Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Monday, February 24, 2014

Sifuri zatawala kidato cha nne

“Hawa wa mwaka juzi (2012)  D ilikuwa ni kuanzia alama 35 mpaka 39 na mwaka 2013 ikaanzia 30 mpaka 39, kwa hiyo yawezekana kabisa kuwa matokeo haya ni sawa na yale ya mwaka jana au ni mabaya zaidi.” Rakesh Rajani 
Na Fredy Azzah, Mwananchi
Dar es Salaam. Licha ya Baraza la Mitihani kueleza kuwa ufaulu katika matokeo ya Kidato cha Nne Mwaka 2013 umeongezeka kwa asilimia 15.17, baadhi ya wadau wa elimu wamesema yawezekana matokeo hayo ama yakawa sawa na yale ya mwaka 2012 au mabaya zaidi.
Wanafunzi waliopata daraja sifuri mwaka 2012 walikuwa ni 210,846 sawa na asilimia 56.92 ya watahiniwa  458,139,  wakati mwaka 2013, waliopata daraja hilo ni 151,187 sawa na asilimia 42.91 ya watahiniwa 404,083. Waliopata daraja la kwanza mpaka la nne mwaka 2012 walikuwa ni 124,260 sawa na asilimia 33.54 huku mwaka 2013 waliopata daraja hilo wakiwa 126,828 sawa na asilimia 36.
Waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu mwaka 2012 walikuwa ni watahiniwa 35,349 sawa na asilimia 9.55 huku wale wa mwaka 2013 wakiwa 74,324 sawa na asilimia 21.09.
Mkurugenzi wa Twaweza, Rakesh Rajani alilieleza Mwananchi jana kuwa, ni vigumu kuyafananisha matokeo ya mwaka 2013 na yale ya mwaka 2012 kutokana na kubadilika kwa mfumo wa kuyapanga.
“Ni vigumu kuyalinganisha haya matokeo, ni sawa na kumfananisha golikipa aliyedaka mpira wakati goli likiwa na upana wa mita tano na mwingine aliyedaka wakati goli likiwa na mita sita.
Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Herme Mosha alisema  ingawa matokeo yanaonekana kupanda, lazima uwekezaji zaidi uwekwe kwenye sekta ya elimu.
“Matokeo bado ni mabaya ukilinganisha na hali halisi, shule nyingi za umma zimefanya vibaya kutokana na kutokuwapo na uwekezaji wa kutosha, lazima tuwekeze kwenye elimu,” alisema Profesa Mosha.
Awali alama za ufaulu zilizotangazwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Profesa Sifuni Mchome, ni A:75-100, B+:60-74, B:50-59, C:40-49, D:30-39, E:20-29 na F:=0-19.
Kwa mfumo huu, alama ya ufaulu ilikuwa iwe E na CA zilitakiwa kuchangia asilimia 40. Hata hivyo mfumo huo haukutumika kama ilivyotangazwa na badala yake alama ya ufaulu imekuwa D na CA zimechangia 30, jambo ambalo bado halijawafurahisha wadau.
Necta yafafanua
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde amefafanua juu ya mfumo uliotumika kupanga mwaka 2013 huku akisema hata mtoto wa kidato cha pili angeweza kufaulu mtihani huo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Dk Msonde alisema alama ya ufaulu kwenye matokeo hayo ilikuwa ni D, lakini ili mwanafunzi awekwe kwenye fungu la waliofaulu ni lazima apate angalau C moja au D mbili kwenye masomo yake yote.
Kuna watu wanasema, inakuwaje mimi mtoto wangu amepata pointi 42 lakini inaonekana kapata daraja la sifuri na wapo waliopata pointi 46 lakini wapo kwenye daraja la nne.
“Mtu ukipata E zote ambazo ndiyo msingi wa kupata pointi, utaonekana una pointi 42, na mwingne akapata F sita na C moja anaonekana amefaulu licha ya yeye kuwa na point 46,” alisema.
Akifafanua juu ya alama zilizotumika kwenye mtihani huo, alisema A: 1, B+:2, B:3, C:4, D:5, E:6 na F:7. na kwamba A:75-100, B+:60-74,B:50-59,C:40-49,D:30-39,E:20-29 na F:0-19.
“Kwa upande wa pointi, Daraja la Kwanza awali ilikuwa ni kuanzia pointi 7- 17, na halikubadilika, daraja la pili ilikuwa ni 18-21 sasa  ni 18-24, daraja la tatu zamani 22-25 sasa hivi 25-31, daraja la nne zamani ilikuwa 26-32 sasa ni 32-46 na sifuri zamani ilikuwa ni 33-35 sasa ni 47-49,” alisema.
Akizungumzia ubora wa matokeo hayo, alisema kuwa 2013 watahiniwa wamejitahidi ukilinganisha na wale wa 2012.
Chanzo:www.mwananchi.co.tz
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment