Writen by
sadataley
11:50 AM
-
0
Comments
Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia Siraj Fegessa amesema sheria ya hali ya hatari itaendelea kutekelezwa nchini humo kwa muda wa miezi sita kufuatia kujiuzulu Waziri Mkuu Hailemariam Desalign.
Fegessa amewaeleza waandishi wa habari kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kukabiliana na machafuko yaliyolikumba taifa hilo la pili kwa idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika.
Amesema serikali imefanya jitihada kadhaa hapo kabla za kudhibiti machafuko lakini maisha ya watu yameendelea kupotea, watu wengi wamepoteza makazi yao na miundomsingi ya uchumi imeharibiwa.
Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia amesema, mbali na kutangazwa sheria hiyo ya hali ya hatari hatua nyengine zitakazochukuliwa na serikali zitatangazwa baadaye.

Waziri Mkuu wa Ethipia aliyejiuzulu Hailemariam Desalign
Katika hatua ya kushangaza, Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalign siku ya Alkhamisi alitangaza kujiuzulu wadhifa huo katika hotuba aliyotoa kupitia televisheni ya taifa, ikiwa ni mara ya kwanza katika zama za sasa kushuhudiwa waziri mkuu aliyeko madarakani nchini humo akichukua uamuzi wa kung'atuka madarakani. Alisema amefanya hivyo ili kurahisisha mchakato wa mageuzi nchini humo.
Siku ya Ijumaa serikali ilitangaza sheria ya hali ya hatari, uamuzi ambao unatazamiwa kuidhinishwa ndani ya muda wa wiki mbili na bunge ambalo viti vyake vyote 547 vinahodhiwa na muungano tawala wa vyama vinne vya siasa.
Mamia ya watu wamepoteza maisha nchini Ethiopia katika ghasia na machafuko ya ndani yaliyopamba moto zaidi mwaka 2015 na 2016 kutokana na malalamiko ya watu wa makabila ya Oromo na Amhara.
Mnamo Oktoba mwaka 2016 serikali ya Addis Ababa ilitangaza pia hali ya hatari ambayo ilidumu hadi mwezi Agosti mwaka uliopita wa 2017. Marufuku ya kutotoka nje ilitekelezwa wakati huo na watu wapatao 29,000 waliwekwa kizuizini.
PARSTODAY
No comments
Post a Comment