Writen by
sadataley
3:27 PM
-
0
Comments
Kashfa za kuchupa mipaka za kimaadili zilizofanywa na Vatican na Kanisa Katoliki katika miaka ya hivi karibuni zimegeuka kuwa mada na ajenda kuu zinazojadiliwa na kuripotiwa na vyombo vya habari hivi sasa.
Hatua ya Kanisa Katoliki ya kuwapiga marufuku mapadri kuoa imelitumbukiza kanisa hilo katika uasherati na ufisadi wa kila aina wa kimaadili. Miongoni mwa kashfa maarufu zaidi zilizolikumba Kanisa Katoliki hivi sasa ni vitendo vya ulawiti hasa dhidi ya watoto wadogo vinavyofanywa na makasisi na mapadri wa kanisa hilo. Katika miaka ya hivi karibuni, Kanisa Katoliki limekumbwa na kashfa kubwa za mfululizo za kuwanajisi na kuwalawiti watoto wadogo.
Kesi za ulawiti na udhalilishaji wa kijinsia zinazowahusu mapadri wa Kanisa Katoliki zimelisababishia hasara kubwa kanisa hilo hadi hivi sasa hasa nchini Marekani. Suala hilo limekuwa zito kiasi kwamba Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani amesema katika siku ya pili ya ziara yake huko Ireland kwamba kuna wajibu wa kutendeka uadilifu dhidi ya makasisi waliowafanyia unyama watoto wadogo kama ambavyo pia ameomba radhi rasmi kutokana na unyama huo uliofanywa na viongozi wakuu wa kanisa lake.
Katika moja ya hotuba zake, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amesema: Hakuna yeyote anayeweza kunyamazia kimya matukio ya watu waliodhalilishwa, waliotekwa nyara bila hatia na kubakiwa na kovu na kumbukumbu chungu sana.
Hivi karibuni pia Papa Francis alilalamikia vikali kashfa za kimaadili zilizowakumba makasisi wa kanisa lake kiasi kwamba aliwaandikia barua wafuasi milioni mia mbili wa Kanisa Katoliki kulaani vikali kudhalilishwa watoto wadogo kunakofanywa na makasisi wa kanisa hilo kama ambavyo alilaani pia jinsi viongozi wa Kanisa Katoliki walivyokuwa wanaficha kashfa hizo. Vatican inasema kuwa, hii ni mara ya kwanza kwa Papa yaani kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani kuzungumza moja kwa moja na wafuasi wote wa kanisa hilo kuhusu suala la udhalilishaji wa kijinsia unaofanywa na mapadri na viongozi wa ngazi za juu wa kanisa.
Hata mwanzoni kabisa kwa kuchukua uongozi wa kanisa hilo, Papa Francis alikiri kuweko ufisadi mkubwa na lobi ya mabaradhuli na makundi ya wafuasi wa ngono za watu wa jinsia moja huko Vatican na pia alikiri kuwa hana uwezo wa kupambana na uchafu huo. Hata hivyo mashinikizo ya walio wengi yamemlazimisha kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki kuchukua hatua za kupoza hali ya mambo. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Papa Francis ni ile ya mwezi Juni 2016 alipotoa hukumu iliyosema kuwa inatosha kabisa mtu kuvuliwa vazi la kanisa iwapo tu atazembea au kupuuza kufuatilia kesi na kitendo chochote kinachofanywa na viongozi wa Kanisa Katoliki cha kuwadhalilisha kijinsia watoto wadogo.
Ukweli wa mambo ni kuwa, kwa makumi ya miaka sasa, Vatican imekumbwa na migogoro mikubwa ya matumizi mabaya ya fedha na maadili maovu hasa ya kudhalilishwa kijinsia na kunajisiwa watoto wadogo walioko masomoni katika makanisa ya madhehebu hayo ya Kikristo katika nchi mbalimbali za Ulaya na Marekani.
Hata Papa Francis mwenyewe amelikiri jambo hilo kwa kusema: Pamoja na kwamba ndani ya Vatican kuna watu wazuri na wasio na doa, lakini pia kuna mrengo wa ufisadi na lobi ya wafuasi wa ngono za jinsia moja hivyo yeye hawezi kufanya mabadiliko yoyote ya uongozi katika suala hilo, ndio maana ameamua kulifikisha suala hilo kwa jopo la maaskofu waaminifu.
Hatua ya kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani ya kukiri hadharani kwamba kuna mabaradhuli na wafuasi wa ngono za jinsia moja wenye nguvu ndani ya Vatican na kitendo chake cha kuomba radhi kutokana na unyama wa kunajisiwa na kulawitiwa watoto wadogo kunakofanywa na makasisi na mapadri wa Kikatoliki, ni mambo ambayo yanaonesha kina kikubwa cha uchafu wa kimaadili uliogubika moja ya vituo muhimu sana katika ulimwengu wa Kikristo na makanisa ya Kikatoliki katika nchi nyingine duniani. Vile vile tahadhari iliyotolewa na Papa Francis ya kwamba kuna hatari ya kusambaratika kabisa Kanisa Katoliki kama hakutafanyika mabadiliko ya kimsingi ndani ya kanisa hilo, kunaonesha ukubwa wa kuporomoka kimaadili kanisa hilo maarufu duniani na kuzidi kuwa kwake mbali na mafundisho sahihi ya Masihi Isa (Yesu) AS.
No comments
Post a Comment