Writen by
sadataley
4:47 PM
-
0
Comments
Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai ameonyesha kuumizwa na kitendo cha baadhi
ya wabunge wa upinzani kutojumuika pamoja na wabunge wenzao katika
masuala ya kijamii ikiwepo kususia futari iliyokuwa imeandaliwa na
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Kufuatia jambo hilo Ndugai amewaomba viongozi na wabunge kwa pamoja
kuachana na mambo ya kujitenda kwani yanaweza kuleta athari kubwa ambazo
hakuna anayehitaji, na kudai kama kuna mambo ambayo yanakwaza basi
viongozi hao wanapaswa kukaa pamoja na kumaliza mambo hayo.
"Tumekuwa tukiandaa baadhi ya hizi shughuli siku ile ya bajeti tulipata
nafasi ya kupata futari iliyokuwa imeandaliwa na Waziri Mkuu na wageni
wote waliokuwepo, mabalozi tulihudhuria pale na ilikuwa imeandaliwa kwa
wema kwa kweli. Leo (jana) pia na mimi nimepata nafasi ya kuandaa kama
nilivyowataarifu lakini nikajifunza kitu kimoja ambacho sikupenda
kukisema lakini ngoja nikiseme hapa kidogo, kuna baadhi yetu wengine
wamekatazana rasmi kutohudhuria shughuli kama hizi, sasa mimi sitaki
kuingilia uhuru wao, wana haki kufanya hivyo kama wanaona ni sawa lakini
mimi mwenzao ningependa kuwashauri tu hasa viongozi wanaofanya mambo
hayo kutazama tena njia zao, yako mambo mengine ni ya kijamii tu,
ukifika mahali kiongozi unaanza kuwazuia watu hata mambo ya kijamii ujue
unaenda mbali kidogo" alisema Ndugai
Spika wa Bunge aliendelea kutoa malalamiko yake dhidi ya vitendo vya
baadhi ya wabunge wa upinzani kususia shughuli hizo za kijamii ambazo
zinawaweka pamoja na kusema
"Hili bunge linavyoendeshwa labda wabunge wa kambi mbalimbali mnaweza
msielewe bunge hili linaendeshwa katika mawasiliano mbalimbali ya sisi
kwa sisi endapo kuna jambo linakwaza mpaka linasababisha hata watu
wasipate futari kwa pamoja basi ni vizuri viongozi wa pande zote tukakaa
tuzungumze na kuondoa vikwazo hivyo kama vipo maana mimi sijui kama
vipo lakini kama havipo ni vizuri tuwe tunajumuika kwa pamoja, maana
sera hizo zikienea na hakika kabisa na pande zingine nazo zitaanza na
hakika matokeo yake italeta mipasuko ambayo hakuna anayehitaji hapa"
alisisitiza Job Ndugai
Ndugai alisema kuwa yeye anatambua kuwa wanamjibu na kufanya
wanayoyafanya lakini Mungu anajua kuwa wanachokifanya si busara kwa
kufanya hivyo na kusema kuwa katika mwezi huu mtukufu wanapaswa
kusameheana, kuombeana, kutoa mikono upande wa pili na kufanya ibada
kwani si mwezi wa chuki na kubaguana.
No comments
Post a Comment