Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Thursday, July 11, 2013

Obama ateua msaidizi wake balozi Tanzania

Rais wa Marekani, Barack Obama (kushoto) akizungumza na washauri wake waandamizi akiwemo Mark Childress (kulia) ambaye amemteua kuwa balozi mpya wa nchi hiyo hapa nchini. Picha na Ikulu ya Marekani Washington. Rais wa Marekani Barrack Obama amemteua msaidizi wake wa karibu, Mark Childress kuwa balozi wa nchi hiyo, hapa nchini.
Childress ni msaidizi wa Obama katika Ikulu ya Marekani (White House) akiwa Naibu Mkuu wa Utumishi anayeshughulikia mipango katika Serikali ya nchi hiyo na aliwahi kufanya kazi katika Bunge la Seneti.
Obama amefanya uteuzi huo ikiwa ni wiki moja tangu alipohitimisha ziara yake katika nchi tatu za Bara la Afrika, Tanzania ikiwa mojawapo. Pia alizitembelea Senegal na Afrika Kusini.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani jana ilisema nafasi hiyo inahitaji kuidhinishwa na Bunge la Seneti la nchi hiyo. Uteuzi wake unaweza kuwa na maana kubwa katika kutekeleza sera za nje za Marekani.
Katika miaka ya karibuni, Tanzania imeshuhudia ziara za viongozi wakuu wa nchi hiyo nchini ambao ni Bill Clinton, George Bush na Obama.
Kuteuliwa kwa Childress, kunaashiria kwamba Balozi wa sasa wa Marekani nchini Alfonso Lenhardt anakaribia kumaliza muda wake.
Awali, Childress ambaye aliwahi kuwa msaidizi na msiri wa muda mrefu wa Seneta wa zamani, Tom Daschle, alitarajiwa kushika moja ya nyadhifa mbili katika utawala wa Rais Obama ambazo ni Mkuu wa Utumishi katika Idara ya Huduma ya Afya ya Jamii (HHS) au Naibu Mkurugenzi katika Ofisi ya Maboresho ya Afya katika Ikulu ya Marekani.
Hata hivyo, jina lake liliondolewa katika mapendekezo ya uteuzi wa kuongoza ofisi hizo baada ya kuhusishwa katika masuala ya kodi Februari 2009, hivyo kubaki pasipo na jukumu maalumu.
Pamoja na mkanganyiko uliojitokeza awali kuhusu majukumu yake, Childress alimudu kufanya kazi kubwa katika kuwezesha kupitishwa kisha kutekelezwa kwa mabadiliko makubwa katika sekta ya afya ya nchi hiyo. Aliteuliwa kuwa Naibu Mkuu wa Utumishi wa Marekani, 2012.
Mwaka 2009, mpigania mabadiliko na maboresho ya sekta ya afya Marekani ambaye sasa ni Seneta, Edward M. Kennedy alimwomba Childress kujiunga na timu yake ya ushauri wa masuala ya afya, elimu, wafanyakazi na pensheni.
Timu hiyo pia ilikuwa na kazi ya kumshauri kuhusu masuala ya mabadiliko ya afya na Childress alikuwa miongoni mwa watu walioshiriki kutoa rasimu ya kwanza ya muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Afya 2009.
Baada ya muswada huo kupitishwa Februari 2010, Childress aliondoka katika kamati hiyo na kujiunga na Idara ya Huduma ya Afya ya Jamii Marekani ambako alikuwa na wajibu wa kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo mpya akiwa Kaimu Msimamizi Mkuu wa idara hiyo.
Childress ni mwanasheria aliyebobea katika masuala ya kanuni za uhakika wa chakula na dawa akifanya kazi hiyo jijini Washington.
Katika miaka yake ya utumishi katika Seneti ya Marekani (Capitol Hill) akiwa na Maseneta; Daschle na Kennedy, mara nyingi aliteuliwa kuongoza midahalo ya usuluhishi wa migogoro ya masuala nyeti ndani ya Seneti na kuratibu majadiliano muhimu kama vile uteuzi wa watendaji wa Mahakama.
Mark Childress pia anatajwa kuwa mmoja wa watu wa karibu sana na Obama, huku akielezwa kuwa mmoja wa watu wenye nguvu kubwa ya ushawishi katika uongozi wa sasa wa Rais wa Marekani.
Tangu alipojiunga na timu ya Obama baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2008, Childress amekuwa na nafasi muhimu na amekuwa akitumika katika kuweka sawa mambo magumu yanayojitokeza White House.
Anatajwa pia kuwa mmoja wa watu ambao wamekuwa wakitumika kusahihisha makosa mengi yanayofanywa na utawala wa Obama hasa katika Ikulu ya Marekani.
Childress (53) akitokea Carolina ya Kaskazini, pia ameongoza katika kukabili tuhuma dhidi ya Taasisi za Ukusanyaji Kodi Marekani ambazo zilikuwa zikiwagusa wahafidhina.
Anatajwa kwamba siyo mtu wa kupenda kujulikana na katika mtandao wa Wikipedia, maelezo kuhusu maisha yake na kazi alizofanya ni mistari miwili tu.
Gazeti la Washington Post linampigia debe Childress kwamba ana sifa nyingi zinazoeleza mafanikio katika kazi zake alizowahi kufanya na kwamba ‘anafaa kwa wadhifa aliopewa wa kuwa Balozi nchini Tanzania’.
Naibu Meya wa Los Angeles, Jay Carson ambaye aliwahi kuwa msemaji wa Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton alinukuliwa akimwita Childress kuwa ni ‘mtu mwenye akili nyingi’, ambaye ana uwezo wa kutanzua mizozo mipya yenye kukanganya.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment