Writen by
sadataley
3:05 PM
-
0
Comments
Na Fidelis Butahe, MwananchiDar es Salaam. Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imetoa tamko zito ikieleza kushangazwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kupinga mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya Watanzania na kusema kitendo hicho kimeishusha hadhi Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyoiteua.
Tamko hilo la CCT ni mwendelezo wa lawama ambazo
Rais Kikwete amekuwa akitupiwa na taasisi na watu mbalimbali kutokana na
mchakato wa kuandika Katiba Mpya kwenda mrama baada ya mkuu huyo wa
nchi kueleza maoni yake dhidi ya mapendekezo ya muundo wa Serikali ya
Muungano wakati akilihutubia Bunge la Katiba.
Miongoni mwa watu waliojitokeza kuzungumzia kauli
hiyo katika siku za karibuni ni aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa,
John Tendwa, maaskofu wa Kanisa Katoliki, katibu mkuu wa Chadema, Dk
Willbrod Slaa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharrif
Hamad.
Jana, CCT iligongomea msumari juu ya lawama hizo
ikifananisha kauli ya kiongozi huyo aliyoitoa Machi 21, mwaka huu wakati
akifungua Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma na mama anayeamua kubeba
mimba na kujifungua kwa uchungu, kisha kumtelekeza mtoto, badala ya
kumfurahia.
Pia katika tamko lake (limechapishwa kwa ukamilifu
Uk. 36 wa gazeti hili), jumuiya hiyo imewataka wajumbe wa Bunge hilo
kuheshimu maoni ya Watanzania yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kuacha
kujadili maoni ya vyama vyao vya siasa.
“Inashangaza jinsi chama kimoja cha siasa
kinavyolazimisha wabunge na wanachama wake kukubaliana na mapendekezo
yake ambayo yanapingana wazi na yaliyomo katika rasimu ya Katiba,”
linaeleza tamko hilo lililotolewa baada ya Mkutano wa 48 wa Halmashauri
Kuu ya Jumuiya hiyo uliofanyika Julai 2 na 3 mjini Dodoma.
Tamko hilo pia limetaja mambo mengine saba yanayolikabili Taifa.
Kabla ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa
ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba kutoa rasimu ya pili ya Katiba Desemba
30, CCM ilisambaza waraka kuwaarifu wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka
CCM kuwa msimamo wa chama hicho tawala ni Muungano wa serikali mbili,
tofauti na mapendekezo ya wananchi yaliyo kwenye rasimu hiyo ambayo
yanataka serikali tatu.
Licha ya mara kadhaa Jaji Warioba kutetea kile
kilichopendekezwa na Tume yake, wajumbe hao kutoka CCM wameyapinga maoni
hayo na kusisitiza kuwa yanaweza kubadilishwa kadri Bunge la Katiba
litakavyoona inafaa.
Kitendo hicho kilisababisha wajumbe kutoka vyama
vingine kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao Aprili 16
uliamua kususia vikao vya Bunge hilo ukitoa masharti kuwa utarejea
bungeni kama chombo hicho cha kuandika Katiba kitajikita kujadili
mapendekezo ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba.
Bunge hilo litaendelea na vikao vyake Agosti 5 na mwenyekiti wake, Samuel Sitta anahaha kushawishi Ukawa walegeze msimamo wao.
Katika hotuba yake ya kufungua Bunge la Katiba,
Rais Kikwete aligusia mambo kadhaa yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na
kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha kuwa mengine hayawezekani
kutekelezeka, ikiwa ni pamoja na muundo wa serikali tatu kwa maelezo
kuwa idadi ya watu waliotaka muundo huo ni ndogo.
“Tunampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kutoa wazo la kuandikwa kwa Katiba Mpya na kuteua wajumbe wa Bunge la Katiba. Tunaamini kilichoandikwa katika Rasimu hiyo alikikubali na kubariki kutolewa kwa rasimu hiyo kwa sababu alijua ndiyo maoni ya wananchi,” linasema tamko hilo.
“Tunampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kutoa wazo la kuandikwa kwa Katiba Mpya na kuteua wajumbe wa Bunge la Katiba. Tunaamini kilichoandikwa katika Rasimu hiyo alikikubali na kubariki kutolewa kwa rasimu hiyo kwa sababu alijua ndiyo maoni ya wananchi,” linasema tamko hilo.
“Pia tunaamini kuwa mwenye kutoa hoja (Rais
Kikwete) alikuwa na uwezo wa kuzuia rasimu hiyo isitolewe endapo kuna
ibara ambayo ina mwelekeo ambao ungekuwa hatari kwa mustakabali wa taifa
letu.”
Jumuiya hiyo imesema kitendo cha Rais Kikwete
kupingana na kilichomo katika rasimu ya Katiba kimeshusha hadhi ya
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Hotuba hiyo ilishusha hadhi ya kazi nzuri
iliyofanywa na wajumbe wa Tume ambao waliteuliwa na rais mwenyewe kwa
ajili ya kukusanya maoni ya wananchi,” linasema tamko hilo.
“Jambo hili linaweza kufananishwa na mama
anayeamua kubeba mimba, kuilea mimba hiyo kwa gharama na kujifungua kwa
uchungu halafu mtoto akishazaliwa, badala ya kufurahi anaamua
kumtelekeza.”
Ushauri kwa vyama
Tamko hilo linasema: “Viongozi wa vyama vya siasa
na wabunge waheshimu uhuru wa mawazo ya wanachama wao hata kama
watatofautiana katika hoja moja au nyingine na wasitumie nafasi zao
kulazimisha wanachama wote kukubaliana na mawazo yao.”
Jumuiya hiyo imeifananisha hatua hiyo na udikteta kwa wanachama wa chama husika.
“Katika jambo hili CCT inahimiza wabunge wote waangalie masilahi ya kitaifa kwa upana zaidi na siyo ya vyama vyao.”
Inasema licha ya kuwa wakati wa kutoa maoni CCT
ilipendekeza muundo wa serikali moja, inakubaliana na pendekezo la
kuwapo serikali tatu kwa sababu ni maoni yaliyotolewa na wananchi
walioamini kuwa zitamaliza kero za muungano.
Lugha za kejeli
Katika tamko hilo, CCT imeshangazwa jinsi vikao
vya Bunge la Katiba vilivyotawaliwa na mjadala wa muundo wa serikali,
huku mambo mengine ya msingi yaliyomo katika rasimu ya Katiba yakiwekwa
kando.
“Lugha zisizo za kiungwana zinazotolewa na baadhi ya wajumbe wa
Bunge la Katiba kwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba zinaonyesha
ni jinsi gani wabunge hao wasivyoheshimu uteuzi wa wajumbe wa Tume
hiyo,” linasema tamko hilo.
Katika tamko hilo, CCT pia iligusia suala la
udini, maadili, kukosekana kwa uvumilivu wa kisiasa nchini, mauaji ya
raia, uchaguzi, umasikini na ulipaji wa kodi, hasa kwa mashirika ya
dini.
No comments
Post a Comment