Writen by
sadataley
3:08 PM
-
0
Comments
Na Mwandishi Wetu, MwananchiDar es Salaam. Matamanio ya wanasiasa wengi kwa sasa yako kwenye urais, lakini hali ni tofauti kwa mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, ambaye ameweka bayana kuwa nafasi ya juu kisiasa anayotamani ni kuwa katibu mkuu wa CCM.
Mtoto huyo wa Rais Jakaya Kikwete aliamua kuweka
bayana ndoto yake ya sasa katika mahojiano na gazeti hili yaliyofanyika
mjini Dodoma.
Ridhiwani, ambaye ni mwanasheria, alisema anapenda
nafasi ya chama na ndiyo maana hata katika ‘posti’ zake katika ukurasa
wa facebook amekuwa akiandika kikada zaidi.
“Kwangu mimi ngoja niseme ukweli, napenda sana
nafasi ya chama kwa maana napenda sana chama na kuna siku nilikuwa
nafanya mahojiano na Star Tv na niliwahi kuwaambia kwamba mapenzi yangu
ni kuwa katibu mkuu wa chama,” alisema Ridhiwani alipoulizwa kama
anafikiria kuwania urais.
“Yaani naamini nafasi ya katibu mkuu wa chama ni
nafasi kubwa sana. Hizi siasa za urais ni matokeo tu,” aliongeza
Ridhiwani ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
Ridhiwani, ambaye aliingia bungeni mwezi Aprili
baada ya kushinda kwenye uchaguzi mdogo, alisema iwapo wenzake wataona
yeye anafaa hilo ni suala la mbele, lakini tamaa yake ni kushika nafasi
hiyo ya mtendaji mkuu wa chama hicho tawala.
“Ukiwa katibu mkuu wa chama ndiyo nchi ya kwako
hii, kwa sababu leo hii (katibu mkuu wa CCM, (Abdulrahman) Kinana
anaweza kuwaambia wabunge wa CCM tokeni bungeni na wakatoka,” alisema
mwenyekiti huyo wa zamani wa Umoja wa Vijana wa CCM wa Wilaya ya
Bagamoyo.
“Anaweza akatuambia tulale chini na tukalala. Yeye
ndiyo tajiri wetu, lakini kubwa la msingi zaidi ni kwamba mimi napenda
zaidi nafasi za chama. Hizi nafasi za serikalini ni nafasi za baadaye.
Kama ikitokea kusaidia nchi tutasaidia, lakini hisia zangu zipo sana
kwenye chama,” alisema.
Makundi ya kampeni
Alipoulizwa iwapo kuna kundi au mtu aliyemwomba
amsaidie au awe katika kambi yake kusaka nafasi ya urais, Ridhiwani
alijibu, “Nataka nikwambie ukweli kabisa. Hakuna mtu anayeweza kufanya
hivyo, tena akiwapo basi atakuwa na moyo sana. Kwa sababu wanajua mimi
matamanio yangu ni kumwona Rais yKikwete anamaliza uongozi wake vizuri.”
Alisema anaamini iwapo Rais Kikwete atamaliza
vizuri na kuwaachia nchi yao vizuri, yeye (Ridhiwani) ataendelea kupata
heshima katika nchi hii.
“Sasa leo hii nikijiingiza kwenye makundi ya siasa
nitamvuruga mzee na nikifanya hivyo akashindwa kufanya kazi, tena
tutarudi mwanzoni na akiondoka kesho watasema tumewavurugia nchi na
akisemwa yeye nimesemwa mimi.”
Wanaowania urais kujitoa CCM
Ridhiwani pia alizungumzia tishio la watu
kujiondoa ndani ya chama hicho iwapo hawatapitishwa kugombea urais,
akisema hali hiyo ipo, lakini CCM imejiandaa na hakutakuwa na mpasuko
kama inavyodhaniwa.
“Leo hii mtu anaposema mimi nisipochaguliwa
najitoa, nitakigawa chama, nataka nikwambie CCM inajua hata mtu huyo
akiondoka leo hii wanachama kumi nendeni, chama kitaendelea kama
kawaida. Chama kimejiandaa kwa hali zote. Hakutakuwa na mpasuko ila kuna
watu wataondoka kwa hasira zao ambao hao tunawatarajia,” alisema.
Hata hivyo, Ridhiwani alipoulizwa kama anayajua
majina ya watu hao alijibu: “Hapana. Lakini kama kuna watu wanasema
wasipochaguliwa watu wangu au mtu ninayemtaka sisi tutajiondoa CCM,
maana yake asipochaguliwa mtu huyo ataondoka kweli. Kwa hiyo tunasema
acha aondoke lakini chama kinajua kwamba likitokea hili kuna fulani
atakasirika.”
Alisema ndiyo maana hata mwaka 1995 Rais Kikwete
alipokuwa hajachaguliwa wako watu ambao walisema kwamba wataondoka,
lakini kwa kuelewa kinachofanyika ni kitu gani, Kikwete aliamua kuwa
hataondoka na watu wakasema nao hawaondoki.
Ampinga Pius Msekwa
Akitoa maoni yake kuhusu mchakato wa katiba na
kauli ya Pius Msekwa kwamba hakuna haja ya katiba, Ridhiwani alisema:
“Kwenye chama chochote kilicho hai kuna watu ambao hawataki kubadilika.
Hata CCM tunalo tatizo hilo.
“Sasa Msekwa anatakiwa ajue kuwa hapa tulipo leo
hii nchi yetu inapita miaka 50. Katika mfumo tulionao kuna vitu vya
msingi huwezi kuvishughulikia kutokana na Katiba ya sasa. Hivyo ni
lazima tukubaliane kupata Katiba Mpya ambayo inaweza kutupa mwanga
mpya,” alisema na kuongeza: “Lazima ajue kuwa huhitaji ufike kwenye
matatizo ili uanze kujitathmini.”
Kuhusu mvutano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar
juu ya Muungano, alisema, “Mambo haya yanatakiwa kupatiwa majibu na
majibu yake ni lazima watu wasema katika Katiba yao.”
Alisema kama suluhu ya hilo ni kuunda serikali
tatu basi twende kwa serikali tatu au kama suluhu ni kuziunganisha nchi
hizo ili tuwe na serikali moja basi twende kwa serikali moja basi iwe
hivyo.
“Au kama mfumo tulionao unatosha lakini unatakiwa kufanyiwa marekebisho fulani basi twende kwa mfumo huu ambao unapendekezwa.
“Lakini kusema kwamba hatuhitaji Katiba Mpya, hilo
jambo mimi sikubaliani nalo. Sikubaliani na Msekwa katika hilo. Lazima
ajue mahitaji ya leo yanahitaji hilo.”
Kumiliki mali
Ridhiwani amekuwa akihusishwa na umiliki wa
kampuni kubwa, majumba na mali nyingine ambazo watu wanahoji alizipataje
katika umri wake wa miaka 35 akiwa amehitimu masomo si zaidi ya miaka
mitano iliyopita.
Miongoni mwa mali ambazo inadaiwa ana hisa ni Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), kampuni ya mafuta, hoteli na malori.
“Nimekuwa nikihusishwa na mali hizo kwa sababu ni za marafiki zangu,” anasema Ridhiwani.
“Kuna marafiki zangu ambao nimewakuta wakiwa wana
mali zao, lakini katika maisha kwa sababu wanaendelea kuhangaika,
wanaendelea kupata mali pia. Hao nao wanadai kwamba Ridhiwani
anashirikiana nao,” alisema.
“Mimi nataka kukwambia hayo yote unayoyasikia
sijui ya Uda, sijui ya Lake Oil na nini, hao wote ni watu ninaofahamiana
nao katika safari za maisha. Sina ushirika wowote nao wa kusema labda
wana uhusiano wowote wa kibiashara na mimi. Ndani ya hizo kampuni zao
mimi sina lolote.”
Alitoa mfano wa mwendeshaji wa Uda, Robert Kisena,
akieleza kuwa alijuana naye mwaka 2003 na kwamba alimkuta Mwanza akiwa
na kampuni yake ya Simon Group ambayo ilikuwa inasaga mbegu za pamba na
kutoa mashudu.
“Nilimkuta akiwa na kiwanda cha pamba Malampaka.
Nilimkuta anajenga kiwanda cha tumbaku Kaliua kule kwa Mzee (mbunge wa
Urambo Magharibi, Juma) Kapuya. Kwa hiyo leo hii yeye anapojitanua
kibiashara na kuwa mmiliki wa sehemu ya Uda, hilo jambo halihusiani na
mimi. Ni yeye Kisena na harakati zake.
“Kwa sababu yeye anakopa, ananunua vitu, anauza
vitu, kusafirisha na kuuza vitu. Sasa watu wanategemea akikutana na
Ridhiwani ndiyo arudi chini, ni kitu ambacho hakiwezekani.”
Pia, alimzungumzia rafiki yake Saidi Mtanda,
ambaye ni mbunge wa Mchinga akisema wakati akiwa mwenyekiti wa Umoja wa
Vijana Wilaya ya Bagamoyo, alikuwa mhamasishaji wake.
“Amekuwa rafiki yangu tangu enzi hizo, amekuwa
mbunge, mbona hajapewa hata unaibu waziri. Mbona watu hawazumgumzii hilo
kwamba Ridhiwani amemnyima rafiki yake uwaziri. Wanachoangalia ni wale
waliofanikiwa tu. Lazima wajue katika safari ya maisha kufanikiwa ni
sehemu ya maisha na kutopata pia ni sehemu ya maisha.”
Mahojiano kamili ‘Swali na Jibu’ na Ridhiwani yatakuwa Ndani ya Habari kuanzia kesho
No comments
Post a Comment