Writen by
sadataley
8:52 PM
-
0
Comments
Umoja wa Mataifa umeziasa nchi za Afrika kuelekeza sera na bajeti zao za fedha katika utumiaji wa gari za nishati ya umeme ili kupunguza uchafuzi wa hewa.

Nasaha hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP) Erik Solheim, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wiki ya Uendeshaji Safi Afrika (Africa Clean Mobility Week) unaofanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Solheim ameueleza mkutano huo kwamba, kuna udharura kwa bara la Afrika kuanzisha mpango wa utumizi wa magari ya nishati ya umeme ili kupunguza kiwango cha uchafuzi wa hewa kutokana na kuongezeka kwa kasi uhamiaji wa watu mijini.
Amesema, kuna uwezekano mkubwa kwamba changamoto kubwa zaidi itakayozikabili nchi za Afrika katika miongo ijayo itakuwa ni ya ukuzaji wa miji kutokana na ongezeko la idadi ya watu watakaohitajia suhula za ziada na huduma ya usafiri.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP amezishauri serikali za nchi za Afrika zianze kuipanga upya miji kwa kutenga sehemu za watembeaji wa miguu na waendeshaji baiskeli kando ya barabara kuu ili kupunguza utumiaji wa magari na uchafuzi wa hewa.
Solheim amesema anashangaa kuona nchi za Afrika zinaendelea kuagiza magari ya mitumba kutoka nje ilhali inajulikana kuwa bei ya gari zinazotumia nishati ya umeme ni nafuu zaidi kulinganisha na zile zinazotumia petroli.
Amesisitiza kuwa nchi za Afrika zinahitaji kuanzisha utumiaji wa treni, magari na mabasi yanayotumia nishati ya umeme ili kupunguza uchafuzi wa hewa na msongamano wa magari na kutanabahisha kwamba ujenzi wa barabara kuu tu hautoweza kupunguza wingi wa magari mabarabarani.
Parstoday.com
No comments
Post a Comment