Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Friday, April 8, 2016

Waumini KKKT Mufindi wahama Dayosisi wakimpinga Askofu

Dar es Salaam. Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini, Jimbo la Mufindi wametoa tamko la kuhamia Dayosisi ya Iringa kwa madai ya kuchoshwa na mgogoro wa siku nyingi baina yao na Askofu wao, Isaya Mengele. Mbali na mgogoro huo, tamko hilo lilidai kwamba hawawezi kuendelea kubaki Njombe kwa madai kuwa jimbo hilo linapaswa kuwa Iringa kulingana na mipaka ya kimikoa. Juzi, waziri wa zamani, Joseph Mungai aliandika barua kwa Mkuu wa KKKT, Dk Frederick Shoo akimwomba achukue hatua za haraka katika mambo matano likiwamo la kuzingatia hoja za Wakristo wa jimbo hilo anaodai wanatengwa na kunyanyaswa na Askofu Mengele. Akizungumza tamko hilo jana, Askofu wa KKKT Jimbo la Iringa, Dk Owdenburg Mdegela alisema amelipokea na ameamua kuwapokea kwa mikono miwili huku akiwasihi watulie kusubiri usuluhishi utakaofanywa na viongozi wa kanisa hilo. Akisimulia hali halisi, Dk Mdegela alisema Februari 26, waumini hao walitaka kuandamana hadi Arusha ili kumuomba Askofu Shoo aingilie kati mgogoro huo. Alisema kabla ya kufanya maandamano hayo, waumini hao walikwenda Iringa kumsihi awapokee jambo lililomfanya awatulize akiahidi kuzungumza na Askofu Mengele ili kumaliza tatizo lililopo. “Niliwaomba watulie, nikawasiliana na Askofu Mengele nikimsihi aumalize mgogoro huu kwa mazungumzo. Hata hivyo, mgogoro huu ni wa kihistoria na unahitaji hekima na maombi kuumaliza,” alisema Dk Mdegela. Alisema Machi 8 waumini hao walimfuata tena safari hii walimpelekea tamko kwamba wameamua kuihama dayosisi yao na kuhamia Iringa. Dk Mdegela alisema hatua ya waumini hao ilimuudhi Askofu Mengele ambaye aliamua kumfukuza kazi Mkuu wa Jimbo la Mufindi, Mchungaji Anthony Kipangula na hivyo kuwaudhi zaidi waumini. Mchungaji Kipangula alipopigiwa simu alikiri kuwapo kwa tatizo la muda mrefu baina ya waumini na Askofu Mengele. “Kwa sasa nipo Mwanza, hivyo sitaweza kuongea zaidi masuala ya jimbo japo mgogoro huu ni wa muda mrefu, waumini wanataka wahamishiwe Iringa na si kuendelea kuwapo Njombe,” alisema. Katika tamko lao, waumini hao walidai kuchoshwa na mgogoro huo na kwamba hawatatambua uongozi wa Askofu Mengele. Katiba barua yake, Mungai alimuomba Dk Shoo kuunda tume ili ichunguze mgogoro huo na kusikiliza pande zote mbili. Askofu Mengele alipopigiwa simu kuzungumzia tatizo hilo, alipokea lakini ilikatika na alipopigiwa tena haikupatikana.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment