Writen by
sadataley
10:46 AM
-
0
Comments
Msikiti wa Al Aqsa
Maandamano ya siku ya Quds mjini London
Intifadha au mwamko wa Wapalestina unazidi kuchacha huku Siku ya Kimataifa ya Quds ikikaribia jambo ambalo limewatia kiwewe wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Pamoja na kuwa utawala huo wa Kizayuni umechukua hatua kadhaa za utumiaji mabavu kukandamiza mwamko wa Wapalestina katika siku za hivi karibuni lakini utawala huo pandikizi, sawa na siku za nyuma, umefeli kukabiliana na Intifadha.
Hakuna shaka kuwa kufanyika Siku ya Kimataifa ya Quds ni chanzo cha Wapalestina kupata motisha zaidi wa kuendeleza mapambano ya kukomboa ardhi zao kutoka makucha ya utawala ghasibu wa Israel. Kufuatia kuongezeka njama za kudhoofisha kadhia ya Palestina sambamba na njama za Marekani za kuunga mkono mkakati hatari wa utawala wa Kizayuni wa kueneza satwa kamili katika Quds Tukufu, Wapalestina wanatazamia kupata uungaji mkono zaidi wa walimwengu kwa harakati zao za ukombozi.
Katika hali kama hii tunashuhudia kushadidi uchochezi wa Rais Donald Trump wa Marekani kwa lengo la kuimarisha sera za utawala wa Kizayuni wa Israel katika kudhibiti kikamilifu Quds Tukufu. Katika upande mwingine watawala wa nchi za Kiarabu nao wanafuata kibubusa maamurisho ya Marekani ya kuwa na uhusiano na utawala wa Israel na hivyo wao pia kuwa sehemu ya njama dhidi ya Quds Tukufu.
Katika miaka ya hivi karibuni, watawala wa nchi nyingi za Kiarabu pamoja na kuwa wanadai kuunga mkono Wapalestina lakini uhalisia wa mambo ni kuwa si tu kuwa hawaungi mkono Palestina bali wanashirikiana na utawala haramu wa Israel katika kuwakadamiza Wapalestina. Ni katika mazingira kama haya ndio tukasuhudia malengo matukufu ya Wapalestina hasa mustakabali wa Quds Tukufu, yakikabiliwa na hatari na tishio kubwa.
Katika mazingira kama haya, Wapalestina waliamua kuanzisha mwamko au Intifadha kukabilianan na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel na muungaji mkono wake mkuu, yaani Marekani.
Kumekuwepo na Intifadha kadhaa ambapo ya kwanza ilianza mwaka 1987, ya pili ambayo ni maarufu kama Intifadha ya Al Aqsa mwaka 2000 na Intifadha ya tatu ambayo ni maarufu kama Intifadha ya Quds ikaanza Oktoba mwaka 2015 na ingali inaendelea hadi sasa. Katika Intifadha hii kadhia ya ukombozi wa Quds Tukufu imepewa umuhimu wa kipekee katika malengo matukufu ya Wapalestina.
Kwa msingi huo, ubunifu uliotolewa na shakhsia muhimu wa ulimwengu wa Kiislamu ni jambo ambalo limepelekea ifahamike kuwa Wapalestina hawako peke yao katika mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kwamba Waislamu daima wako nao katika mapambano hayo. Ni kwa msingi huo ndio maana Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mnamo Agosti Mosi 1979 akatangaza kuwa, Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani iwe ni Siku ya Kimataifa ya Quds kwa lengo la kuhakikisha kuwa Wapalestina wanapata uungaji mkono wa kimataifa katika mapambano yao.
Kwa hakika Imam Khomeini MA alikuwa na nafasi muhimu katika kuibuka Intifadha ya Kimataifa kwa lengo la kuunga mkono kadhia ya Palestina hasa ukombozi wa mji wa Quds.
Kuongozeka harakati za kimataifa katika kuunga mkono Quds Tukufu miongoni mwa wakaazi wa mabara yote matano ya dunia ni ishara ya malalamiko ya kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Akthari ya watu wa dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds kwa njia mbali mbali huku wakibainisha kuchukizwa kwao na utawala wa Kizayuni wa Israel na waitifaki wake wa Magharibi ambao wanahusika katika kuwakandamiza Wapalestina.
Ubunifu wa Imam Khomeini umepelekea kuwepo mwamko wa watu wa maeneo mbali mbali ya dunia kuhusu ukombozi wa Palestina na hasa Quds Tukufu na hivyo weledi wa mambo ya kisiasa wameitaja siku hiyo kuwa Intifadha ya kimataifa katika kuunga mkono watu wa Palestina. Kimsingi siku ya kimataifa ya Quds imepelekea wafuasi wa dini zote duniani kuungana kwa sauti moja katika kuwaunga mkono Wapalestina sambamba na kutangaza mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni na waitifaki wake yaani uistikbari wa kimataifa. Kuhusu kufanyika siku ya kimataifa ya Quds kupitia makundi ya kijamii duniani mwaka huu, Masoud Shadjareh Mkuu wa Tume ya Kiislamu ya Haki za Binadamu mjini London anasema: "Siku ya Kimataifa ya Quds ina umuhimu hasa maandamano ya kutangaza kufungamana na taifa madhlumu la Palestina." Aidha ameashiria kufanyika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds jana Jumapili mjini London Uingereza ambapo maelfu ya watu walijitokeza kuunga mkono ukombozi wa Palestina na kulaani utawala ghasibu wa Israel. Anasema tokea Imam Khomeini MA atoe fatwa ya kufanyika Siku ya Kimatiafa ya Quds, wakaazi wa London wamekuwa wakifanya maandamano katika siku hiyo kila mwaka. Anasema Siku ya Kimataifa ya Quds sasa imebadilika na kuwa moja kati ya hafla za kudumu za kila mwaka mjini London.
No comments
Post a Comment