Writen by
sadataley
4:18 PM
-
0
Comments
Na Mwandishi Wetu, MwananchiDar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kuwa kinaamini kilishinda uchaguzi wa rais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 chini ya mfumo wa vyama vingi.
Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willbrod Slaa, ambaye
pia alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho kwenye uchaguzi huo,
alibainisha hayo hivi karibuni wakati wa mahojiano maalumu na waandishi
wa gazeti hili.
Dk Slaa alisema kuwa ana uhakika kuwa chama chake
kilipata kura nyingi zaidi za urais, tofauti na mgombea wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete aliyetangazwa mshindi.
“…Baada ya uchaguzi wa mwaka 2010, tulikataa
kumtambua Rais Kikwete, ingawa wakati ule hatukujua kwa uhakika kama
tulishinda. Kadiri nilivyozunguka, ndiyo kadiri tulivyoanza kuamini
kwamba tulishinda,” alisema Dk Slaa.
Alisema kuwa takwimu walizonazo zinaiaminisha Chadema kwamba ilishinda Uchaguzi Mkuu wa urais mwaka 2010.
“Sababu, unafika kwenye jimbo wanakusomea kura
ulizopata katika uchaguzi ule wakizilinganisha na alizozipata Kikwete na
Profesa Ibrahim Lipumba… wanasema Dokta hapa ulimshinda… kwa kura
20,000, pale ulimshinda kwa kura 15,000 pale ulimshinda kwa kura…,”
alifafanua na kusisitiza:
“Sasa ndiyo, tuna uhakika kama tulishinda na ndiyo
maana Kikwete hajawahi kwenda kwa wananchi kushukuru kwa kumchagua,
tofauti na tabia yake. Anachofanya sasa ni kwenda kuzindua miradi.”
Hata hivyo, Dk Slaa alisema hawakuweza kuendelea
na madai yoyote kwa sababu kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya nchi,
mshindi wa urais akishatangazwa hairuhusiwi kupinga kwa namna yoyote
hata mahakamani, akieleza kuwa hiyo pia ndiyo sababu ya kuhitaji Katiba
Mpya.
Tume ya uchaguzi na CCM
Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo, Mwenyekiti wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema
anasubiri kwanza kusoma kwenye vyombo vya habari alichokisena Dk Slaa
ndiyo ataweza kuzungumzia suala hilo.
“Kwa kuwa wewe ndiyo umeniambia Dk Slaa amesema hivyo, ngoja nione kwanza halafu tume itatoa maelezo,” alisema Jaji Lubuva.
Alipopigiwa simu Makamu Mwenyekiti wa CCM- Bara,
Philip Mangula ili atoe ufafanuzi kuhusu suala hilo, alimsikiliza
mwandishi wetu, kisha akasema yupo katika kikao na kukata simu.
Kwa habari zaidi ingiahttp://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Tulishinda-urais-2010/-/1597296/2389694/-/8ximoi/-/index.html
Kwa habari zaidi ingiahttp://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Tulishinda-urais-2010/-/1597296/2389694/-/8ximoi/-/index.html
No comments
Post a Comment