Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Wednesday, December 21, 2016

Mwinyi apongeza makanisa kwa huduma bora za kijamii nchini


Rais Mstaafu Alhaji Ali Hassan Mwinyi amepongeza makanisa kwa kutoa huduma bora za kijamii nchini na kuwatia moyo watendaji ili kazi hiyo iendelee kwa lengo la kuleta ustawi wa jamii ya Watanzania.
Rais Mwinyi alisema hayo Kata ya Maji ya Chai, Wilayani Arumeru 24 Nov 2016 katika sherehe za miaka 25 ya Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC) ambacho ni chombo cha pamoja cha makanisa ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu (TEC).

Aliwapongeza waasisi wa chombo hicho kwa maono ya kuundwa kwa chombo hicho ambacho kimsingi kinaleta pamoja kwa kuratibu na kusimamia ubora wa huduma za elimu na afya kwa ubia na Serikali.
Mzee Mwinyi ambaye alikuwa amefuatana na mkwewe Mama Sitti Mwinyi, kuhusu afya, akinukuu Biblia Luka 10: 34 na kusema anatambua kuwa wakristo wanaitikia wito wa Yesu wa kuwahudumia wana jamii na kuhusu elimu alinukuu Mithali 4: 13.
Alhaji Mwinyi alisema Korani haikatazi waislamu na wakristo kushirikiana wala kupokea huduma za kijamii zinazotolewa na wakristo. Alisema alipokuwa Rais, aliidhinisha mkataba baada ya kugundua kwamba malengo ya viongozi wa Serikali na yale ya viongozi wa Kikristo katika kuihudumia jamii yanafanana.
Katika sherehe hiyo pamoja na mambo mengine Rais Mwinyi alifungua rasmi jengo jipya la CSSC Kanda ya Kaskazini baada ya jengo hilo kuwekwa wakfu na Rais wa CSSC, Askofu Dkt. Alex Malasusa ambaye pia ni Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani.
Akimkaribisha mgeni rasmi kuhutubia umati uliokuwepo, Askofu Dkt. Malasusa, alishukuru Serikali kwa ushirikiano na kwa ubia uliopo kwa kutoa raslimali fedha na watumishi kwa ajili ya kusaidia kuendesha hospitali za Kanisa.
Askofu Dkt Malasusa alisema makanisa yataendeleza huduma za kijamii nchini kwani ni sehemu ya Ibada kwani wakristo wanatekeleza wito wao wa kumhudumia mwanadamu kwa ukamilifu: kiroho, kimwili na kiakili.
Maaskofu kutoka KKKT, Kanisa Katoliki, Kanisa la Anglikana, Kanisa la Mungu, na Kanisa la Menonnite toka Ukanda wa Kaskazini yaani Mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro walishuhudia Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt. Fredrick Shoo, akiweka saini hati ya kuhamisha Kampuni ya Misioni ya Kusambaza Madawa na Vifaa Tiba (MEMS) iliyokuwa chini ya KKKT kwenda CSSC. Viongozi wa Idara na watendaji makanisa hayo na kutoka CCT na CSSS pia walihudhuria kwa wingi katika tukio hilo.
Kwa niaba ya waanzilishi wa CSSC, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Arusha Mhashamu Josephat L. Lebulu alisema wazo la kuwa na CSSC lilikuwa tangu miaka mingi ambapo makanisa ya Tanganyika yaliunda Tanganyika Christian Medical Board (TCMB) na baadaye Christian Education Board of Tanganyika (CEBT) kwa kushirikiana na makanisa ya Ujeumani.
Waasisi wa CSSC ambao ni pamoja na Askofu Lebulu na Askofu Mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Erasto Kweka, walianza mchakato kwa kuwasiliana na Rais Mwinyi alipokuwa kiongozi wa Awamu ya Pili; ndipo hatimaye mwaka 1992 chombo hicho kikaanza kwa kuunganisha kazi zilizofanywa na bodi zile mbili TCMB na CEBT.
Askofu Lebulu alisema “tuliona tuunganishe nguvu kwa kuanzisha chombo kitakachopanga kwa pamoja, kupanua na kuboresha utoaji huduma za afya na elimu kwa kuwa katika matatizo kama ugonjwa, hakuna malaria ya kikatoliki, ya kilutheri au ya kiislamu,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa CSSS, Bw. Peter Maduki, alisema CSSC ina kanda tano nchini yaani Kanda ya Kaskazini; Kanda ya Ziwa; Kanda ya Magharibi; Kanda ya Mashariki na Kanda ya Kusini.
Alisema kwa pamoja katika sekta ya elimu makanisa yanamiliki taasisi za elimu 691 na kati ya hizo kuna vyuo vikuu tisa; vyuo vikuu vishiriki 19; vyuo vya ufundi stadi 126; vyuo vya ualimu 14; shule za sekondari 362 na shule za msingi 161.
Pia makanisa nchini yanamiliki hospitali 102 ambapo kati ya hizo mbili ni hospitali za kanda, hospitali teule za Wilaya 38; hospitali 62 zinatoa huduma katika hospitali mbalimbali; vituo vya afya 102; zahanati 3,987; Vyuo vya mafunzo ya watumishi wa afya ngazi ya elimu ya juu na ya kati; chuo kikuu kimoja na vyuo vikuu vishiriki vitatu vya tiba.
Kwa niaba ya wawakilishi kutoka kanda mbalimbali, Askofu Dkt. Benson Bagonza, kutoka KKKT Dayosisi ya Karagwe ambaye ni Mwenyekiti wa Kanda ya Ziwa CSSC, alipongeza juhudi za Kanda ya Kaskazini zilizowezesha kukamilisha ujenzi wa jengo la kanda hiyo. Alisema jengo hilo lililojengwa kwa ushirikiano wa makanisa yote ni alama muhimu ya umoja na ukamilifu wa wito wetu wa kumtumikia mwanadamu.
Alimshukuru Rais Mstaafu kwa kupokea maono ya kuwa na chombo kama CSSC na kukubali kianzishwe chini ya uongozi wake.
Askofu Rogath Kimaryo wa Jimbo Katoliki la Same, Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini CSSC, alitoa wito vituo va kanisa na hospitali za kanisa viwe mahali pa kuhudumia watu kwa huruma, upendo na kuwapa wagonjwa matumaini ili waweze kupona.
Askofu Kimaryo aliomba Serikali iweze kuendelea kutoa ushirikiano kwa makanisa kupita CSSC kwa kuheshimu makubaliano yake na makanisa ili kuwa suluhu ya changamoto katika sekta ya afya na elimu nchini.
Pia aliwakaribisha na kumshukuru Rais Mstaafu na wote waliohudhuria kwani mahudhurio yao ndio yaliyofanikisha sherehe ya jubilii ya miaka 25 ya CSSC. 
 
   Rais Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi alikata utepe kufungua jengo jipya la Ofisi ya CSSC Kanda ya Kaskazini huku Askofu Dkt. Malasusa akipiga makofi. Kulia ni Mkuu wa KKKT, Askofu Fredrick Shoo na kulia kwa Rais Mwinyi ni mkwewe Mama Sitti Mwinyi.
   Picha kulia ni Askofu Dkt. Alex G. Malasusa, Rais wa CSSC (aliye nyuma ya msalaba) na Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt. Fredrik Shoo wakitia saini hati ya makabidhiano ya kampuni ya madawa na vifaa tiba toka KKKT kwenda CSSC. Wanaoshuhudia ni Mkurugenzi Mtendaji wa CSSC, Bw. Peter Maduki (kulia) akifuatiwa na Katibu Mkuu wa KKKT, Bw. Brighton Killewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi MEMS, Bw. Pius Maneno.



Bishops from various denominations attended the CSSC 25th anniversary celebrations at Maji ya Chai Ward, Arumeru District.
Chanzo: ELCT website
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment