Writen by
sadataley
6:57 AM
-
0
Comments
Polisi mjini London Jumamosi imepandisha idadi ya watu waliofariki na kufikia watu 58 ambao wamethibitishwa kufariki ama wanafikiriwa wamefariki kufuatia moto uliozuka katika jengo refu la mjini London la Grenfell Tower.
Ghadhabu ya umma inaongezeka wakati wakaazi na majirani wanadai majibu kuhusu kwa nini moto huo uliozuka mapema alfajiri siku ya Jumatano ulisambaa haraka na kuwanasa watu wengi wakaazi wapatao 600 wa jengo hilo . Vyombo vya habari nchini Uingereza vimeripoti kwamba wakandarasi waliweka vifaa hafifu, ambavyo havizuwii moto katika kuta za nje za jengo hilo lenye ghorofa 24 katika ukarabati ambao ulimalizika mwaka jana tu.
Kamanda wa polisi Stuart Cundy alisema idadi ya watu 58 waliofariki inatokana na ripoti kutoka kwa umma na huenda ikaongezeka. Inajumuisha watu 30 waliofariki ambao tayari wamethibitishwa, na ripoti za watu ambao bado hawajulikani waliko na wanaaminika kwamba wamefariki. Amesema itachukua wiki kadhaa ama hata zaidi kuwapata na kuwatambua wote waliofariki katika jengo hilo.
"Bahati mbaya, katika wakati huu kuna watu 58 ambao wameelezwa kwamba walikuwamo katika jengo hilo la Grenfell Tower katika usiku huo ambao hawajulikani waliko. Na kwa hiyo , kwa masikitiko, nataka niamini kwamba wamefariki," alisema.
Amesema polisi watatafakari kuchukua hatua za kihalifu iwapo kutakuwa na ushahidi wa makosa na kwamba uchunguzi wa polisi utajumuisha uchunguzi wa mradi huo wa ukarabati katika jengo hilo, ambao wataalamu wanaamini umesababisha jengo hilo kuwa katika hali mbya ya kukabiliwa na maafa ya moto.
Polisi wamepata shida ya kupata idadi rasmi ya nani alikuwa katika jengo hilo wakati moto ulipozuka, na kufanya kuwa vigumu kutambua ni watu wangapi wamefariki.
Watu wengi hawajulikani waliko
Cundy amesema huenda kulikuwa na watu wengine katika jengo hilo ambao polisi haina habari nao, na kwamba inaweza kuongeza idadi ya vifo. Amemtaka kila mtu ambaye alikuwa katika jengo hilo na ambaye amenusurika kuwasiliana na polisi mara moja.
Polisi imesema msako wa mabaki ya miili ya watu ulisita siku ya Ijumaa kutokana na wasi wasi wa usalama katika jengo hilo lililoungua moto lakini sasa zoezi hilo limeanza tena.
Cundy amesema wafanyakazi wa kutoa huduma ya dharura sasa wamefikia juu kabisa mwa jengo hilo.
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May , akikabiliwa na ukosoaji kwa jinsi serikali ilivyoshughulikia maafa hayo, alikutana jana Jumamosi (17.06.2017)na watu 15 walionusurika katika moto waliokaribishwa ofisini kwake mtaa wa Downing namba 10. Kundi hilo liliondoka baada ya mkutano ambao ulidumu kwa zaidi ya masaa mawili lakini hawakuzungumza na waandishi habari waliokusanyika nje ya ofisi hiyo.
Maandamano mjini London wakipinga jinsi utawala wa waziri mkuu Theresa May ulivyoshughulikia maafa hayo mjini London
Mkutano huo huenda utatuliza malalamiko kwamba May amekuwa taratibu mno kuwawafikia watu walionusurika, licha ya kutangaza mfuko wa dola milioni 6.4 wa dharura kuwasaidia familia ambazo hazina makaazi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Sudi Mnette
DW Swahili
No comments
Post a Comment