Writen by
sadataley
7:59 AM
-
0
Comments
Hivi karibuni Waziri wa fedha na mipango, Dr Philip Mpango aliwasilisha bajeti kuu ya Serikali ya mpango wa maendeleo ya Taifa na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018 huku dhana yake kuu ikiwa ni kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi.
Kabla ya kuwasilisha bajeti, waziri huyo aliwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa ambayo ilijikita katika kuelezea mipango ya maendeleo kwa mwaka ujao.
Tarehe 8 Juni nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, Rwanda na Uganda zilitangaza bajeti zao, huku Kenya ikitangulia kutangaza yake mwezi Machi kwa ajili ya kuilinganisha na maandalizi ya kura za urais inayotarajiwa kupigwa mwezi August.
Bajeti hiyo ambayo imeonekana kutoa kipaumbele kwenye masuala yatakayoweza kupunguza makali ya maisha kwa watanzania, imepokelewa kwa mitazamo tofauti.
Waziri Kivuli wa kambi rasmi ya upinzani wa Fedha na Mipango, Mh.Halima Mdee ameizungumzia Bajeti ya mwaka 2017/18 kuwa imewabeba zaidi wakulima kwa kuwapunguzia zaidi ushuru wa kusafirisha mazao na kuwasahau wafanyakazi hali inayoweza kuzorotesha maendeleo nchini na kusema kuwa Serikali ilipaswa kuangalia kada zote kwa uwiano sawa.
Hata hivyo amesema kuwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/18 takwimu za vitabu vyake vya mapato na matumizi zinatofautiana, ambapo kitabu cha mapato kinaonyesha kwa mwaka Serikali 2017/18 itakusanya Sh trilioni 23.9, huku kitabu cha matumizi kikionyesha inakusudia kutumia Sh trilioni 26.9, ikiwa ni ongezeko la Sh trilioni 3, wakati huo huo sura ya bajeti inaonyesha bajeti kwa mwaka 2017/18 ni Sh trilioni 31.7.
Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa dini wameipongeza bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18 wakisema inalenga kuondoa kero za wananchi wa hali ya chini huku wengine wakisema ni bajeti ya maumivu kwa watu wa hali ya chini baada ya gharama za mafuta kuongezeka.
Akitoa maoni, Padri Deus Mulokozi wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma amesema bajeti hiyo imekidhi matakwa ya wananchi ingawa bado hajafahamu wananchi wameipokea vipi. “Kimsingi yale tuliyokuwa tunayapinga kidogo yamerekebishwa, nataka niwapongeze wabunge kwa kuwapigania wananchi hadi kuleta bajeti nzuri, kazi iliyobaki ni sisi kushirikiana na Serikali kuhakikisha tunayafikia malengo,”amesema.
Hata hivyo amesema katika kipindi cha miaka mingi haijawahi kutokea bajeti nzuri iliyowalenga wananchi wa chini kama ya mwaka huu na kutolea mfano maeneo ya kodi katika mazao ya wakulima, pembejeo, mbolea na kodi za magari za kila mwaka kuwa ziliwaumiza wakulima.
Mbali na hayo amesema kuwa ni jambo zuri kwa Serikali kuondoa kodi za magari za kila mwaka lakini kwa kuifidia katika mafuta kunalenga kumuongezea mzigo mwananchi wa hali ya chini.
Pamoja na hayo baadhi ya wabunge wameizungumzia bajeti hii na kusema kuwa ni changa la macho kwa sababu asilimia 37 ya fedha inategemea mikopo yenye masharti nafuu na misaada kutoka nje ya nchi ambapo wakati mwingine wahisani huwa hawatoi fedha hizo na hivyo kukwamisha malengo ya maendeleo.
Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia amesema bajeti hiyo ina mapungufu kwa sababu asilimia 37 ya fedha inategemea mikopo yenye masharti nafuu na misaada kutoka nje ya nchi huku Deni la Taifa likiwa limekua kutoka shilingi trilioni39 hadi 50.
Akitoa maoni kuhusu bajeti ya mwaka huu Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Mh.Maftaha Nachuma amesema ni bajeti ambayo imeakisi matakwa ya wananchi kwa kuondoa ushuru ambao ni kero kwenye maeneo mbalimbali.
“Kwa kuwa bajeti ya mwaka huu imeondoa ushuru katika bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi, hali hii italeta unafuu kwa kuwa ndiyo kilikuwa kilio chetu, sasa kitafanya watu ambao walikimbia kutumia bandari zetu kurejea na hivyo kukuza uchumi wa nchi,” amesema.
Hata hivyo mtaalamummoja wa masuala ya uchumi anasema kuwa,uzoefu unaonyesha kuwa maranyingi bajeti huwa na mambo mazuri lakini utekelezaji wake unakuwa ni tofauti kwani hata ile iliyopita utekelezaji wake haukuridhisha.
Daud Manase akitoa maoni yake katika majadiliano na gazeti hili amesema kuwa bajeti ya mwaka jana haikutimia kabisa ambapo anasema malengo ilikuwa kukusanya trilioni 29.5 lakini ilipatikana trilioni 20.1 ambayo ni sawa na asilimia 70.1 wakati bajeti ya mwaka huu ni trilioni 31.6 ongezeko la trilioni 11.
Kutokana na bajeti ya mwaka huu wananchi wengi wameonekana kuifurahia japo wataalamu wa masuala ya uchumi wanaonya kuwa huenda isitimie.
Chanzo: tec1956.blog
No comments
Post a Comment