Writen by
sadataley
4:19 PM
-
0
Comments
Na Ibrahim Yamola, MwananchiDar es Salaam. Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeshikilia msimamo wake kuwa uko tayari kufanya mazungumzo ya kumaliza mpasuko uliojitokeza katika Bunge Maalumu la Katiba na siyo kurudi bungeni.
Pia umesema kwamba hawatashiriki Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 endapo Katiba Mpya haitapatikana au iliyopo haitafanyiwa marekebisho.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na
Mwenyekiti wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa Kamati Kuu ya Chama hicho.
“Ukawa hatuwezi kukataa mazungumzo ya kutafuta
mwafaka na faida kwa Watanzania lakini tunaweza kukataa kurudi bungeni
endapo kile kilichotufikisha hapa na nini kilisababisha hakijapata
ufumbuzi.
Mbowe alisema Rais Jakaya Kikwete kwa mujibu wa
sheria ndiye mwenye uwezo wa kuufanya mchakato huu ukamalizika salama na
ikapatikana Katiba yenye kujali masilahi ya wananchi wote.
“Tunamtaka Rais (Kikwete) tunakwenda katika
majadiliano aache kuwa kigeugeu na asimame kama kiongozi wa wananchi ili
amalize uongozi wake salama na kuiacha nchi katika amani kama
alivyoikuta,” alisema Mbowe.
Hivi karibuni katika mahojiano maalumu na gazeti
hili, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema Ukawa wako
tayari kurejea bungeni hata usiku wa manane endapo watahakikishiwa kuwa
mjadala wa Bunge hilo utajikita katika rasimu iliyopo mezani.
“Sisi Ukawa tuko tayari kurejea bungeni hata saa
nane za usiku ila wakituhakikishia tunakwenda kujadili Rasimu iliyobeba
maoni ya Watanzania kinyume na hapo hatutakubali kurejea,” alisema Dk
Slaa.
Alisisitiza kwamba “Hata kama tutarejea bungeni, yakitokea yaliyotufanya tutoke, tutachukua uamuzi haraka.”
Alisema CCM haina nia ya kupatikana kwa Katiba
Mpya na imekuwa ikitumia nguvu kutaka kuuharibu ili Katiba hii iliyopo
iendelee kutumika.
“Tuna ushahidi wa sauti ya Kamati Kuu ya CCM
iliyokaa hivi karibuni wakionyesha kutokuwa na dhamira ya kweli ya
kuipatia nchi hii Katiba na muda utakapofika tutauweka wazi ili
Watanzania wauone na wausikie,” alisema Mbowe.
Ukawa unaoundwa na vyama vya siasa vya Chadema,
CUF na NCCR-Mageuzi vilisusa na kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge Aprili
16 mwaka huu kwa madai ya kuwa zipo dalili za kutaka kuichakachua Rasimu
ya Katiba iliyosheheni maoni na mapendekezo ya wananchi.
Kufuatia mpasuko huo na Agosti 5 mwaka huu Bunge hilo
likitarajia kukutana kwa siku 60, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba,
Samuel Sitta ameteua wajumbe 30 wa kamati ya mashauriano inayotarajia
kukutana Julai 24 mwaka huu.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao mwakani, Mbowe alisema,
“Kama Katiba haitapatikana na ikabaki hii hii....Hatuwezi kuingia katika
uchaguzi kwa kutumia katiba ya sasa ambayo inaonyesha kuwapo kwa tume
huru ya uchaguzi kumbe siyo kweli.”
Naye Mjumbe Kamati Kuu ya Chadema na aliyekuwa
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu alisema,
“tukijidanganya nchi hii ikishindwa kupata Katiba Mpya itakuwa ni
upumbavu.”
Alisema: “Kilichowatokea majirani zetu Kenya
kinaweza kikatokea hata hapa kwetu, busara na hekima inatakiwa itawale
ili mchakato huu umalizike salama.”
Profesa Baregu alisema “Rais (Kikwete) inabidi avue koti lake la uanachama wa CCM kama Mwenyekiti ana avae joho la urais.”
No comments
Post a Comment