Writen by
sadataley
10:24 AM
-
0
Comments
Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Palamagamba
Kabudi (kulia) akizungumza kwenye mdahalo wa Katiba, uliofanyika Dar es
Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar/ Mikoani. Mdahalo wa Katiba ulioandaliwa na
Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kurushwa juzi na ITV umeelezwa kuwa
uliotoa mafunzo makubwa kwa watu wengi katika maeneo mbalimbali nchini
kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.
Wakati waliohudhuria mdahalo huo Dar es Salaam
walikuwa kila mara wanawakatisha watoa mada kwa makofi na vibwagizo vya
“CCM, CCM, CCM” na “Babu, Babu, Babu”, katika mikoa mbalimbali watu
walikusanyika katika maeneo mbalimbali ya vijiweni, baa, madukani
kusikiliza huku wengine wakibeba redio na simu za mkononi
Mjini Dodoma, wananchi katika maeneo ya Mitaa ya
Nyerere Square, Soko la Dk Rehema Nchimbi na viwanja vya Bunge,
walishindwa kuvumilia na kujikuta wapiga kelele za juu katika mada
iliyokuwa ikitolewa Profesa Palamagamba Kabudi kuhusu umuhimu wa kupata
Katiba Mpya.
Moshi
Makundi ya wafanyabiashara, wafanyakazi na
wananchi wa kawaida walionekana wakifuatilia mdahalo huo uliomhusisha
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba na wajumbe wengine.
Wakati mjadala huo ulipoanza tu, watu mbalimbali
walionekana kupigiana simu na wengine kutumiana meseji wakihimizana
kuufuatilia.
Mmoja wa waliofuatilia, Christopher Shayo
‘Kimeta’, alisema baada ya kumalizika kwa mdahalo huo ameweza kujua
pumba ni zipi na mchele ni upi.
“Sijui kama hawa viongozi wa CCM na wajumbe wao wa
Bunge la Katiba waliuangalia, lakini kwa kweli wameumbuka mchana
kweupe. Upotoshaji wao ulifikia tamati jana,” alisema Shayo.
Mfanyabiashara, Festo Minja alisema ufafanuzi
uliotolewa na wajumbe wa Tume unapaswa kuwa dira ya majadiliano kwa
wajumbe wa Bunge la Katiba lililoanza jana bila maridhiano.
Bukoba
Mchuuzi, Derick Edmund anayeuza bidhaa karibu na
Hospitali ya Mkoa wa Kagera alisema amefahamu mambo mengi baada ya
kufuatilia mjadala huo.
Alisema hoja zilizotolewa na Jaji Warioba kutetea
Rasimu ya Katiba ndizo zilizomvutia zaidi na kusema kwa mvutano uliopo
sasa itakuwa vigumu kupata Katiba Mpya hivi karibuni.
Mkazi wa Bukoba, Fadhili Hamis alisema kilichomshangaza wakati
wa akifuatilia mjadala huo ni jinsi wajumbe wa Tume walivyotetea msimamo
wao bila kutofautiana.
Alisema pamoja na kuwa hapendelei muundo wa
serikali tatu, hoja zilizotolewa na wajumbe hao wakati wa mjadala
zilionekana kuwa nzito na alivutiwa zaidi na mjumbe wa Tume hiyo kutoka
Zanzibar, Awadh Ali Said.
Kigoma
Mkazi wa Masanga, Kigoma mjini, Alphonce Mbasa
alisema kwa ufafanuzi uliotolewa juzi, wabunge wakipitisha maoni ya
vyama vyao kwa kisingizio cha wingi ndani ya Bunge la Katiba
hayatasaidia kwa vile wananchi wanajua nafasi yao.
Mkazi wa Kijiji cha Kalinzi, Kamsige Kamsige
alisema wajumbe wa Tume wameonyesha uzalendo na hawakuwa tayari
kuyasaliti maoni ya wananchi waliyoyatoa katika kuandaa rasimu zote
mbili za Katiba.
Mwanza
Ofisa Taaluma Mwandamizi wa Chuo cha Usimamizi wa
Fedha (IFM), Tawi la Mwanza, Charles Kadikilo alisema pamoja na hoja
nyingi zinazojadiliwa katika midahalo mbalimbali ukiwamo wa juzi, bado
haoni ufumbuzi wa kupata Katiba mpya, bali kinachofanyika ni kila mtu
kutetea upande wake.
Alisema inawezekana kila mmoja akawa yuko sahihi
kwa upande wake ila kinachotakiwa ni kukaa sehemu moja katika meza ya
maridhiano na kuacha tofauti zao za masilahi binafsi na vyama vyao.
Arusha
Kada wa CCM, Lembrise Sirikwa alisema mdahalo wa
juzi umemsaidia kujua mambo mengi ambayo yalikuwa yamejificha...
“Nimefuatilia kwa makini mjadala, kweli kuna mengi nimejifunza na kama
kweli tunataka katiba bora ni muhimu kuzingatia kujadili Rasimu iliyopo
bungeni na si vinginevyo.”
Fundi wa magari, eneo la Sakina, Godi Kweka
alisema kati ya midahalo yote ya Katiba iliyofanyika, amevutiwa na
mdahalo wa juzi, kwani ulikuwa ni wa kutoa elimu na kuweka kando
ubabaishaji ambao umetawala majadiliano juu ya Bunge la Katiba.
“Nilimpenda sana yule Profesa Kabudi, ametupa
historia na elimu juu ya Katiba, kweli alichokisema ni muhimu kukifuata
kwani Katiba ni ya wananchi na si ya viongozi,” alisema Kweka.
Mkazi mwingine, Julius Nkya alisema mdahalo wa juzi umechelewa
kwani ulitakiwa kufanyika mapema kwa kuwa ndiyo umetoa dira ya ambacho
kinapaswa kufanyika na ni busara yaliyojadiliwa juzi kufuatwa na wajumbe
wa Bunge la Katiba na Serikali.
Iringa
Mfanyabiashara wa Miyomboni, Iringa, Peter Kibona
alisema wajumbe wa Tume walitumia fursa hiyo kutoa majibu ya maswali
mengi ya msingi kuhusu Katiba Mpya ambayo wanasiasa wanaopingana bungeni
hawana majibu yake.
“Sasa tumeelewa kuwa hata kitendo cha kuivunja
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya kukamilika kwa mchakato wenyewe
kilifanywa kimakosa,” alisema Kibona na kuongeza:
Kwa msingi huo, Katiba haiwezi kupatikana. Wito
wangu kwa viongozi, watumie busara au la Bunge la Katiba lisimamishwe
yapatikane maridhiano.
Mfanyabiashara wa kanda za muziki karibu na Kituo
Kikuu cha Mabasi cha Iringa, Lema Raymond alisema alilazimika kuongeza
sauti wakati wa mdahalo huo ili kuwezesha wananchi kupata ufahamu juu ya
mchakato wa Katiba mpya.
Imeandikwa na Geofrey Nyang’oro, Mussa
Juma, Ngollo John, Jesse Mikofu, Anthony Kayanda, Phinias Bashaya, Habel
Chidawali na Daniel Mjema.
No comments
Post a Comment