiwa kutangaza Neno la Mungu hata
mawe yatalitangaza. Neno la Mungu halifungwi minyororo. Aidha mambo yote
yapita, Neno la Mungu halitapita kamwe (rej. Lk. 21:33). 2.2.7 Neno la Mungu
lina nguvu ya ajabu. Tunapaswa kulitafuta Neno la Mwenyezi Mungu siku zote na
mahali pote na kwa nguvu zetu zote.
Katika
kipindi hiki cha Kwaresima, tunaalikwa kutenga muda maalum wa kulisoma,
kulitafakari, na kulitangaza kwa watu wote kwa maneno, matendo yetu mema na ushuhuda wa maisha yetu. Jukumu hili litekelezwe na
mtu binafsi, familia, jumuiya, vyama vya kitume na Kanisa lote kwa ujumla (rej.
Mk. 16:15-16). Kama asemavyo Mtume Paulo, “Litangaze Neno, sisitiza, hakikisha,
onya, himiza kwa uvumilivu wote na elimu” (2Tim. 4:2); na Bwana wetu Yesu
Kristo hatatuacha (rej. Mt. 28:20). Matunda ya Neno la Mungu ni haki, amani na
furaha kwa mtu binafsi, familia, jumuiya, taifa na ulimwengu wote. Aidha wokovu
na uzima wa milele ni matunda ya Neno la Mungu (rej. Yn.14:6, Mt. 22:29,
Rum.1:16, Flp. 2:6-11). Neno la Mungu ni uhai wetu. “Mtu hataishi kwa mkate tu
ila kwa kila Neno litokalo katika kinywa cha Mungu” (Mt. 4:4). Tunapata uhai
katika mateso na vifungo vya kimwili kwa sababu tunajishibisha kwa Neno wake
Mungu, Yesu Kristo anayetufundisha na kutulisha. Neno la Mungu ni nuru yetu
(rej. Yn. 3:19-20). Tuwapokee wanaotutangazia Neno la Mungu na tulizingatie.
(rej. Mt. 10:40-42)
Neno
la Mungu linatupatia uthabiti na kutuimarisha katika ukweli kwamba kwa neema ya
Mungu, tunao uwezo wa kushinda dhambi na kuufanya Ufalme wa Mungu ufike. Neno
la Mungu linasema kuwa yeye alifanywa mdhambi kwa ajili yetu sisi, alichukua
dhambi zetu na adhabu katika mwili wake msalabani. Alifanywa kuwa laana kwa
ajili yetu, na kwa ajili ya wale wote wanaoweka tumaini lao katika yeye kwao
hao hakuna adhabu (rej. 1 Pet. 2: 21-24). Neno la Mungu linaleta matumaini
kwamba hitaji la wanadamu kuokolewa limetekelezwa na Mungu tayari. Neno hili
ndilo Habari Njema. Lakini Habari Njema hii inaleta pia wajibu kwa upande wa
pili, yaani, waamini tunapaswa kumgeukia na kumrudia Mungu, na hiyo ndiyo maana
ya kutubu na kuiamini Injili. Kwa namna hiyo Ufalme wa Mungu utakuwa unadhihirishwa
maishani mwetu.
Neno
la Mungu ni ukweli, na sifa moja ya ukweli ni kwamba hudumu daima bila
kubadilika. Kwa vile Neno lake lina pumzi ya
Roho wa Mungu, vile ambavyo Roho wa Mungu hafungwi, kadhalika na Neno la Mungu
halifungwi na pingu au vizuizi au vikwazo vinavyoweza kumfunga Roho, kama
ambavyo usivyoweza kufunga mnyororo upinde wa mvua. Neno lake li hai, tena
lenye nguvu (rej. Ebr. 4:12-13); lina nguvu zaidi kuliko kitu chochote hapa
duniani. Mambo yote mengine hayana uwezo wowote ukilinganisha na Neno la Mungu.
Ilikuwa kwa njia ya Neno la Mungu kwamba mbingu ziliumbwa. Mungu anapotamka
kinachotamkwa hufanyika na mambo yote hutii. Neno la Mungu haliwezi kufungwa
minyororo kwa sababu ni nguvu isiyoweza kuzuiwa; ni yenye uwezo wa kutaalamisha
na kuangaza na kuwafanya watu wengi bila idadi kwa pamoja wafanane zaidi na
Kristo. Yesu Kristo ni Neno aliyetwaa mwili, hekima aliyemwilishwa, ukweli
uliomwilishwa, na chimbuko lililomwilishwa la kila kitu. Kukosa ukweli, kukosa
uwazi na u-ndimi mbili ni kinyume cha uhalisia wa Mungu na Ufalme wa Mungu.
Popote ambapo mtu anamkana Kristo, atakuwa daima anaukataa ukweli.
Kupenda
lisilo kweli, kutokuwa na msimamo kuhusu ukweli, kuubinafsisha ukweli, kuuweka
ukweli na lisilo kweli katika ngazi moja, yote haya hupatikana katika kiini cha
dhambi ya Adam na Eva (rej. Mwa. 3:1-24). 2.2.10 Kristo alikuja ili kuubomoa
Ufalme wa uwongo na kuusimika Ufalme wake wa ukweli, kwa lengo la kumweka huru
binadamu dhidi ya giza la uwongo na udanganyifu: “Kwa sababu hii nalitokea
ulimwenguni, ili niushuhudie ukweli. Yeyote yule aliye wa ukweli huisikia sauti
yangu” (Yoh. 18: 37). Yesu ndiye ukweli na uzima aliyekuja kuwaweka watu huru
dhidi ya utumwa wa utawala wa shetani. Ukweli huu ni nafsi yake mwenyewe
anayetualika tumsikie ili tupate kuwa raia wa ufalme wake na ili tupate
hatimaye kufika kwa Baba. (rej. Yoh. 14: 6). Kumbe, Neno analotuambia Kristo ni
ukweli unaotuonyesha njia ya kufikia uzima wa milele.
HITIMISHO: Kwa kushika Neno lake, tunafanyika warithi wa uzima wa
milele na raia wa Ufalme wa Mbinguni. Katika kipindi hiki cha Kwaresima tunao
uchaguzi wa kufanya. Tunaalikwa kuliishi Neno la Mungu kwa maneno na matendo
yetu; na pia kulishuhudia kwa watu wengine ili ufalme wa Mungu uendelee
kujidhihirisha kwetu na watu wengine. Hii ndiyo njia pekee itakayoyafanya
maneno haya yatimie, “Ufalme wako Ufike”.
SURA
YA TATU UFALME WA MUNGU NA MAMLAKA YA WATU:
Katika Barua yake kwa Warumi, Mtume Paulo anachagua sura ya 13:1-7 kueleza
uhusiano uliopo kati ya mamlaka au tawala za watu na ufalme wa Mungu. Mtume
Paulo anatambua kuwa tawala zote za dunia zilizo halali zimewekwa na Mungu
mwenyewe aliyeumba ulimwengu kwa upendo wake mkubwa. Hivyo kila mtu inabidi
atii mamlaka hizo ili kuweza kuendana na mpango wa mwenyezi Mungu aliyeweka mamlaka
hizo. Mungu anaendelea kuvileta viumbe vyote pamoja ili vibaki katika mpango
wake wa uumbaji: kumjua, kumpenda, kumtumikia na hatimaye kuurithi uzima wa
milele. Katika sura hii tunawaalika kutafakari uhusiano uliopo kati ya ufalme
wa Mungu na mamlaka ya watu, tukiongozwa na Maandiko Matakatifu na Mafundisho
ya Kanisa Katoliki.
AGANO
LA KALE: Mwanzoni Taifa la Israeli lilikuwa
tofauti na mataifa mengine kwani hawakuwa na mfalme bali walitambua utawala wa
Yahweh pekee. Ni Mungu aliyeingilia kati kwa niaba ya Waisraeli kwa kupitia
watu wenye karama kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Waamuzi. Watu
wanamwendea aliyekuwa wa mwisho wa hao, Samweli, nabii na mwamuzi, wakimwomba
awateulie mfalme (rej.1Sam. 8:5; 10: 18-19). Samweli anawaonya Waisraeli
kuhusiana na athari za utawala dhalimu (rej.1Sam. 8:11-18). Hata hivyo, mamlaka
ya Mfalme yanaweza kuonekana kama zawadi ya Mungu anayekuja kuwasaidia watu
wake (rej. 1 Sam. 9:16). Mwishowe, Sauli anapakwa mafuta na kuwa mfalme (rej. 1
Sam. 10: 1-2). Matukio haya yanadhihirisha fadhaa iliyowafanya Waisraeli
kuelewa ufalme kwa namna tofauti na vile ulivyokuwa ukieleweka kwa jirani zao.
Mfalme, aliyeteuliwa na Mungu (rej. Kum. 17: 15; 1 Sam. 9:16) na aliyewekwa
wakfu naye (rej.1 Sam. 16:12-14), anaonekana kama mtoto wa Mungu (rej. Zab.
72).
Mfalme,
kwa hivyo, anakuwa mlinzi wa walio dhaifu na mdhamini wa haki kwa watu wake.
Shutuma za manabii zinalenga haswa katika wafalme kushindwa kutekeleza wajibu
hizo (rej. 1 Fal. 21; Isa 10:14; Amo. 2:6 – 8:48, Mik. 3:1-4). 3.1.2 Katika
Agano la kale, kwa nyakati tofauti, Mungu anajionyesha kuwa ndiye anayewaongoza
watu wake kwa mkono wa wale aliowachagua yeye mwenyewe kutenda kwa niaba yake.
Anaeleza wazi kuwa, katika yeye, watawala na mamlaka yao hutekeleza kile
kilicho ndani ya mpango wake mwenyewe (rej. Mith. 8:15). Mungu aliye mtawala
pekee katika wateule wake, anazidi sana kuwajalia hekima na busara ya kutenda
kwa niaba yake (rej. 1Fal. 3:4-15). Watawala wanakuwa vyombo anavyotumia Mungu
kutekeleza kazi alizokusudia yeye mwenyewe kwa watu wake (rej. Isa. 11:2-5;
Yer. 23:5; Sir. 10:4). Watawala nao kwa upande wao walijifungamanisha na upendo
wa Mungu ili kuimarisha uhusiano mwema na Mungu wao. Aidha watawala wa Agano la
Kale walitekeleza majukumu yao kadiri ya mapenzi ya Mungu. Hivyo waliheshimiwa
kwa kazi zao hizo zilizowastahilisha wao wokovu na wale waliowaongoza (rej.
Hek. 6:12, YbS.1:16). 3.1.3 Mungu mwenyewe aliwaweka watawala, akiwatarajia
kuwaongoza watu na kuyafanya mawazo na matendo yao kuwa ya hekima, kwani Mungu
alikusudia kutengeneza Taifa lenye heshima na mwenendo mwema (rej. Hek. 6:3;
Zab. 2:10; Mith. 8: 15-16).
Watawala
hao wa Agano la Kale pia walipaswa kuwa waamuzi kati ya watu. Kwa hiyo,
iliwabidi kujaa hekima itokayo kwa Mungu ili wahukumu kwa upendo na haki maana
walitenda mahala pa Mungu mwenyewe mwenye upendo na haki (rej. Hek. 6:4-7; Ayu.
34:17-19; YbS. 35:12). Mungu aliyekusudia hayo yote yafanyike, pia aliwasaidia
watu kutii kanuni, taratibu, na sheria za mamlaka halali za watu. Sio tu
wanadamu peke yao walipaswa kutii mamlaka hiyo bali kila kitu kilichoumbwa na
Mungu (rej. Yer. 27:7-10; Jdt11:7). Kwa jinsi hiyo, watu walimtii Mungu na
Watawala pia (rej. Yer. 27:5-7), ambao wanamwakilisha Mungu aliye chanzo cha
mamlaka zote duniani.
AGANO
JIPYA: Mtume Paulo katika waraka wake kwa
Warumi anaongea juu ya kuheshimu serikali, yaani “kujisalimisha” kwa serikali,
“kuwa chini” ya serikali au “kutii” serikali; kwani mamlaka zilizopo duniani
zimetoka kwa Mungu (rej. Rum. 13:1). Mungu kwa huruma na upendo wake anawashirikisha
baadhi ya wanadamu zawadi ya kuwa na mamlaka juu ya wanadamu wenzao. Ingawa
Mungu ameamua kuwashirikisha baadhi ya wanadamu zawadi ya kuwa na mamlaka juu
ya wanadamu wenzao, lakini namna ya kuchagua viongozi hao na jinsi
wanavyoongoza ni jukumu la kibinadamu. Hii inafanya suala la kuongoza kuwa
taasisi ya kibinadamu iliyowekwa na Mungu mwenyewe, hivyo watu wanahimizwa
kuzitii mamlaka hizo (rej. Rum. 13:1-7).
Kwa
kusema: “Hakuna mamlaka yasiyotoka kwa Mungu, na kila yaliyoko yamewekwa na
Mungu” (Rum. 13:1), Mtume Paulo analinganisha utii kwa serikali na utii kwa
Mungu. Utii huu wote ni wa lazima. Wakristo ambao hawatii kanuni, taratibu na
sheria halali za serikali hawamtii Mungu. Hata Bwana wetu Yesu Kristo akiwa
hapa duniani alitii mamlaka za kibinadamu zilizokuwa zikiongoza Taifa lake la
Israeli wakati wake (rej. Lk. 2:51-52, Mt. 17:24-17). Hata hivyo, ni vema
ijulikane wazi kuwa hatutakiwi kutii tu mamlaka halali zilizowekwa na Mungu
bila kuzingatia dhamiri yetu njema (rej. Rum. 13:5) yenye kutambua wajibu na
nafasi yetu katika jamii.
Tena
tutii tukijua kuwa yatupasa kuzitii mamlaka zilizo halali ili tuweze kuuona
ufalme wa Mungu. Tunahimizwa kutimiza wajibu wetu kwa Mungu, kwa mamlaka za
kidunia na kwa jamii (rej. Mt. 22:21) ili kuwepo haki, amani, furaha,
maelewano, na kuchangia maendeleo ya jamii zetu; kwa mfano, kwa kulipa kodi
(rej. Rum. 13:7, Mt. 22:21). Mtume Paulo aliamini kuwa Wakristo na raia wote
kwa ujumla lazima walipe kodi kwa serikali, ili Serikali nayo kwa upande wake,
itoe huduma nzuri za kijamii ikitumia mali ya raia wake kwa ukweli na uaminifu.
Raia kwa upande mmoja, na serikali kwa upande mwingine, tunapaswa kufanya vivyo
hivyo, tukizingatia kanuni, taratibu na sheria zetu.
Watawala
kwa upande wao, wanaowaongoza watu, wanatakiwa wawaelekeze namna ya kuenenda
kadiri ya mpango wa Mungu, wakiwakumbusha
kanuni, taratibu, na sheria za msingi za kufuata. Iwapo raia watakosea, basi
namna inayofaa kadiri ya mpango wa Mungu, itumike kuwakosoa. Kumbe, watawala
wameshirikishwa hadhi ya Baba mwenye upendo na huruma ambaye anahukumu kwa haki
na ambaye anakemea na kukaripia ikiwa ni kwa uvumilivu na mafundisho (rej.
2Tim. 4:2). 3.2.4 Hata hivyo, Watawala wanalo jukumu la kuwaadhibu watu waovu
kwa mujibu wa sheria halali za nchi. Raia wema hawana sababu ya kuwaogopa
watawala. Watu ambao hufanya vitendo vibaya lazima watarajie kuadhibiwa na
watawala wao. Kwa hiyo, watu waovu wana sababu ya kuogopa watawala wao (rej.
Rum. 13:3-4). Kile kinachoweza kuonekana kuwa ni uasi wa raia, kinaweza
kuhesabiwa haki ikiwa tu sheria ya serikali inapingana waziwazi na sheria ya
Mungu.
Mtakatifu
Petro anawasihi Wakristo asemapo, “Tiini kila kiamriwacho na watu kwa ajili ya
Bwana” (1 Pet. 2:13). Mfalme na watawala wake wana wajibu “wa kuwaadhibu
watenda mabaya na kuwasifu watenda mema” (1 Pet. 2:14). Mamlaka yao hayo sharti
“yaheshimiwe”, yaani, yatambuliwe kwa sababu Mungu anadai mwenendo sahihi” (1
Pet. 2:17). Uhuru usitumike kwa kusisitiza ubaya, bali kumtumikia Mungu (rej. 1
Pet. 2:16). Msisitizo ni juu ya utii ulio huru wa kuwajibika kwa mamlaka
iwezeshayo haki kuheshimika, ikihakikisha manufaa kwa wote.
Kwa
upande mwingine, Kanisa linatufundisha kwamba hatuna ruhusa ya kuwatii viongozi
wetu pale wanapotuamuru kutenda kinyume na Amri za Mungu. Ni muhimu kuzingatia
kuwa kujiweka chini ya mamlaka haya hakumaanishi kwamba ni lazima tutii kama
vipofu amri inayotolewa na dola ambayo ni mbaya au inakwenda kinyume na Amri ya
Kristo ya kuwapenda jirani zetu. Hoja ni kwamba raia wanapotii mamlaka iliyoko,
mamlaka hiyo nayo lazima imtii Mungu. Hivyo, mamlaka inapoacha kutunuku matendo
mema au tabia njema, au inapoacha kuadhibu maovu, na badala yake ikaamrisha
mambo yaliyo kinyume; mamlaka hiyo inapoteza nguvu au uwezo wake wa kimaadili
wa kuongoza watu. Mamlaka ya kiraia yamewekwa ili kudumisha utulivu katika
jamii. Hivyo basi, raia ni lazima wafanye kile ambacho ni sahihi ikiwa wanataka
kuepukana na hukumu au adhabu. Tuitii mamlaka kwa sababu ya dhamiri zetu
sahihi. Kwa maneno mengine, dhamiri zetu zituelekeze kwamba Mungu, ambaye ndiye
mwenye mamlaka kuu kupita zote, ameweka ngazi mbalimbali na kuweka sheria ili
kuhakikisha kuwa kuna utulivu na utaratibu. Aidha, kupingana na ngazi hizo ni
kupingana na mpango wa Mungu wenye lengo la kuwa na jamii yenye utulivu. (rej.
Mdo. 4:18-20).
Kwa
kuwa Mungu ametuumba ili tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho tufike kwake
mbinguni, ni wajibu wa kila mmoja wetu kwa nafasi yake, awe mtawala au
mtawaliwa, kuutafuta kwanza ufalme wa Mungu (rej. Lk 12:31). Ufalme wa Mungu
tutaupata kwa kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu na kutimiza wajibu wetu
itupasavyo katika nafasi zetu. Kila mmoja wetu ni kiongozi wa nafsi yake
mwenyewe, hivyo tujifunze kuzitii dhamiri zetu njema zinazotuongoza kutenda
mema na kutuzuia kutenda mabaya. Kwa kufanya hivyo tutaweza kueneza utawala wa
Mungu maishani mwetu, utawala wa haki, amani na furaha. Basi, utawala wa watu
au mamlaka ya watu iwe na lengo la kuuleta ufalme wa Mungu karibu zaidi katika
maisha ya kila siku ya watu.
MAFUNDISHO
YA MTAGUSO MKUU WA PILI WA VATICAN.
Kadiri ya mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican moja kati ya maeneo
yaliyotiliwa mkazo ni uhusiano kati ya Ufalme wa Mungu na utawala wa watu,
hususani katika Hati ya Kichungaji juu ya Kanisa na Ulimwengu (Gaudium et
Spes-GS). Utambuzi hai wa hadhi ya binadamu katika mahali pengi duniani,
unaamsha juhudi ya kuunda utaratibu wa kisiasa na kisheria ambapo haki za
binadamu katika maisha ya hadhara zinalindwa vema zaidi. Nazo ndizo haki za
kujumuika na kuunda umoja kwa uhuru, haki ya kila mmoja kutoa maoni yake na
kukiri imani yake akiwa peke yake au hadharani.
Maana,
ulinzi wa haki za binadamu ni sharti la lazima ili raia, kila mmoja peke yake
au kama wanachama, waweze kushiriki kimatendo maisha ya umma na uongozi wa
mambo yanayowahusu. (rej. GS. 73). Pamoja na maendeleo ya kiutamaduni, kiuchumi
na kijamii, hamu ya walio wengi ya kuchukua wajibu mkubwa zaidi katika kuratibu
maisha ya jumuiya ya kisiasa inazidi kupata nguvu. Katika dhamiri ya watu wengi
bidii ya kuhifadhi haki za makundi ya wachache katika nchi zao inastawi, lakini
bila ya makundi hayo ya wachache kusahau wajibu zao mbele ya jumuiya ya
kisiasa. Aidha, inazidi kukua heshima mbele ya watu wenye maoni au dini
tofauti. Na wakati huohuo ushirikiano mpana zaidi unaundwa; nao unalenga kwa
raia wote (rej. GS. 73). Ili kuunda maisha ya kisiasa yaliyo kweli ya
kibinadamu, hakuna lililo bora zaidi kuliko kustawisha ndani ya watu hisia za
haki, upendo na huduma kwa manufaa ya wote. Pia ni kuuimarisha msimamo wa
msingi mintarafu maumbile halisi ya jumuiya ya kisiasa; tena kuhusu lengo,
matumizi halali na mipaka ya wajibu wa serikali (rej. GS. 73).
Utawala
wa kisiasa, uwe unatekelezwa na jumuiya yenyewe au na vyombo vinavyowakilisha
dola, ni lazima daima ufanyike ndani ya mipaka ya sheria ya kimaadili. Lengo lake ni kuyafikia manufaa ya wote, tena manufaa
yenye maendeleo yake, kadiri ya kanuni za utaratibu wa kisheria uliokwisha
kuwekwa, au wa kuwekwa. Na hapo ndipo raia wanapolazimishwa kutii kwa sababu ya
dhamiri zao (rej. GS. 74). Aidha katika Hati ya Kanisa katika Ulimwengu
mamboleo (GS), Mtaguso unasisitiza kuwa utekelezaji wa madaraka ya kisiasa
daima ukusudie katika kumuunda mtu mwadilifu, mtulivu, na mkarimu kwa wote, kwa
manufaa ya familia nzima ya wanadamu.
Ili
kukuza maisha ya hadhara ya kisiasa, sharti ipatikane miundo ya kisiasa na
kisheria inayowawezesha zaidi na zaidi raia wote – bila ubaguzi wowote –
kushiriki kwa uhuru na kwa matendo katika kutengeneza misingi ya kisheria ya
jumuiya ya kisiasa. Lengo lake ni kuongoza mambo ya dola, katika kuainisha
uwanja wa kazi na mipaka yake kwa taasisi mbalimbali, na hatimaye katika
kuwachagua viongozi. Kwa sababu hiyo, raia wote wakumbuke haki yao, ambayo pia
ni wajibu, ya kutumia kura yao huru kwa minajili ya kuhamasisha manufaa ya
wote. Kanisa linasifu na kuthamini wale ambao, kwa ajili ya kuwatumikia
wanadamu, wanajitoa kwa manufaa ya dola na kubeba uzito wa wajibu husika (rej.
GS. 75).
Katika
nyakati zetu hizi, ugumu wa masuala yanayojitokeza unazilazimisha serikali
kujihusisha zaidi katika fani za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni ili kuleta
mazingira yanayofaa zaidi, kusudi raia na makundi waweze kuyafuatilia kwa bidii
na kwa uhuru manufaa kamili ya binadamu. Uhusiano mzuri miongoni mwa watu na
uwezo wa kujiratibisha na kujiendeleza kwa mtu binafsi, unaweza kufikiriwa kwa
namna tofauti katika nchi mbalimbali za ulimwengu na kwa mujibu wa maendeleo ya
mataifa. Raia hawana budi kustawisha upendo kwa taifa lao kwa ari na unyofu,
lakini si kwa mtazamo finyu, yaani hivi kwamba wayazingatie daima mema ya
familia nzima ya wanadamu inayounganika kwa vifungo mbalimbali kati ya
makabila, mataifa na nchi (rej. GS. 75).
UJUMBE
WA PAPA FRANCISKO (01.01.2019)
Baba Mtakatifu Francisko, katika Ujumbe wa Siku ya Kuombea Amani Duniani mwaka
2019, wenye kauli mbiu ya “Siasa safi ni huduma ya amani”, aliangalia mambo
kadhaa, kwa kuzingatia kuwa Injili ya amani ni sehemu ya utume wa Kanisa. Mambo
hayo ni a) Changamoto za siasa safi; b) Upendo na fadhila za kiutu kwa ajili ya
siasa inayohudumia haki msingi na amani; c) umuhimu wa siasa safi
inayowashirikisha vijana na kujengeana imani; na d) kukataa kishawishi cha vita
na mbinu mkakati wa vitisho, kwa kuwekeza katika mradi mkubwa wa amani.
Changamoto
za siasa safi: Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema, amani ni sawa na matumaini
yanayosongwa na changamoto pamoja na magumu yanayowaandama walimwengu, hasa
kutokana na uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka, na matokeo yake
ni matumizi mabaya ya madaraka na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Siasa
safi ni nyenzo inayosaidia ujenzi wa huduma kwa binadamu, lakini siasa
ikitumiwa vibaya inaweza kuwa chombo cha dhuluma, mipasuko na hatimaye
kusababisha madhara makubwa kwa jamii. Kuhusiana na hilo naye Papa Paulo VI
alikuwa na haya, “Siasa ikichukuliwa katika umuhimu wake kuanzia ngazi ya
kijiji, kimkoa, kitaifa na kidunia- ni kukubali wajibu wa kila mtu kukiri
ukweli na thamani ya uhuru ambao unatolewa kwake na jamii kuufanyia kazi kwa
manufaa mazuri ya mji, taifa na binadamu wote,” (rej. Octogesima Adveniens, 14
Mei 1971, 46).
Upendo
na fadhila za kiutu ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na
amani: Baba Mtakatifu Fransisko akimnukuu
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema, “Kila mtu ajitahidi kujikita
katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili
kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu” (rej. Benedict XVI,
Caritas in Veritate 29 June 2009). Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na
kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi
zinazoboresha siasa safi. Mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu
wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi
anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tena,
anapaswa kuwa mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima
akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, awe tayari kuchochea
mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri.
Siasa
safi inajengeka katika unyenyekevu, kielelezo
makini cha huduma katika ngazi mbali mbali za maisha ya binadamu: Lengo ni
kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha
zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa
siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza,
kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha
maisha ya wananchi wao katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya
binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa chombo cha upendo. Umuhimu wa
siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani: Baba Mtakatifu
anaendelea kuhimiza umuhimu wa kudumisha siasa safi inayowashirikisha vijana na
kujengeana imani, kiasi kwamba, hata vijana wa kizazi kipya wanajisikia kuwa ni
sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii yao na kwamba, wanaweza kushirikisha
karama na mapaji waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao ya wengi.
Hawa ni vijana ambao dhamana ya amani inapenyeza katika akili na nyoyo zao,
tayari kujitosa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Siasa
safi inayojikita katika ujenzi wa Amani: Siasa
ya namna hii inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano, watu
kuaminiana, kuthaminiana na kujenga upendo. Haya yatafuta dalili za ubinafsi unaofumbatwa
katika dhana ya utaifa usiokuwa na tija. Jamii inawahitaji wanasiasa ambao
watakuwa wajenzi wa amani, watakaokuwa watangazaji, mashuhuda na vyombo vya
wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake ambaye anawatakia watoto wake
furaha.
HITIMISHO Hivyo, basi tunaalikwa tuwaombee viongozi wetu waweze
kutawala kadiri ya mapenzi ya Mungu (rej. Dn. 4:17). Daima watawala watambue
kuwa uongozi ni utumishi, dhamana, uwakili, na kuwa watatakiwa kutoa hesabu ya
utumishi wao kwa Mungu na kwa jamii. Hata hivyo, tunaamini kuwa watawala ni
wajumbe wa Mungu ambao licha ya ubinadamu wao, neema ya Mungu huwasaidia katika
kutimiza majukumu yao (rej. Mith. 8:15-16). Ndiyo maana ni muhimu kuwaombea
watawala. Mtakatifu Paulo alipendekeza hata alipokuwa akiteswa, kuwa “sharti
pawepo dua, sala, maombi na sala za shukrani kwa Mungu kwa ajili ya watu wote,
kwa ajili ya wafalme na watu wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya
utulivu na amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema” (1Tim 2:1 – 2).
SURA
YA NNE MAZOEZI YA KIROHO NA UFALME WA MBINGUNI. Ni ukweli usiopingika kwamba mazoezi ya kimwili yana faida
nyingi, ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa mwili na akili, kujenga mahusiano
mema baina ya watu katika jamii, na faida nyingine nyingi. Lakini, mazoezi ya
kiroho yana faida zaidi, faida za kila namna na pekee. Kwani humuandaa
mwanadamu kwanza kuwa na mahusiano mema na wenzake katika jamii, na zaidi
humuandaa kwa maisha ya umilele mbinguni; “Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za
mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani unayo ahadi ya
uzima wa sasa, na ya ule utakaaokuwapo baadaye” (rej. 1Tim. 4: 8).
KWA
NINI MAZOEZI YA KIROHO? Mazoezi
ya kiroho ni matendo yanayofanywa mara kwa mara ili kuiweka roho katika hali ya
uhusiano mzuri na Mungu kwa njia ya muunganiko wa ndani na Bwana wetu Yesu
Kristo (rej. Yn. 15: 1-17). Matendo hayo ni sala, kufunga lakini pia kutenda
matendo mema kwa wote. Utii kwa mapenzi ya Mungu, unyenyekevu, kushiriki
maadhimisho ya mafumbo matakatifu kwa ibada na uchaji mkubwa, kupokea
Sakramenti, kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, kusoma na kutafakari maisha
ya Watakatifu, kusoma vitabu mbalimbali vya maisha ya kiroho, n. k. Mazoezi ya
kiroho yanahitaji zaidi msukumo wa ndani wa mtu binafsi ili kuweza kuleta mafaa
katika maisha yake ya kiroho (rej. Yoe. 2:17). Mazoezi haya yanahitaji sana
msaada wa neema ya Mungu ili mtu aweze kuuvua utu wa kale, avae utu mpya na
kujibidisha katika kuufanya upya utu wa ndani unaodhihirishwa na matendo mema
ya nje.
Kwaresima
ni kipindi cha “Mazoezi zaidi ya Kiroho”. Mama Kanisa anatualika katika kipindi
hiki cha Kwaresima kwamba tufanye mazoezi ya kiroho, yaani kujiandaa katika
kuvishwa taji ya Utukufu mbinguni: taji isiyoharibika. Hiki ni kipindi maalum
kwa ajili ya waamini kujitafiti katika maisha ya kiroho, ili pale walipokosea
basi waombe toba na kuanza maisha mapya. Ni mwaliko wa kujitafakari kwa kina,
na kwa ndani kabisa; kuutafakari uhusiano wetu na Mungu, na kuyaacha yote yale
yanayotufanya tuwe mbali na Mungu. Ni kipindi cha kujifunza kutenda mema, kama
tunavyoalikwa na Nabii Isaya anaposema:” Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu
na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane”
(rej. Isa. 1:17).
Mazoezi
ya Kiroho huimarisha uhusiano wetu na Mungu. Kwa asili mwanadamu si mkamilifu
kama Mungu alivyo; mara kwa mara huanguka katika dhambi. Kwa sababu hiyo Kanisa
limeweka utaratibu wa mazoezi ya kuendelea kuutafuta ushirika na Mungu
tunaoupoteza kwa sababu ya dhambi. Ni mwaliko wa pekee kutaka na kutamani sana
kuuchuchumilia Utakatifu ambao ndio wito wa kila mbatizwa. 4.1.4 Kwaresima ni
kipindi kizuri cha kufanya tafakari, kusali, kufunga, na kufanya matendo ya
huruma kwa mwili na kwa roho bila ya kujali cheo, umri au jinsia. Mama Kanisa
anamwalika kila mkristo mkatoliki kujifunza unyenyekevu, huruma kwa maskini,
utu wema, mapendo kwa Mungu na kwa jirani. Hiki ni kipindi cha kutafuta
ushirika na Mungu na Kanisa kwa njia ya toba na maungamo, ili kuyaondoa
majeraha yaliyomo ndani yetu.
AINA
YA MAZOEZI YA KIROHO Biblia inaonyesha aina mbalimbali
za mazoezi ya kiroho, mfano: 4.2.1 Kufunga na kusali (rej. Mt. 6:6): Sala ni
kuinua akili na mioyo yetu kwa Mungu, na kuongea naye. Hili ni zoezi la kwanza
kabisa la kiroho ambapo mwanadamu anakutana na Mungu, muumba wake na kuongea
naye (rej. Zab. 4:4) ili kujua mapenzi yake (ufalme wake) na kuyatimiza,
akimwomba msamaha wa dhambi zake (rej. 1Yn. 1:9), akipumzika kwake (rej. Mt.
11:28 – 30) pamoja na kuisikiliza sauti ya Mungu wake (rej. Lk.10:39). Katika
Agano la Kale pia, tunamwona nabii Danieli akifunga na kuwaombea watu wake ili
Mungu awasamehe maovu yao (rej. Dn. 9:3 – 6). Aidha, katika Agano Jipya, Bwana
wetu Yesu Kristo anatuonyesha mfano bora wa kusali na kufunga (rej. Mt. 4:2,
10:1 – 4, Mk. 3:13 –19, Lk. 6:12 – 16). 4.2.2 Matendo mema yafaa Zaidi:
Kutokula kwafaa sana lakini kutoa ambacho sitakula kwa wahitaji kwafaa zaidi.
Kusaidia
wahitaji kwafaa sana lakini kusaidia bila ya kujionyesha
mbele ya watu kwafaa Zaidi (rej. Mt. 6:16-18); “maana imeandikwa, unapotoa
sadaka hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume.” (Mt.
6:3). Kuwasaidia wahitaji wakati wa sikukuu kwafaa sana lakini kuwasaidia kila
mara unapojaliwa chochote kwafaa zaidi. Hivyo, matendo yetu ya nje yafaa kuwa
ya unyenyekevu ili yazifaidie roho zetu, tusiwe sawa na wanafiki ambao hufanya
mambo yao kwa matangazo makubwa na kupenda kujulikana na kila mtu kwamba wao
ndio waliotenda jambo hili ama lile (rej. Mt. 6:1). Kusoma kiaminifu Neno la
Mungu na kulitafakari: Kama tulivyodokeza hapo juu, na hili ni mojawapo ya
mazoezi muhimu sana ya Kiroho. Ili kuwa imara kiroho yatupasa kulisoma na
kulitafakari Neno la Mungu mara kwa mara na kulielewa. Kwa kulisoma Neno la
Mungu, kulitafakari na kulielewa tunapata ulinzi wa Mungu (rej. Isa. 30:12),
tunapewa hekima ya kimungu (rej. Yak.1:5), tunapata faraja (rej. Zab 23:4), na
mwangaza wa kiroho (rej. Zab119:18).
Kutoa
sadaka na dhabihu: Tunapaswa siku zote kutoa sadaka
iliyo ya kweli na dhabihu safi kwa Mungu ili kuweza kutakatifuzwa katika maisha
yetu na kupata mafaa yetu sisi na Kanisa zima. Katika kitabu cha Mwanzo,
tunaambiwa Abeli alitoa sadaka yake kwa Mungu pasipo kuwa na choyo na hivyo
kubarikiwa na Mungu, lakini Kaini alitoa kwa choyo na kwa sababu hiyo
alilaaniwa (rej. Mwa. 4:3 – 15).
Kufanya
toba: Zoezi hili la kiroho linahitaji
zaidi msukumo wa ndani wa mtu wa kuwa tayari kukiri na kutubu uasi wake kwa
mapenzi ya Mungu, yaani kuwa tayari kukiri na kutubu uasi ili kupokea huruma na
msamaha wa Mungu ambao siku zote unasubiri utayari wetu wa kurudi na kusema
Baba tumekosa. Katika Agano la Kale, nabii Yona alikuwa tayari kufanya zoezi la
kiroho la kutubu hata akasamehewa dhambi zake (rej. Yon. 2:2-9). Kitabu cha
Esta pia kinabeba fundisho la zoezi hili la kiroho la kufanya toba (rej. Esta
4:17). Aidha Mwana mpotevu alikuwa tayari kurudi kwa baba yake na kukiri kwamba
amekosa na hivyo kufanya zoezi la kiroho kwa kutubu na kuomba msamaha (rej. Lk.
15:11 – 32). Lakini pia yule mwizi aliyetubu pale msalabani, anatupa fundisho
la kufanya toba hata kama ni dakika zetu za mwisho hapa duniani ili tuweze
kuurithi uzima wa milele. (rej. Lk. 23:40 – 43).
FAIDA
ZA MAZOEZI YA KIROHO KATIKA KUUTAFUTA UFALME WA MBINGUNI: Mtume Paulo katika barua yake ya kwanza kwa Wakorintho
(9:24-27), anaongelea faida ya mazoezi ya kiroho kuwa ni: Uzima wa milele:
Anayetoa tuzo hiyo ni Mungu aliye hai na wa milele. Hivyo mtu anayefanya
mazoezi ya kiroho vizuri na kwa ufanisi mwisho atapata tuzo hiyo, uzima wa
milele ambao pia ni ufalme wa mbinguni. Mtakatifu Paulo anasisitiza hili
akifuata maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye daima aliwaasa Mitume wake
waishi kwa namna ambayo watatoa kipaumbele kwa maisha yajayo, yaani ya umilele
(rej. Mt. 6:19-21). Mazoezi ya kiroho pia husaidia kuvumilia mateso na kushinda
majaribu mbalimbali ya shetani (Ayu.1:21- 2:10b): mazoezi ya kiroho ya Ayubu
yalimsaidia kukabiliana na majaribu yaliyompata, na kwa njia hiyo alizidi
kuimarika hata katika matatizo.
Hivyo
basi, akaweza kuvumilia na kumshinda shetani, akiyazingatia daima mapenzi ya
Mungu. 4.3.3 Mazoezi ya kiroho hutusaidia kuwa raia wema na wana wa Mungu na
hivyo twaweza kuurithi ufalme wa Mungu. Mtume Petro anawaambia waamini
waliokuwa wamekusanyika katika nyumba ya Korneli, kuwa yeyote anayeshiriki
mambo ya Kimungu ataurithi ufalme wa Mungu bila kujali ukoo au mahali
alipozaliwa mtu huyo (rej. Mdo.10:34-35). 4.3.4 Mazoezi ya kiroho pia humsaidia
Mkristo kuujua ufalme wa Mungu: Mazoezi mbalimbali ya kiroho kama vile semina
za maisha ya kiroho husaidia watu kupata elimu juu ya ufalme wa Mungu, kama anavyofundisha
Nabii Isaya “…. Mimi ni BWANA, Mungu wako nikufundishaye ili upate faida,
nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata. Laiti ungalisikiliza amri zangu!
Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya
bahari” (48:17-18).
Mazoezi
ya kiroho hutusaidia kuishi imani yetu kwa matendo: Kama Mtume Yakobo
anavyotuambia katika barua yake kwa watu wote (rej. Yak. 2:14-26), imani yetu
inapoonekana katika matendo yetu hapo ndipo kweli twaweza kusema tu watu wa
imani, yaani wana wa Mungu tunaosubiri kwa matumaini kuurithi uzima wa milele,
na imani yetu inakuwa ya kweli. Mazoezi ya kiroho hali kadhalika hutusaidia
kuwa makini katika mambo ya kiroho zaidi kuliko mambo ya kimwili: Wanaotafuta
kwa nguvu kubwa mambo ya kimwili waweza kupuuzia yale yote yanayohusu ufalme wa
Mungu, lakini wanaotafuta ya kiroho kwanza basi watakuwa katika njia nzuri ya
kuurithi ufalme wa Mungu (rej. Ebr. 13:5-19, 1Yn. 2:15-17, Mwa. 3:6, Mith.
27:20, Yer. 45:1-5). Katika Injili ya Mathayo (6:25-33), Bwana wetuYesu Kristo
anatusihi kuhangaikia zaidi kuurithi uzima wa Kimungu hasa kwa njia ya mazoezi
ya kiroho. 4.3.7 Mazoezi ya kiroho hutusaidia pia kuishi maisha ya upendo,
haki, amani na furaha katika jamii yetu, nchi yetu, taifa letu na ulimwengu
wote kwa ujumla. Matunda ya mazoezi ya kiroho hujidhihirisha kati yetu tangu
ulimwengu huu mpaka ulimwengu ujao. Tujibidishe zaidi kufanya mazoezi ya
kiroho.
Mazoezi
ya Kiroho Hujenga Mazoea Katika kipindi hiki cha Kwaresima, kufunga, kusali na
kujitoa kwa wahitaji hakuna maana kwamba tunamhonga Mungu
ili atusamehe au atupokee kwake mbinguni. La hasha! Pia haina maana kwamba
vipindi vingine vyote hatupaswi kufanya matendo hayo. La hasha! Maana yake ni
kufanya mazoezi ili iwe ni mazoea katika maisha yetu ya kila siku kama wakristo;
kama vile mwalimu amwandaavyo mwanafunzi wake aweze kufanya vyema au kocha
aandaavyo wachezaji wake, vivyo hivyo Kanisa huwaandaa waamini katika kufanya
yale yampendezayo Mungu na kuendelea kuwahimiza mazoezi hayo yawe sehemu ya
maisha yao.
HITIMISHO Wapendwa Taifa la Mungu, sisi Maaskofu wenu tunawatakieni
kila baraka katika safari hii ya kukua na kukomaa kiroho. Tumwombe Mungu
athibitishe imani yetu iweze kujidhihirisha katika maisha na matendo yetu ya
kila siku katika kuzingatia haki na kutenda mema. Katika kipindi hiki tunapenda
tuchukue maneno ya Yesu mwenyewe yawe dira yetu: “Ufalme wangu sio wa ulimwengu
huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu
wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio
wa hapa” (Yoh. 18:36). Hivi sisi pia ufalme wetu sio wa dunia hii kwani
tunashirikishwa ufalme wa Yesu kwa sakramenti mbalimbali na kwa njia ya mateso
katika Kanisa.
Yesu
Mwenyewe alisema anaenda kutuandalia makao ili alipo nasi tuwepo. Hivyo kama
vile Yesu asivyo wa ulimwengu huu hali kadhalika sisi nasi ufalme wetu sio wa
dunia hii. Daima tunawakumbusha kuwa; maisha yetu si ya kudumu. Hivyo yatupasa
kumtanguliza Mungu daima. Ikiwa sisi sio wa dunia hii tunapaswa kutafuta yaliyo
juu Kristo aliko “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo
juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu” (Kol. 3:1). Hata hivyo
hatuwezi kuyapata haya bila ya kufanya mazoezi ya kiroho. Mazoezi ya kiroho
tunayoalikwa tuyafanye yatusaidie: Kukua kiimani katika kumwelekea Mungu yaani
kuufikia Utakatifu. Kuwa karibu zaidi na Mungu. Kufika mbinguni baada ya
maisha ya hapa duniani. Kuelewa kuwa matendo ya huruma na huduma ni sehemu ya
maisha yetu ya kila siku. Tuendelee kuziombea falme zote za dunia zipate kujua
kuwa Mungu ndiye Bwana peke yake (rej. Isa. 37:20, Yoe. 3:17) na zitimize
mapenzi yake. Mungu aweze kuwa pamoja na falme hizo na watu wote kwa ujumla
(rej. Isa. 7:14, 8:8, 10, Zab. 46:8, 12). Hali za falme hizo na watu wote kwa
ujumla ziboreshwe: laana ziondolewe, magonjwa yaponywe, Mungu aendelee kufanya
maajabu makuu zaidi, ambapo haki, amani na furaha vitawale milele yote (rej.
Joe. 4:1-21). Hatimaye tunawatakieni matunda tele ya kipindi hiki cha Kwaresima
na mwishowe furaha za Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Ni
sisi Maaskofu wenu, 1. Mhashamu Askofu Mkuu Gervas
Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Mkuu, Mbeya 2.
Mhashamu Askofu Flavian Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania, Geita 3. Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ruzoka, Tabora 4. Mhashamu Askofu
Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi, Ofm Cap, Dar es Salaam 5. Mhashamu Askofu Mkuu
Beatus Kinyaiya, Ofm Cap, Dodoma 6. Mhashamu Askofu Mkuu Damian Dallu, Songea
7. Mhashamu Askofu Mkuu Isaac Amani, Arusha 8. Mhashamu Askofu Mkuu Renatus
Nkwande, Mwanza 9. Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Iringa 10. Mhashamu
Askofu Bruno Ngonyani, Lindi 11. Mhashamu Askofu Anthony Banzi, Tanga Ujumbe wa
Kwaresima - 2020 40 12. Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Mahenge 13. Mhashamu
Askofu Augustino Shao, CSSp, Zanzibar 14. Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi,
Rulenge-Ngara 15. Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma, Bukoba
16.
Mhashamu Askofu Method Kilaini, Bukoba (Askofu Msaidizi) 17. Mhashamu Askofu
Ludovick Minde, ALCP/OSS, Askofu, Moshi 18. Mhashamu Askofu Alfred Leonard
Maluma, Njombe 19. Mhashamu Askofu Michael Msonganzila, Musoma 20. Mhashamu
Askofu Almachius Rweyongeza, Kayanga 21. Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, CSSp
Same 22. Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa, (Askofu Msaidizi), Dar es Salaam
23. Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Ifakara 24. Mhashamu Askofu Bernadin
Mfumbusa, Kondoa 25. Mhashamu Askofu John Ndimbo, Mbinga 26. Mhashamu Askofu
Titus Mdoe, Mtwara 27. Mhashamu Askofu Joseph Mlola, ALCP/OSS, Kigoma 28.
Mhashamu Askofu Prosper Lyimo, (Askofu Msaidizi), Arusha 29. Mhashamu Askofu
Liberatus Sangu, Shinyanga 30. Mhashamu Askofu Edward Mapunda, Singida 31.
Mhashamu Askofu Beatus Urassa, Sumbawanga 32. Mhashamu Askofu Anthon Lagwen,
Mbulu 33. Mhashamu Askofu Filbert Mhasi, Tunduru-Masasi.
No comments
Post a Comment