Writen by
sadataley
6:18 PM
-
0
Comments
Moshi. Mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo
amemtaka Rais Jakaya Kikwete na chama chake, CCM kuwa makini na msimamo
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akisema haamini kama umoja huo
umesema kila unachokusudia kukifanya.
Badala yake Kisumo alisema kinachofanywa na Ukawa
ni mbinu za kujiimarisha kisiasa, jambo alilolisema iwapo CCM na
Serikali yake haitakuwa makini, huenda ikaingia katika mtego na
kushindwa kujinasua baada ya umoja huo kuimarika.
Kauli ya Mzee Kisumo imekuja wakati ambao viongozi
wa Ukawa wameendelea kusisitiza kwamba wataendelea kususia vikao vya
Bunge Maalumu la Katiba vinavyoanza mjini Dodoma, Agosti 5 mwaka huu,
hadi pale madai yao yatakapozingatiwa.
Ukawa ambao unaundwa na Vyama vya Chadema, NCCR
Mageuzi, CUF na baadhi ya wajumbe kutoka kundi la wajumbe 201
walioteuliwa na Rais, wanasisitiza kwamba lazima Bunge hilo lijadili
Rasimu ya Katiba kama ilivyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba
na wakitaka pendekezo la muungano wa serikali tatu lizingatiwe.
Kamati zote 12 za Bunge hilo katika maoni ya wengi
zilipendekeza muundo wa Serikali mbili tofauti na uliopendekezwa katika
rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kisumo alisema
kinachotakiwa ni Ukawa kurudi bungeni wakabishane kwa hoja na kama
wakishindwa, bado wenye uamuzi wa mwisho juu ya Katiba ni wananchi kwa
kupiga kura ya ndio au hapana.
Awananga Z’Bar
Wakati huohuo, Kisumo alisema kuna unafiki
miongoni mwa wanachama wa CCM Zanzibar ambao alisema wanasaliti kwa siri
sera ya chama hicho ya muundo wa serikali mbili.
Alionyesha kushangazwa na baadhi ya wana CCM Zanzibar kupinga waziwazi sera hiyo ya CCM na kushabikia serikali tatu.
“CCM ina kamati maalumu kule Zanzibar na Tanzania
Bara vilevile, lakini inaelekea kamati ile ya Zanzibar haina nguvu ya
kuwabana wachache hawa wanaokiuka sera zake,” alisema Kisumo aliyepata
kuwa mdhamini wa CCM kwa muda mrefu.
Kisumo alitoa mfano uamuzi wa kumvua uanachama
aliyekuwa mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mansour Yusuph Himid kuwa
haukupata uungwaji mkono Zanzibar.
“Kama sera ya CCM ni serikali mbili sasa
anapotokea mtu anashabikia serikali tatu ni lazima chama kiwe na msimamo
kuwa huyu siyo mwenzetu na uamuzi huo uungwe mkono,” alisema.
No comments
Post a Comment