Writen by
sadataley
5:01 PM
-
0
Comments
Nyarugusu. Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi
(UNHCR) imeeleza kuwa Tanzania ndiyo nchi inayoongoza kwa kuhifadhi
idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Burundi, miongoni mwa nchi za Afrika
Mashariki.
Ripoti hiyo imetolewa wakati jana dunia iliadhimisha siku ya wakimbizi duniani.
Imeonyesha kuwa hadi sasa, kuna wakimbizi 245,000 kutoka Burundi wanaoishi katika kambi zilizopo Kigoma.
UNHCR imeeleza kuwa idadi kubwa ya wakimbizi hao, ni watoto ambao ni asilimia 60 ya wakimbizi wote.
“Katika kipindi cha miezi mitano ya mwaka 2017, wakimbizi 44,487 waliingia nchini wakitokea Burundi,” imeeleza ripoti hiyo.
UNHCR inasema huu ni mzigo mkubwa kwa Tanzania lakini kwa bahati mbaya,
nchi hii haipati fedha za kutosha kuwahudumia wakimbizi na wengine
wanaotafuta hifadhi.
Kwa mfano, kambi ya Nyarugusu, ambayo ni moja ya kambi kubwa za wakimbizi duniani, inahifadhi wakimbizi 139,000.
Ripoti hiyo imeisifu Tanzania kwa kuendelea kubeba mzigo huu mkubwa wa
wakimbizi lakini zaidi kwa kukubali kutekeleza mkakati mpya wa kimataifa
wa kutafuta namna endelevu ya kuwasaidia wakimbizi na kuwapa mahitaji
na ulinzi.
“Lakini zaidi sana mkakati huu una dhamira ya kutafuta namna ya
kuwashirikisha wakimbizi hawa katika shughuli mbalimbali za maendeleo
katika nchi wanazokimbilia,” imesema ripoti hiyo.
No comments
Post a Comment