Writen by
sadataley
5:23 PM
-
0
Comments
Na Goodluck Eliona na Fidelis Butahe, MwananchiWakati Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakitarajiwa kuendelea na vikao mjini Dodoma kesho, Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Antony Lusekelo, amesema kuwa hali ya kisiasa hairuhusu nchi kupata Katiba Mpya kwa sasa, akishauri Bunge hilo kusitishwa hadi baada ya uchaguzi mkuu mwakani.
Lusekelo pia ameonya wajumbe wa Bunge hilo akisema
iwapo wataendelea na mchakato huo, Katiba itakayoandikwa itakataliwa na
wananchi baadaye hivyo kuwa wamepoteza muda na fedha za walipakodi
bure.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano
maalumu ofisini kwake jijini hapa juzi, Mchungaji Lusekelo alisema kuwa
Mchakato wa Katiba Mpya, umevurugika kutokana na wanasiasa kujiona
miungu watu na kukataa kusikiliza ushauri wanaopewa.
“Kwa upande wangu, kama viongozi wangekuwa
wanatusikiliza, mchakato huu usingefika ulipofika leo. Hii misukosuko
isingetokea, wanasiasa wetu wana tatizo hilo. Ni miungu watu, wana
shingo ngumu utafikiri Farao,” alisema Mchungaji Lusekelo.
Mchungaji huyo anayefahamika zaidi kwa jina la
Mzee wa Upako, alisema kuwa viongozi hawataki kusikiliza ushauri kutoka
kwa watu wengine kwa sababu wanaamini kuwa wamesoma, wana hekima,
wamesafiri sana na wanaijua nchi kuliko mtu mwingine.
“Kwa hiyo tatizo limeanza baada ya wanasiasa
kuweka pamba masikioni. Nchi inahitaji uwanja mpana zaidi wa mawazo
ndipo unaweza kuijenga, hasa katika mfumo wa sasa wa uhuru wa habari na
vyama vingi. Dunia ya sasa siyo ya mwaka 1970,” alisema na kuongeza:
“Ni busara tu, haihitaji kwenda shule, kusema kuwa
sisi tunaijua nchi, nani asiyeijua nchi yake? Kwani sisi ni Wazambia?
Kila mtu anaijua nchi yake katika eneo lake.
“Iwapo viongozi watalazimisha kupatikana kwa
Katiba Mpya, haitakuwa na uzito, itapoteza heshima muda mfupi kwa kuwa
itapingwa na wananchi.
“Kwa hiyo, mtapata hasara kubwa sana kwamba
mlitumia Sh75 bilioni kwa Warioba (Jaji Joseph Warioba, Tume ya
Mabadiliko ya Katiba) na bilioni kadhaa kwenye Bunge la Katiba.
Atakayeumia sana Katiba Mpya ikianguka ni yule aliyeanzisha wazo.
Tanzania haiwezi kuandika Katiba katika mazingira haya.”
Aliongeza kuwa katika hali ya kawaida hauwezi kuanzisha mashindano ya mbio ukiwa peke yako halafu ukajipongeza kwa kushinda.
“Au mpira uko peke yako, unafunga goli, halafu unasema ehhh nimefunga, haiwezekani,”alisema.
Kiongozi huyo, alisema kwamba anaamini Rais ajaye
wa awamu ya tano, ataweza kuwaunganisha wananchi waliotofautiana
kutokana na Mchakato wa Katiba kwa kuwa mazingira ya sasa hayawezi
kuwapa wananchi Katiba wanayoitaka.
“Mwaka 2016 unamwacha rais wa awamu ya tano atusaidie kuirudisha
nchi pamoja, tuligawanyika, unaponya majeraha halafu mwaka 2017 Bunge
la Katiba linaendelea,” alisema.
Hata hivyo, alieleza kwamba kabla ya uchaguzi mkuu
wa mwaka 2015 kufanyika, Bunge la Jamhuri ya Muungano litapaswa
kufanyia marekebisho baadhi ya vipengele kwenye Katiba ya sasa
vinavyolalamikiwa, ambavyo ni suala la mgombea binafsi, Tume ya Uchaguzi
na madaraka ya Rais.
“Rais apunguziwe madaraka kidogo kwa sababu Rais
wa Tanzania ana madaraka makubwa mno, ukimtoa Mungu anakuja yeye.
Bahati, Mungu ametusaidia katika vipindi vinne, tumepata marais ambao
tumeishi kwa huruma zao,” alisema.
Vilevile aliwataka wanasiasa kukumbuka kuwa amani
na chakula kinachopatikana nchini leo ni matokeo ya mazingira
yaliyoandaliwa na viongozi miaka ya 1960 na 1970 na kwamba uamuzi wowote
wanaofikia leo lazima ukusudie kulinufaisha taifa kwa miaka mingi
ijayo.
“Viongozi wa sasa hivi hawataki kutengeneza
mazingira ya miaka 30, 40 ijayo, hawajui jamii lazima ibadilike, sasa
wakati wote mabadiliko ukiyasubiri yaje huwa yanajileta na maafa sana,”
alieleza.
Joto la uchaguzi
Akizungumzia kuhusu joto la kisiasa kuelekea
Uchaguzi Mkuu wa Rais mwaka 2015, Mzee wa Upako alisema unatarajiwa kuwa
mgumu kwa kuwa tayari watu wenye majina makubwa wameshaanza kuonyesha
nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu nchini.
“Ingekuwa nafuu kama rais huyu anaendelea, lakini
tunabadilisha rais na ukisoma hisia, unaona wanaogombea urais hata ndani
ya CCM ni wakubwa, siyo watu wadogo, wana makundi makubwa kwenye chama
chao,” alisema.
Alibainisha kuwa kutokana na mchakato wa urais
kuanza chini kwa chini, baadhi ya wananchi na viongozi wameanza
kugawanyika kila mtu akimtaka rais atakayenufaika naye.
Pia, alisema katika uchaguzi huo, siyo vyema
kupuuza nguvu ya vyama vya upinzani kwa kuwa vina wafuasi wengi baadhi
ya maeneo nchini.
“Unaweza kupuuza nguvu ya Chadema, NCCR-Mageuzi na
CUF huku Tanzania Bara, lakini huwezi kupuuza nguvu ya CUF Zanzibar.
Wabunge wote wa CUF na wawakilishi wao hawapo kwenye Bunge la Katiba,
ukitoa Hamad Rashid hawako wote. Nguvu ya kisiasa Zanzibar kati ya CUF
na CCM ni asilimia moja kwa 49,” alisema.
Sifa za Rais ajaye; vijana wakae kando
Akizungumzia kuhusu sifa za rais ajaye, alisema
hata ikitokea kijana mwenye miaka 45 akiingia katika kinyang’anyiro
hicho, hawezi kupata nafasi kwa kuwa umri huo hautoshi kulifahamu taifa
vizuri.
“Naamini katika umri, unaweza kusema Mwalimu
Julius Nyerere alikuwa na miaka 38 alipokuwa Waziri Mkuu, hayo yalikuwa
ni mazingira ya wakati ule, lakini siyo kama leo,” alisema na kuongeza:
“Rais anatakiwa kuanzia miaka 50 na kuendelea, huo
ndio ukweli hata kama watasema urais ni taasisi kwa miaka 40 umeijua
nchi wapi? Hata akina Nyerere (Julius Nyerere) iliwasumbua sana.”
Alizitaja sifa nyingine kuwa ni pamoja na kujua
matatizo ya Watanzania ukiwamo umaskini, uzalendo, mwadilifu ambaye hana
kashfa, siyo mdini wala mdhehebu, rais ambaye ataendelea kuwaunganisha
Watanzania na atakayesimamia Katiba ya nchi.
“Sijajua Katiba ya sasa itaitamkaje Zanzibar,
tupate watu wanaosimamia Katiba, sasa unaona Katiba ya Zanzibar imevunja
Katiba ya Jamhuri wa Muungano. Tunataka rais wa awamu ya tano ambaye ni
jasiri, ukicheza na matendo yanayoshiria uvunjifu wa amani rais anakuwa
mkali kwa wahalifu,” alisema.
Kuhusu baadhi ya watu wanaotajwa kutaka kugombea
urais, alisema baadhi yao wana sifa alizozitaja isipokuwa wale ambao
walishakuwa kwenye madaraka wakashindwa kuleta maendeleo.
“Sasa wewe serikalini ulisahau nini? Ulikaa pale
miaka yote, chochote haujaonyesha, sasa unataka kurudi tena kwa njia
nyingine, haiwezekani. Hauwezi kupata mabadiliko kwa kutumia watu
walewale kwa njia zilezile, kwa hiyo lazima upate watu ambao hawajawahi
kushika madaraka makubwa ya nchi au walishika madaraka makubwa
walionyesha utendaji.”
Kuhusu maadili ya viongozi wa umma
Mzee wa Upako alisema ingawa hakuna kipimo cha mtu
aliyejilimbikizia mali, viongozi wanaofanya hivyo ni wale yenye hofu na
wasio na uhakika na maisha yao baada ya kustaafu.
“Sisi hatukatai mtu kuwa na mali, lakini apate katika njia
iliyokuwa halali. Haumizi wenzake na kuliingiza taifa kwenye mikataba
isiyo na tija. Binadamu anastahili kula, hastahili kuwa mlafi,
anastahili kuwa na mali, lakini siyo mali iliyopitiliza katikati ya watu
maskini,” alisema.
Akitoa mfano namna maisha ya viongozi wa umma na
watoto wao yalivyokuwa miaka ya 1970, alisema: “Mimi nimesoma na watoto
wa Mkuu wa Mkoa Mwakabongo, wadogo zake Waziri Mwakawago, watoto wa
Makweta shule moja. Wote tulikuwa tunavaa makobazi.”
Alisema hali ni tofauti hivi sasa, ambapo kuna
shule za maskini na matajiri. Viongozi waliojilimbikizia mali ni vizuri
wakaifikiria zaidi jamii, maana ikisambaratika hata mali yao haitakuwa
na thamani.
“Hata ukikimbilia Ulaya kunakuwa kuzuri tu kama
nyumbani kuna amani. Nasema wenzetu wenye dhamana wafanye jitihada
kulitoa taifa kwenye umaskini.”
Vitega uchumi na amani nchini
Mzee wa Upako, alisema kuwa baada ya miaka 10
Tanzania haipaswi kuwa katika hali ya kiuchumi iliyonayo sasa na kwamba
kama hakutakuwa na mabadiliko, amani itatoweka nchini.
“Kama nchi hii itakuwa maskini hivi kwa miaka 10
ijayo usitegemee itakuwa kisiwa cha amani tena. Huku chini kumeshaanza
kuteketea, ukipata ajali hapa watu hawakimbilii kukuokoa wanakimbilia
kukusachi. Viashiria vimeshaanza kuonyesha kwamba watu wanaendekeza
njaa, kuliko utu wao.
No comments
Post a Comment