Writen by
sadataley
4:49 PM
-
0
Comments
BUNGE limeelezwa kuwa ni vigumu mfungwa mwanamke wa kifungo cha muda mrefu kupata mimba akiwa gerezani.
Hayo yalibainishwa jana bungeni na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mwigulu Nchemba, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti
Maalum (CUF), Raisa Abdallah Mussa.
Mbunge huyo alitaka kujua ni kwanini sehemu ya magereza inayoaminika
kama ni sehemu salama, lakini wanawake wanapata mimba wakiwa gerezani.
Akijibu swali hilo, Mwigulu alisema amezunguka katika magereza yote na
hakuna eneo ambalo amefika na kukuta mwanamke aliyefungwa kifungo cha
muda mrefu amegundulika kuwa na mimba akiwa kwenye kifungo hicho.
“Ni kweli unaweza kukuta wale wenye kifungo cha muda mfupi wakajifungua
wakiwa gerezani, lakini kujifungua wakiwa gerezani haina maana kuwa
mimba kaipatia gerezani,” alisema Mwigulu.
Alibainisha kutokana na sheria kali za majeshi likiwamo Jeshi la
Magereza, haitawezekana mwanamke mfungwa apate mimba akiwa ndani ya
gereza halafu taarifa zikafichwa.
Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua serikali imejipanga
vipi katika kuwanusuru watoto ambao wanawake wamekuwa wakijifungua
wakiwa magerezani.
“Je, serikali haioni kuwa inavunja haki za binadamu kwa kuwaweka
magerezani watoto hao wasio na makosa, na je, inaweza kulipa Bunge
takwimu za wanawake waliokinzana na sheria na kufungwa kwa miaka mitano
iliyopita?” alihoji.
Akijibu swali hilo la msingi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad
Yusuf Masauni, alisema kwa muda wa miaka mitano jumla ya wanawake 2,008
walikinzana na sheria na kufungwa magerezani.
Aidha, alisema kwa watoto kuwapo magerezani na wazazi wao ni kutokana na
sheria ya mtoto ya kutaka mtoto kupata haki yake ya kunyonya maziwa ya
mama.
No comments
Post a Comment