Writen by
sadataley
9:01 PM
-
0
Comments
Ushahidi unaonyesha kuwa, bara la Afrika sasa limegeuka na kuwa medani mpya ya mashindano ya kuwania ushawishi katika mgogoro unaonedelea kutokota baina ya Qatar na madola ya Kiarabu ya 3+1.

Tokea Juni 5 mwaka 2017, kumekuwepo na mzozo mkubwa baina ya Qatar na kundi la Kiarabu la 3+1 ambalo linajumuisha Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Bahraini ambazo ni nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi pamoja na Misri. Ukiachilia mbali vita vya maneno baina ya nchi hizo, inaelekea kuwa pande hizo mbili sasa zinawania kuwa na ushawishi katika nchi za bara la Afrika.
Sudan sasa imegeuka na kuwa kituo cha malumbano baina ya Qatar na nchi hizo za Kiarabu za kundi la 3+1.
Sheikh Mohammad bin Abdulrahman Aal Thani, Naibu Waziri Mkuu wa Qatar, wiki hii ameitembelea Sudan na kukutana na kufanya mazungumzo na wakuu wa nchi hiyo. Kabla ya hapo pia, mwezi Februari, balozi wa Qatar mjini Khartoum alimkabidhi Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo barua rasmi kutoka kwa Emir wa Qatar. Katika kujibu barua hiyo, Rais al Bashir alitaka uimarishwe zaidi uhusiano wa Doha na Khartoum.
Hayo yalijiri wakati ambao utawala wa Saudia na waitifaki wake wamekuwa wakiitaka Sudan ikate uhusiano na Qatar. Pamoja na kuwa serikali ya Sudan ina wasi wasi kuhusu ushawishi wa Qatar miongoni mwa wafuasi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin nchini humo, pia wakati huo huo inataka kuendelea kupokea misaada ya kifedha ya Saudia. Katika upande mwingine serikali ya Sudan hairidhii kuona ukuruba uliopo baina ya tawala za Misri na Saudi Arabia.
Kwa msingi huo, weledi wa mambo ya kisaisa kama vile Nasrudin Mohammad Adame wa Kituo cha Utafiti wa Kimataifa cha Al Maarifa cha Sudan anaamini kuwa, "Muungano wa Saudia na Sudan haujakuwa na faida kwani Saudia sasa imejiunga na Misri. Hii ni katika hali ambayo Misri inapinga pendekezo la kuwepo muungano baina yake na Saudia ukishirikisha Sundan." Anasema Qatar imefahamu vizuri hali hiyo na sasa inajikurubisha kwa Sudan.
Nukta muhimu hapa ni kuwa, wakati serikali ya Qatar inajitahidi kuwa na uhuisiano na nchi za Afrika kwa msingi wa kuheshimiana pande mbili, serikali za Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia na Misri zina mtazamo tofauti kwani zinataka kuingilia mambo ya ndani ya nchi za Afrika na kueneza machafuko na ukosefu wa amani katika nchi hizo.

Wiki hii pia, Makamu wa Pili wa Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Libya amesema kuwa Imarati inatumia pesa zilizozuiwa za Libya kuwaunga mkono wapiganaji wa kamanda mwenye utata nchini humo.
Mohammad Am'azb Makamu wa Pili wa Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Libya huku akitegemea taarifa za kuaminika ametangaza kuwa Imarati imetwaa na kutumia pesa za Libya zilizozuiwa katika mabenki ya Imarati kwa ajili ya kusaidia oparesheni za wapiganaji wa Jenerali Khalifa Haftar Kamanda wa Jeshi la Taifa la Libya mashariki mwa nchi hiyo.
Tunaweza kusema kuwa kinyume na kundi la nchi za Kiarbau za 3+1, Qatar inataka kuwa na uhusiano wa kuheshimiana na nchi za Afrika. Serikali ya Doha imerekebisha sera zake potovu zilizoanza mwaka 2011 za kuingilia masuala ya ndani ya nchi zingine hasa nchi za Kiarabu na sasa imerejea katika nafasi yake ya kabla ya mwaka 2011.
Parstoday.com
No comments
Post a Comment