Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Friday, November 11, 2016

Maandamano dhidi ya Trump usiku wa pili Marekani

New Orleans protest

Image copyrightREUTERS
Image captionWaandamanaji wa kumpinga Trump mjini New Orleans
Maelfu ya watu waliandamana usiku wa pili nchini Marekani kupinga ushindi wa mgombea wa chama cha Republican Donald Trump, ingawa hawakuwa wengi kama usiku wa kwanza.
Waandamanaji sana wamekuwa vijana ambao wanasema uongozi wa Trump utazua migawanyiko kwa misingi ya rangi na jinsia.
Hata hivyo, polisi eneo la Portland wamesema wamekabiliana na wezi na waporaji pamoja na watu wengine waliokuwa wanawashambulia wengine.
Akijibu maandamano hayo, Bw Trump ameandika kwenye Twitter kwamba "si ya haki".
Awali, alikutana na Rais Barack Obama ikulu ya White House na kumweleza kama mtu mzuri.
Hata hivyo, mwandishi wa BBC anasema licha yao kusema mkutano huo ulikuwa wa kufana, Bw Trump bado anaonekana kuwa tayari kubatilisha mambo mengi aliyoyafanya Obama alipokuwa madarakani. Miongoni mwa hayo ni Obamacare, sheria ya bima ya taifa iliyowawezesha Wamarekani wengi zaidi kuliko awali kupata bima ya matibabu.
Image copyright@REALDONALDTRUMP
Waandamanaji walikusanyika katika miji mbalimbal Marekani Alhamisi jioni.
Polisi mjini Portland, Oregon, walisema maandamano hayo yanafaa kuchukuliwa kama ghasia. Walisema madirisha ya maduka yalivunjwa, na baadhi ya waandamanaji walibeba magongo na mawe.
Hakukuwa na ripoti za kuzuka kwa fujo katika maandamano mengine, ingawa waandamanaji Minneapolis walifunga barabara kuu njia zote mbili kwa muda.
Mjini Philadelphia umati wa watu ulikusanyika nje ya ukumbi wa baraza la jiji na kuimba "Not Our President" (Si Rais Wetu), "Trans Against Trump" (Trans Dhidi ya Trump) na "Make America Safe For All" (Ifanye Marekani iwe Salama kwa Wote).
Mjini Baltimore, polisi walisema watu 600 waliandamana kwa amani katika barabara za mji, na kuzuia magari kupita.
Wanafunzi wa shule za upili San Francisco, California nao walibeba mabango yenye rangi ya upinde wa mvua na wengine wakabeba bendera za Mexico.
Kundi ndogo la waandamanaji lilikusanyika nje ya jumba la Trump Tower mjini Chicago, siku moja baada ya maelfu ya waandamanaji kuandamana katikati mwa mji huo.
Baadhi ya wapita njia waliwashangilia lakini kuna dereva mmoja aliyewaambia "nyamazeni na mkubali demokrasia", shirika la habari la Associated Press liliripoti.
Waandamanji pia walikusanyika nje ya jumba kuu la Trump, Trump Tower mwaka New York kwa usiku wa pili.
Akiandika kwenye Twitter, Bw Trump aliwaeleza watu hao kama "waandamanaji wataalamu" na kusema kwamba "wamechochewa na vyombo vya habari".

Joto kimataifa

Hayo yakijiri, rais wa Mexico ameelezea matumaini kwamba taifa lake litakuwa na uhusiano mwema na Marekani chini ya Trump, licha ya kwamba amekuwa akitoa matamshi dhidi ya watu wa Mexico wakati wa kampeni.
Enrique Pena Nieto alisema yeye na Trump wamekubaliana kukutana, ikiwezekana kipindi hiki cha mpito, kabla ya Rais Trump kuapishwa Januari.
Eugene, OregonImage copyrightREUTERS
Image captionMaandamano pia yalifanyika miji midogo kama Eugene jimbo la Oregon
MinneapolisImage copyrightREUTERS
Image captionPolisi walifuatilia maandamano Minneapolis
Nchini Urusi, msemaji wa Rais Vladimir Putin alisema Bw Trump na kiongozi huyo wa Urusi "wanafanana sana" katika jinsi wanavyoitazama dunia.
Dmitry Peskov amesema wataalamu wa Urusi walikuwa wanawasiliana na maafisa wa Bw Trump wakati wa kampeni.
Lakini alisema serikali ya Urusi haikuhusika kwa vyovyote vile na kudukuliwa kwa barua pepe za maafisa wa kampeni wa chama cha Democratic, ambazo baadaye zilichapishwa katika mtandao wa ufichuzi wa Wikileaks.

Mazungumzo mazuri

Bw Trump awali alikuwa amesema ilikuwa ni "heshima kuu" kwake kukutana na Rais Obama wkwa mazungumzo kuhusu kipindi cha mpito na kupokezana mamlaka katika ikulu ya White House.
Bw Obama alisema anatilia umuhimu sana kuhakikisha kunakuwa na shughuli laini ya kupokezana madaraka.
Rais Barack Obama na Rais mteule Donald Trump katika Oval OfficeImage copyrightAP
Image captionRais Barack Obama na Rais mteule Donald Trump katika Oval Office
Melania Trump na Michelle ObamaImage copyrightWHITE HOUSE
Image captionMelania Trump na Michelle Obama wakizungumza White House
Wakati wa kampeni, Bw Obama alikuwa amesema Bw Trump hafai hata kidogo kuwa rais.
Rais mteule Trump aliandamana na mkewe Melania ziara yake White House, ambaye alikutana na Mama Taifa Michelle Obama.
Bw Trump baadaye aliandika kwenye Twitter kwamba alikuwa na "uhusiano mwema" na Obama, na kwamba mkewe "alimpenda Bi O sana."
Yeye na makamu wa rais mtarajiwa Mike Pence baadaye walikutana na Spika wa Bunge la Wawakilishi, mwanachama wa Republican Paul Ryan, na kusema wanataka sana kuanza kazi, "iwe ni kuhusu huduma ya afya au uhamiaji".
Bw Ryan alisema mkutano huo ulikuwa wa kufana.
Mwandamanaji San franciscoImage copyrightREUTERS
Image captionBaadhi ya walioandamana San Francisco siku ya kwanza walibeba mabango yanayosema "Not my president" (Si Rais wangu)
Chama cha Republican sasa kina wingi wa wabunge katika mabunge yote mawili ya Congress na itakuwa rahisi kwa Bw Trump kufanya mabadiliko anayotaka kutekeleza kuondoa baadhi ya sera na sheria za Obama, mfano kuhusu bima ya afya.
Kundi la kushughulikia shughuli ya mpito la Bw Trump litaongozwa na Chris Christie, gavana wa New Jersey, na lina wiki 10 kukamilisha maandalizi hayo.
Rais huyo mteule, ambaye hajawahi kuhudumu katika wadhifa wowote wa kuchaguliwa au kuteuliwa serikalini, amesema kipaumbele chake kitakuwa kufufua na kuimarisha miundo mbinu ya nchi hiyo pamoja na kukuza ukuaji wa uchumi wa taifa hilo maradufu.
Mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha Republican Reince Priebus alisema: "Donald Trump anachukulia hili kwa uzito sana," na kuongeza kwamba mfanya biashara huyo tajiri atatumia uwezo wake wa kutetea na kufanikisha mikataba ya kibiashara kuhakikisha mambo mema "yanatendeka kwa Wamarekani" haraka iwezekanavyo.
Kama Rais mteule, Bw Trump ana haki ya kupokea taarifa za kila siku za ujasusi sawa na Rais Obama, ambazo ni pamoja na habari kuhusu operesheni za kisiri za Marekani pamoja na habari za kijasusi zinazokusanywa na mawakala 17 wa ujasusi za Marekani.
Bw Chris ChristieImage copyrightREUTERS
Image captionBw Chris Christie
Bw Trump na kundi lake wanaaminika kuwa tayari kujaza nafasi kuu za usalama wa taifa haraka iwezekanavyo watakapoingia madarakani.
Lakini haijabainika nani atakuwa kwenye baraza lake la mawaziri au atakayejaza nyadhifa kuu wakati wa utawala wake kama vile mkuu wa majeshi.
Kunao wanaotarajiwa kupewa nyadhifa kuu wakiwemo Christie, spika wa zamani wa bunge Newt Gingrich na meya wa zamani wa New York Rudy Giuliani, mmoja wa washauri wakuu wa Bw Trump ambaye wengi wanasema huenda akafanywa mwanasheria mkuu au mshauri mkuu wa masuala ya usalama wa taifa.
Baada ya kupata hasara kubwa kutokana na ushindi wa kushangaza wa Bw Trump, masoko ya hisa yameanza kuimarika.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment