Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Wednesday, July 30, 2014

MARIDHIANO: Katiba ,Katiba ,Katiba


“Ni muhimu  kudumisha amani nchini, tusizipe nafasi tofauti zetu za kidini kwani tusipokuwa waangalifu tunaweza kusababisha mvurugano katika jamii yetu” Alhad Mussa Salum 
Na Waandishi Wetu, MwananchiDar na Mikoani. Karibu katika kila mkusanyiko wa swala ya Idd el Fitri, neno “Katiba” lilitajwa wakati viongozi wa dini ya Kiislamu walipokuwa wakitoa mawaidha yao ya sikukuu hiyo kusherehekea kumalizika kwa Mwezi Mtukufu wa Mfungo wa Ramadhani.
Katika mahubiri hayo, viongozi hao wa kidini walitaka mchakato wa Katiba uzingatie masilahi ya umma.
Mahubiri hayo yamekuja zikiwa zimebaki siku saba kabla ya vikao vya Bunge Maalumu la Katiba kuendelea mjini Dodoma, lakini kukiwa na sintofahamu kutokana na wajumbe wanaounda Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao kwa madai ya kutozingatiwa kwa maoni yaliyotolewa na wananchi.
Ukawa wanadai mjadala wa Katiba ni lazima ujikite kwenye Rasimu ya Katiba, ambayo imebeba mapendekezo ya wananchi na hali kadhalika kutaka wajumbe wenzao, hasa kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) kuacha kujenga hoja kwa kutumia kejeli, matusi na mizaha.
Jijini Dar es Salaam, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), liliisihi Ukawa kurudi bungeni ili kuweza kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya, lakini likasema mjadala huo uzingatie Rasimu ya Katiba.
Katika salamu zake za Idd, Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaji Suleiman Lolila alisema tayari fedha nyingi za umma zimeshatumika kuandaa mchakato wa Katiba Mpya, hivyo siyo busara kususia mchakato wake katika hatua zake za mwisho.
“Baraza linawasihi waliosusia warejee bungeni kwa sababu gharama kubwa zimeshatumika na kama kuna tofauti ziende zikajadiliwe na kumalizwa ndani ya Bunge,” alisema Lolilo.
Aliongeza kuwa Baraza linasikitika kwani maoni ya Waislamu hayakutiliwa maanani katika kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya na kwamba wanaamini yatazingatiwa katika hatua zinazofuata za mchakato huo.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akihutubia Baraza la Idd jijini Dar es Salaam, alisema  mchakato wa Katiba Mpya una lengo zuri kwa masilahi ya taifa na katika mtikisiko ambao wamepitia hadi sasa ni vyema ukafikia mwisho na maelewano yapatikane.
“Walioko nje ya Bunge nawaomba warudi ndani kwani huko ndiko tunakoweza kujadiliana, tukatofautiana na kufikia hatua kufika makubaliano na nashukuru hata viongozi wa dini mmeligusia hilo,” alisema Pinda.
Alieleza kwamba kwa sasa kilio cha Watanzania wengi ni kuona Bunge la Katiba likiendelea kwa wale walio nje kurudi ndani kisha kujitazama upya na kupitia kuhusu udhaifu wote wa Katiba ya zamani na kurekebisha kwa ajili ya kupata Katiba nzuri itakayotupeleka mbele kwa miaka mingine mingi ijayo.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment