MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeuagiza upande wa Jamhuri kutoa taarifa ya kukamilisha upelelezi wa kesi inayomkabili Kamishna Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake baada ya siku 14.
Kitilya na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya kujipatia na kutakatisha Dola za Marekani milioni sita (Sh. bilioni 1.3).
Kesi hiyo ilitajwa jana katika mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Cyprian Mkeha.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Christopher Msigwa, alidai kuwa tayari upande wa Jamhuri umepokea awamu ya kwanza ya nyaraka za kesi hiyo kutoka nchini Uingereza.
"Mheshimiwa kesi hii imepangwa kutajwa leo, lakini hadi sasa upande wa Jamhuri umepokea awamu ya kwanza ya nyaraka kutoka nchini Uingereza na kwamba unasubiri awamu ya mwisho ya kupokea vielelezo hivyo kutoka nchini humo wakati wowote" alidai Msigwa.
Wakili wa utetezi, Mwanahamisi Adam, alidai kuwa upande wa Jamhuri unatakiwa kueleza kwa uhakika kwamba nyaraka hizo zitawasili lini ili kesi ianze kusikilizwa na washtakiwa wapate haki yao ya msingi kisheria.
Hakimu Mkeha alisema mahakama yake inatoa siku 14 hadi Juni 30, mwaka huu, upande wa Jamhuri upeleke majibu kuwa kuwasili nyaraka hizo utachukua siku ngapi.
Alisema kesi hiyo itatajwa Juni 30, mwaka huu na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.
Mbali na Kitilya, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao wanasota rumande ni, aliyekuwa Meneja Mwandamizi wa Stanbic, Shose Sinare na mwanasheria wa benki hiyo, Sioi Solomon.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili mosi, mwaka huu, wakikabiliwa na mashitaka manane likiwemo la kutakatisha fedha Dola za Marekani milioni sita (Sh. bilioni 1.3) mali ya serikali.
No comments
Post a Comment