Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Thursday, July 11, 2013

Serikali inavyohangaika kuziba aibu baada ya viongozi kufariki

Na Dismas Lyassa, Mwananchi
Karibu viongozi wengi waliofariki nchini, kilichofuatia kabla ya kuzikwa kwao ni Serikali kuingia gharama za kutengeneza mazingira kwa ajili ya msiba kufanyika vizuri, iwe ni kupitisha greda ili magari yaweze kupita, kuingiza umeme au aina nyingine ya huduma ambazo zinaonekana ni muhimu kuwepo.
Hali hii imekuwepo kwa miaka mingi, huku kukiwa hakuna dalili za kukoma. Hata kama matengenezo hayo yamekuwa yakitofautiana ukubwa aliyefariki kutokana na aidha cheo chake  au namna eneo husika lilivyo, utafiti unaonyesha ni kawaida mno, kusubiri matengenezo kufanyika kabla ya mazishi ya viongozi nchini.
Hayati Julius Nyerere
Kwa mfano Oktoba 14 1999, Rais wa kwanza wa Tanzania,  Julius Nyerere alifariki dunia, kisha mwili wake ukapelekwa kijiji cha Butiama, mkoani Mara kwa ajili ya mazishi. Lakini baada tu ya tangazo la kifo chake, kukaibuka matengenezo kadhaa hasa ya miundombinu ikiwemo barabara.
Edward Sokoine
Hali ilikuwa hivyo pia kwa Waziri mkuu,  Edward Sokoine baada ya kufariki 12 Aprili 1984. Barabara zilikarabatiwa haraka ili kuhakikisha mazishi yake ambayo yalifanyika Monduli yanafanyika vema.
Mazishi ya Kawawa
Kama hiyo haitoshi, Serikali ilifanya jambo katika mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu, Mzee Rashid Mfaume Kawawa (83), aliyefariki dunia Disemba 31, 2009.
Rais Jakaya Kikwete na mkewe, Mama Salma, ndio walioongoza maelfu ya wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama kutoka ndani na nje ya nchi, katika mazishi yaliyofanyika kijiji cha Madale, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Hali imekuwa hivyo na imeendelea kuwa hivyo kwa viongozi wengine, kwa mfano hivi karibuni Waziri mkuu, Mizengo Pinda  aliongoza mamia ya waombolezaji kumzika aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Timoth Apiyo, nyumbani kwake kijiji cha Marasibora, kilometa 56 kutoka Musoma mjini, mkoani Mara.
Pinda  alitoa pole kwa familia na wakazi wa Kijiji cha Mara Sibora, Wilaya ya Rorya na Mkoa wa Mara kwa kumpoteza kiongozi na mzalendo aliyeitumikia nchi yake kwa uadilifu.
Wengine waliohudhuria maziko ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu); Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue; Makatibu Mkuu Viongozi wastaafu, Balozi Paul Rupia, Balozi Martin Lumbanga na Philemon Luhanjo pamoja na mke wa hayati Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere pia walishiriki.
Apiyo (82) alifariki hospitalini, Millpark, Johannesburg Afrika Kusini usiku wa Juni 10, mwaka huu alikokwenda kutibiwa na mwili wake kurejeshwa nchini wiki hii.
Alistaafu kuwa Katibu Mkuu wa Rais, Ikulu, sasa Katibu Mkuu Kiongozi, mwaka 1986. Ameacha mjane na watoto saba.
Wasifu uliotolewa kabla ya mwili wake kushushwa kaburini, ulielezea utumishi wake uliotukuka.  Alianza utumishi wa Serikali katika ngazi ya chini akiwa Bwana shamba, baada ya kuhitimu Shahada ya Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda.
Afya yake ilianza kutetereka mwaka 1996 baada ya kupata ugonjwa wa kiharusi. Aliwahi kutibiwa India na Afrika Kusini, kabla ya hali yake kuzorota zaidi mapema mwezi huu na hatimaye kukutwa na mauti.
Alipolazwa ni kwenye kaburi lililo ndani ya uwanja wa nyumba yake, kando ya kaburi la marehemu mke wake, Rhoda Apiyo, aliyefariki mwaka 2006.
MAISHA KATIKA KIJIJI  ALICHOZIKWA
Hali katika kijiji cha Marasibora ni mbaya; Hakina umeme, barabara, maji, huduma za afya, elimu na huduma zingine za kijamii.
Apiyo alifuata nyayo ya hayati Nyerere ambaye kipindi cha utawala wake hakupenda kujilimbikizia mali bali aliangalia maeneo mengine kwanza na kujikuta alikozaliwa panabaki katika hali ya kawaida.
Siku ya mazishi yake, wapo waliotokwa machozi kutokana na kuona hali duni ya kijiji cha kiongozi huyo. Hali ni mbaya mno, ukilinganisha na vijiji vya baadhi ya viongozi waliopo madarakani ambao wamejitahidi kutengeneza kwao.
Hali mbaya ya shule
Kilicho watonesha wengi zaidi ni hali halisi ya shule. Zko shule nyingi ambazo wanafunzi wanakalia mawe; hakuna madawati kiasi kwamba mawe ndiyo yamekua madawati pia ubovu wa majengo hali inayowasababisha walimu wengi kukataa kuhamia shule hiyo.
SIKU YA MSIBA
Serikali ilitandaza nyaya za umeme takribani mwaka zaidi ya moja lakini zilikuwa kama mapambo kwani hadi Apiyo anafariki hakukuwa na mwanga wa umeme, ni siku ya msiba wake ndio transfoma ya kusambaza umeme ilifungwa, kijiji kilipata umeme kwa mara ya kwanza tangu kuzaliwa kwa ulimwengu. Hata hivyo umeme uliwashwa kwenye eneo la msiba tu.
Marehemu Apiyo alitamani kuuona umeme ukifanya kazi kijijini kwake akiwa hai lakini cha kushangaza amefariki bila umeme kuwaka. Serikali ilipata aibu kubwa pale ilipopata taarifa juu ya kifo cha Apiyo kwani hakuna kitu cha maana alichofanyiwa na Serikali katika makazi yake.
Majengo ya aibu
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia majengo mabovu ikiwepo lile la Ofisi ya Serikali ya Kijiji ambayo imemfanya Mwenyekiti wa kijiji hicho, Sproza Charles Oele kuhamishia ofisi yake katika jengo la iliyokua Idara ya Maji ambalo angalau kidogo lina hali nzuri.
Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Marasibora, Samwel Zakaria alipoulizwa kuhusiana na maendeleo ya shule hiyo alikiri kwepo kwa hali mbaya na ya hatari kwa wanafunzi na walimu.
Majengo ya shule hiyo yamechakaa kuliko hata shule zingine ambazo amewahi kufundishia, shule hiyo ina wanafunzi 566, vyumba vya madarasa sita na unakuta chumba kimoja kunakuwa na wanafunzi 102 badala ya 45.
“Tangu nimehamia hapa mwaka 2011 majengo haya niliyakuta hivi, vyoo vimebomoka na yamebaki matundu sita. Kila tundu hujisaidia wanafunzi 25 hivyo kwa sasa tunahitaji matundu 19” anasema Zakaria.
Shule hiyo ina walimu 10 tu badala ya 13 na ina nyumba 2 za walimu na madawati 65 badala ya 196. Taarifa hizo ameshapeleka katika uongozi wa kijij, bado hakuna mabadiliko yoyote.
Mkuu wa mkoa wa Mara, John Gabriel Tupa alipouzwa kuhusiana na hali ya Marasibora hakusema kitu.
Serikali inavyohangaika kuziba aibu baada ya viongozi kufariki
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment