POLISI jana walitumia mabovu ya machozi kutawanya watu wenye ulemavu waliokuwa wamekusanyika na kufunga barabara ya Sokoine jijini Dar es Salaam.
Mabomu hayo yalizua taharuki kwa watumiaji wa njia hiyo na kusababisha usumbufu kwao uliodumu takriban dakika kumi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni, aliliambia Nipashe jana kuwa polisi walilazimika kutumia mabomu kama njia ya kuwakamata watu hao.
Kamanda Hamduni alisema kutokana na kitendo hicho, polisi wanawashikilia watu 40 akiwamo mwanamke mmoja.
Alisema lengo la mkusanyiko huo ulikuwa kwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya kukamatwa na askari polisi wa usalama barabarani.
“Ni kweli tunawashikilia watu 40 akiwamo mwanamke mmoja kwa kosa la kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria.
“Watu hawa walikuwa wanakwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kupeleka malalamiko yao kuhusu kitendo cha kukamatwa na askari wa usalama barabarani,” alisema.
Kamanda Hamduni alisema baada ya polisi kufika eneo hilo na kutoa amri mara tatu ya kuwataka kutawanyika, walemavu walikaidi ndiyo maana waliamua kutumia mabomu ya machozi.
Alisema nguvu hiyo ya kutumia mabomu ilikuwa na lengo la kurahisisha ukamataji wa watu hao waliokaidi amri ya polisi kutawanyika.
No comments
Post a Comment