Writen by
sadataley
5:14 PM
-
0
Comments
Na Neville Meena, MwananchiDodoma. Kadiri siku zinavyosogea kitendawili kuhusu hatima ya Bunge Maalumu kimeendelea kuwa kigumu na sasa kinachosubiriwa ni matokeo ya mkutano baina ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa ambavyo ni wanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Awali kikao hicho baina ya Rais Kikwete na
viongozi hao kilipangwa kufanyika jana mchana, lakini kiliahirishwa hadi
leo saa tano asubuhi kutokana na Rais kukabiliwa na majukumu mengine
yanayohusiana na ziara yake inayoendelea mkoani Dodoma.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zinasema
taarifa ya kuahirishwa kwa kikao hicho ilitolewa juzi usiku kwa wahusika
ambao wote ni viongozi wa vyama vya siasa, na kwamba wale walioko Dar
es Salaam watasafiri leo kwa ndege maalumu hadi Dodoma ambako
watashiriki mkutano huo.
“Mkutano umeahirishwa hadi kesho (leo) saa tano
asubuhi na utafanyika hapahapa Dodoma. Ratiba ya Mheshimiwa Rais kwa leo
(jana) haikuruhusu kwa hiyo wahusika waliarifiwa tangu jana (juzi)
usiku,” kilisema chanzo chetu.
Rais Kikwete anaendelea na ziara yake mkoani
Dodoma na jana ilikuwa siku yake ya tatu alipotembelea Wilaya ya
Chamwino. Leo baada ya kukutana na viongozi wa vyama vya siasa, Rais
Kikwete atalihutubia taifa pale atakapokuzunguza na wazee wa Mkoa wa
Dodoma katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango.
Matokeo ya mkutano wa Rais Kikwete na viongozi wa
vyama vya siasa yanasubiriwa kwa shauku kubwa kwani huenda yakatoa
mwelekeo wa nini kinafuata baada ya kuwapo kwa mkwamo wa mchakato wa
Katiba, ambao hivi sasa umefikia katika hatua ya Bunge Maalumu.
Licha ya kwamba Kamati za Bunge hilo zimemaliza
kazi yake, lakini kuna wasiwasi kwamba kile kilichojadiliwa kitakosa
uhalali wa kisiasa kutokana na kutoshirikisha wajumbe ambao ni wanachama
wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Ukawa walisusia Bunge hilo Aprili 16 mwaka huu kwa
madai ya kwamba hawaridhishwi na mambo yanavyokwenda na wameapa kwamba
kamwe hawatarejea bungeni kutokana na sababu ambazo hivi sasa
zimebadilika tofauti na zile walizokuwa wakizitoa awali.
Awali viongozi hao walikuwa wakidai kwamba
walisusia Bunge Maalumu kutokana na CCM kutumia wingi wao kubadili
maudhui ya rasimu iliyotungwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, lakini
sasa wanasema pamoja na hilo kuendelea na mchakato ni kufuja fedha za
umma kwani hakuna uharaka wa kupatikana kwa Katiba mpya.
Badala yake Ukawa kupitia kwa viongozi wao ambao
ni wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR Mageuzi, wamesikika mara kadhaa
wakidai kwamba hivi sasa taifa linapaswa kujielekeza katika mambo muhimu
yakiwamo uandikishaji mpya wa daftari la kudumu la wapigakura,
maandalizi ya bajeti ya mwisho ya uongozi wa awamu ya nne na maandalizi
ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2015.
Kikao cha leo
Kwa kuzingatia mazingira hayo, kikao cha leo
kinaweza kisijikite katika kuwashawishi Ukawa kurejea bungeni, bali
kuangalia jinsi ya kusitisha Bunge hilo bila kuleta madhara makubwa ya
kisiasa kwa pande zote zinazohusika katika mgogoro unaoendelea.
Kumekuwa na mawazo kwamba kwa mujibu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba Rais hana uwezo wa kusitisha Bunge, lakini baadhi
ya watumishi wa umma wanasema kiongozi wa nchi anaweza kutumia mamlaka
yake (prerogative powers) alizopewa na Katiba kusitisha kuendelea kwa
taasisi hiyo.
“Pengine kuvunja ni tatizo lakini kwa nafasi yake
kama Mkuu wa Nchi, Rais anaweza kusitisha Bunge Maalumu maana ni kama
anavyoweza kuteua mawaziri, hakuna mahali amepewa ruhusa ya kuwaondoa,
lakini huwa akishateua mwingine maana yake yule aliyepo ameondoka,”
alisema mtaalamu mmoja wa masuala ya utumishi serikalini na kuongeza:
“Kwa hiyo hilo Bunge yeye mwenyewe ndiye aliyetoa
GN ya kulianzisha na wanasema siku alizotoa ni chache kwa hiyo wanataka
huyohuyo atoe GN nyingine kuongeza kwa maana ya kufuta ile ya kwanza.
Kwa hiyo anaweza kutoa GN ya kusitisha tu na siyo kosa kisheria”.
Wapinzani kwa upande wao wamekuwa wakijenga hoja
kwamba hata kama Katiba itapitishwa hakuna fursa ya kupigiwa kura ya
maoni kama sheria inavyoelekeza kutokana na muda kutoruhusu.
Mmoja wa viongozi wa Ukawa, Freeman Mbowe aliwahi
kuliambia gazeti hili kwamba uandikishaji wa wapigakura katika daftari
la kudumu ni kazi inayohitaji muda usiopungua miezi sita, ikizingatiwa
kwamba tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeshaweka bayana kwamba
daftari la sasa halifai.
NEC ilipokutana na vyama vya saisa ilitangaza
kwamba uandikishaji mpya wa wapigakura ungeanza kesho, Septemba 1, 2014
lakini hadi jana hakukuwa na dalili zozote za kuanza kwa kazi hiyo.
Changamoto ya muda
Habari kutoka ndani ya Serikali zinasema muda ni
moja ya mambo yanayoifanya Serikali kuona umuhimu wa kusitisha Bunge
kwani mbali na mambo makubwa ya kitaifa yaliyotajwa, vikao vya Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi vinapaswa
kuanza katika muda ambao vinaweza kuingiliana na Bunge Maalumu.
Wakati Bunge la Muungano likitarajiwa kukutana kuanzia Novemba
4, 2014, Katibu wa Bunge Maalumu ambaye pia ni Katibu wa Baraza la
Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad alisema jana kwamba vikao vyake
vilipangwa kuanza katikati ya Oktoba.
Kwa kawaida vikao vya Bunge hutanguliwa na wiki
mbili za vikao vya kamati za kudumu na ikiwa ratiba itabaki kama ilivyo
basi vitaingiliana na vikao vya Bunge Maalumu ambalo ratiba yake
imepangwa kuendelea hadi Oktoba 31.
Awali Bunge Maalumu lilipaswa kukutana kwa siku 60
katika awamu yake ya pili kama zilivyoongezwa na Rais Kikwete Julai 28
mwaka huu na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali (GN) namba 254 ya
Agosti 1, 2014.
Katika gazeti hilo, Bunge Maalumu lilipaswa kuanza
Agosti 5, 2014 na kumalizika Oktoba 4, lakini ratiba rasmi ya Bunge
hilo inaonyesha kuwa litamalizika Oktoba 31, baada ya kuhesabiwa kwa
siku za kazi tu badala ya siku za kalenda.
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta Jumatatu
hadi Ijumaa ndizo kisheria ambazo wajumbe wanapaswa kufanya kazi na
kwamba Jumamosi na Jumapili siyo sehemu ya siku 60 zilizoongezwa na
Rais.
Kutokana na hali hiyo, kulikuwa na jitihada za
kubadilishwa kwa taarifa ya Rais kwenye Gazeti la Serikali ili
kuzingatia mabadiliko hayo, lakini hadi jana Hamad alisema walikuwa
hawajapokea maelekezo ya ziada tofauti na yale ya awali.
“Bado tunasubiri maelekezo au niseme ufafanuzi
kutoka serikalini maana haya mambo ni ya kisheria kwani hadi sasa ile GN
ya kwanza bado haijabadilika,” alisema Hamad ambaye pia ni Katibu wa
Baraza la Wawakilishi (BLW).
Naibu Spika wa Bunge la Muungano, Job Ndugai
alisema kwa jinsi ratiba ya Bunge Maalumu ilivyopangwa lazima itaingilia
na shughuli za Bunge la Muungano, hivyo lazima uamuzi ufanywe ili
kuepusha adha hiyo.
“Sisi tumeishaliona hilo kwamba ni changamoto,
tulikuwa tukijaribu kujadiliana kuona kama baadhi ya vikao vya kamati
vinaweza kuanza mapema hapa Dodoma, lakini uamuzi bado haujafanyika
mpaka sasa,” alisema Ndugai.
Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge la Muungano, kamati
zake za kisekta zilipaswa kuanza vikao wiki mbili kabla ambayo ni Oktoba
20 mwaka huu, siku ambayo bado Bunge Maalumu kwa mujibu wa ratiba
iliyopo sasa litakuwa bado halijakamilisha kazi yake.
No comments
Post a Comment