Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Thursday, July 30, 2015

Lowassa, mkewe watua Chadema, wakabidhiwa kadi

Hatimaye ameingia Chadema. Ilianza kama uvumi lakini jana ilikuwa dhahiri baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutangaza rasmi kukihama chama tawala, CCM na kujiunga na Ukawa kupitia Chadema, huku akisisitiza; “Sasa basi, imetosha.” Baada ya kukabidhiwa kadi ya Chadema na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Lowassa alisema amejiunga na chama hicho kikuu cha upinzani ili kutekeleza azma yake ya kuwakomboa Watanzania na kuendeleza safari ya matumaini kupitia Ukawa. “CCM kimepotoka, kimepoteza mwelekeo na sifa za kuendelea kuiongoza Tanzania,” alisema Lowassa katika mkutano wa kumkaribisha Chadema uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Ledger Bahari Beach na kurushwa moja kwa moja na vituo kadhaa vya televisheni na redio. Dakika chache baada ya mkutano huo, CCM kupitia mitandao yake ya kijamii ilitangaza kuitisha mkutano wa wanahabari leo mchana kutoa taarifa muhimu, ikiaminika kuwa utakuwa wa kumjibu kiongozi huyo. Katika mkutano huo, Lowassa alitumia dakika 13 kueleza sababu za kujiunga Chadema, mbele ya wenyeviti wenza wa vyama vinavyounda Ukawa; Mbowe, Dk Emmanuel Makaidi (NLD), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF). Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, Naibu wake (Bara), John Mnyika, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu hawakuonekana na hawakupatikana kuzungumzia sababu za kutokuwapo katika tukio hilo muhimu. Lowassa ambaye aliingia katika ukumbi huo saa 10.20 jioni akiwa ameambatana na mkewe, Regina, watoto wake, ndugu na jamaa, pia aligusia sakata la kampuni ya kufua umeme ya Richmond lililosababisha ajiuzulu wadhifa wa waziri mkuu mwaka 2008, kwamba alifanya hivyo kwa manufaa ya nchi na alishindwa kuvunja mkataba huo kutokana na amri kutoka mamlaka ya juu. Ahama na wimbo wake Wakati Lowassa akizungumza, wanachama wa Chadema walikuwa wakiitikia ‘peoples power’, na alipomaliza hotuba yake wanachama wao waliimba wimbo maalumu kuwa wana imani naye, “Tuna imani na Lowaasaa, oya oya oyaa.” Wimbo huo pia uliimbwa na wanachama wa CCM katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho mjini Dodoma, baada ya jina mbunge huyo wa Monduli kutokuwamo kati ya wagombea watano waliopitishwa na Kamati Kuu kuwania nafasi ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ambayo ilikwenda kwa Dk John Magufuli. Mchakato CCM Katika hotuba yake, Lowassa aligusia jinsi mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM ulivyogubikwa na mizengwe na kusisitiza: “Nimetumia muda huu kutafakari kwa kina yaliyotokea Dodoma na hatima yangu katika siasa nchini. Pamoja na yaliyotokea Dodoma azma yangu iko palepale ya kuanza mchakamchaka wa maendeleo ya kuiondoa nchi katika umaskini. “Najua sote tumevunjika moyo kwa yaliyotokea Dodoma na mazingira yaliyopelekea matokeo yale. Mchakato uligubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa maadili, uvunjaji wa katiba na taratibu za uchaguzi za CCM.” Alisema mchakato huo ulisimamiwa kwa upendeleo wa dhahiri na chuki iliyokithiri dhidi yake... “Kikatiba Kamati ya Maadili si chombo rasmi na haina madaraka ya kuchuja na kupendekeza majina miongoni mwa wale wanaoomba kugombea urais kupitia CCM. Kilichotokea Dodoma ni kupora madaraka ya Kamati Kuu na kukiuka katiba ya CCM.” Alisema vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu viliitishwa na kuburuzwa ili vitekeleze azma ya watu binafsi bila kujali demokrasia, katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi ndani ya CCM. “Kibaya zaidi ni kile kitendo cha kuwanyima wagombea wote 38 haki ya kujieleza mbele ya Kamati Kuu,” alisema. Alisema Watanzania walitarajia chama kinachoongoza nchi kiwe mfano wa utawala wa sheria na kinara katika kutetea misingi ya haki na demokrasia na siyo kuihujumu, lakini yaliyotokea Dodoma yameitia dosari nchi. Msimamo “Sikutendewa haki. Kwa mantiki hii nitakuwa mnafiki kama nitaendelea kujidanganya mimi mwenyewe na umma wa Watanzania kwa kusema kuwa bado nina imani na CCM…, CCM niliyoiona Dodoma siyo tena kile chama nilichokulia na kilichonipa malezi na maadili ya siasa yaliyojengwa kwenye misingi ya haki, usawa na uadilifu,” alisema. Lowassa alisema hata Mwalimu Julius Nyerere alisema CCM siyo baba yake wala mama yake na kama Watanzania hawapati mabadiliko ndani ya CCM watayatafuta nje ya chama hicho. “Baada ya kutafakari kwa kina nimeamua kuwa kuanzia leo ninaondoka CCM na kuitikia wito wa Ukawa kupitia Chadema kuungana nao katika kuleta mabadiliko ya kweli ya nchi yetu,” alisema. Richmond Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Lowassa alizungumzia sakata la Richmond akisema anashangazwa jinsi anavyohusishwa nalo licha ya kuwa ameshalitolea ufafanuzi na kuwataka wenye ushahidi waupeleke mahakamani. Alisema alijiuzulu uwaziri mkuu kwa niaba ya Serikali huku akisisitiza kuwa wakati huo waliingia mkataba na kampuni hiyo kutokana na shida ya umeme wakati huo, lakini baadaye waligundua kuwa ilikuwa na matatizo mengi na alipotaka kuvunja mkataba huo alizuiwa na mamlaka za juu. Alisema walikaa kikao na makatibu wakuu kujadili suala hilo na kwamba mmoja wa makatibu hao alitoka nje na kuzungumza na simu kwa zaidi ya saa moja, baada ya kurudi katika kikao alimueleza kuwa mkataba huo usivunjwe na kwamba ni amri kutoka mamlaka ya juu. Mbowe aweka msimamo Katika hotuba yake ya kumkaribisha Lowassa, Mbowe alisema wakati jina la waziri mkuu huyo wa zamani likikatwa CCM, alifurahi na kuamini kuwa atajiunga na upinzani. Alisema baada ya kuibuka kwa minong’ono juu ya Lowassa kuhamia Chadema, alipigiwa simu na viongozi wengi wa CCM wakimtahadharisha kuwa wasikubali ajiunge katika chama hicho. “Hata mimi niliwajibu kuwa hatuwezi kumpokea Lowassa, tena niliwajibu kwa Kiingereza, “over my dead body (sitampokea mpaka kufa)”. Lakini kumbukeni kuwa Chadema ni chama cha kujenga mshikamano na hakiwezi kuhukumu bila ushahidi,” alisema Mbowe. Akifafanua kauli ya ‘kula matapishi yake’, inayotokana na viongozi wa chama hicho kuwahi kumtuhumu Lowassa katika masuala mbalimbali ya ufisadi miaka ya nyuma alisema: “Hatuwezi kufikiri mambo mema mapya kwa kutafakari mambo mabaya ya zamani. Ni nani aliye mtakatifu mpaka awe na uwezo wa kushika jiwe na kumpiga mwenzake, hii si CCM tu hata Chadema au Lowassa.” Alisema Ukawa ikichukua dola haitaongoza nchi kwa kulipa visasi, bali kuwaletea Watanzania maendeleo huku akisisitiza kuwa kumleta Lowassa Ukawa haikuwa kazi rahisi kwani vilifanyika vikao vingi. “Lowassa ni waziri mkuu wa kwanza mstaafu kusema CCM si mama yake. CCM kimejenga hofu kwa wanachama wake. sisi Ukawa tunaamini nchi yetu inahitaji fikra na mtazamo mpya, tumevutana sana lakini tumeendelea kuwa kitu kimoja kwa masilahi ya Watanzania,” alisema. Mbowe alisema angekuwa mwendawazimu kumkataa Lowassa ambaye ana nguvu kubwa ya kisiasa kujiunga na Chadema wakati atakiletea chama hicho wanachama zaidi ya milioni moja na kusisitiza kuwa mtaji wa chama cha siasa ni watu. “Lowassa hujui tu minyororo uliyoifungua baada ya kuondoka CCM, umefungua minyororo ya watu wengine akiwamo Ole Medeye yule pale (akimwonyesha, Naibu waziri wa zamani, Goodluck). Siasa ni mchezo unaobadilika kulingana na wakati,” alisema. Alisema chama ambacho hakiamini katika mabadiliko si chama na kwamba Chadema hakiongozwi kwa kauli yake (Mbowe), bali katiba, kanuni, maadili na miiko. “Chadema hatupo kugombea vyeo, bali kulikomboa Taifa na kazi iliyopo mbele yetu ni kubwa, hivyo viongozi na wanachama wa Chadema na Ukawa msihofu. Aliyeingia Chadema 1992 na mwaka huu wote wana haki sawa. Wapo watu tuliowatukana sana huko nyuma lakini hiyo haizuii kuwapokea,” alisema na kuongeza: “Watanzania ondoeni hofu maana tunapambana na mfumo si mtu, Lowassa na wenzake watatupa mbinu za kupambana na mfumo. Leo hii hata ukimchukua malaika na kumpeleka CCM baada ya mwezi mmoja atageuka ibilisi.” ‘Ampongeza’ Kikwete Mbowe alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kitendo cha kuliondoa jina la Lowassa kuwa mgombea urais wa CCM, kwa maelezo kuwa wakati wakimuondoa wapinzani walikuwa wakifurahia. Mbali na Mbowe, Dk Makaidi, Mbatia na Makamu Mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji walipongeza kitendo cha Lowassa kujiunga na Ukawa, huku Mbatia akisema Tanzania bila CCM inawezekana. “Sasa ni Tanzania kwanza na vyama baadaye. Hakuna machafuko yatakayotokea nchini lakini walioko madarakani wasituchokoze maana hoja za kupambana nao tunazo,” alisema Mbatia Ulinzi mkali Watu waliofika katika ukumbi huo, wakiwamo waandishi wa habari walikuwa wakikaguliwa kwa vifaa maalumu kabla ya kuingia ndani. Ukaguzi huo ulifanywa na walinzi wa Chadema (Red Brigade) na walinzi wa kampuni binafsi. Waandishi walioingia ndani ya mkutano huo waliitwa kwa majina yaliyokuwa yameorodheshwa mapema, hata walipokuwa ndani ya ukumbi walikaa maeneo waliyopangiwa na kutakiwa kutosimama hovyo. Chanzo:mwanancho.co.tz
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment