Writen by
sadataley
9:57 AM
-
0
Comments
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila amesema kuwa Waziri Mkuu mpya anatarajiwa kuteuliwa kwa muda wa saa 48 zijazo.
Akilihotubia bunge la Senate na Bunge la kitaifa jijini Kinshasa siku ya Jumatano, rais Kabila ameutaka muungano wa upinzani kukubaliana na kumpa jina la yule wanayempendekeza kuwa Waziri Mkuu.
Akishangiliwa na Maseneta na Wabunge waliokuwa wamefurika katika majengo ya bunge, rais huyo amesema kuwa baada ya uteuzi wa Waziri Mkuu, serikali ya mpito itaundwa mara moja.
Upinzani wamekuwa wakisema kuwa wanataka kupendekeza jina moja huku upande wa serikali ukisema kuwa upinzani kupendekeza majina matatu na rais kumteua mmoja.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu, kiongozi huyo wa taifa hilo kubwa la Afrika ya Kati ambaye amekuwa uongozini tangu mwaka 2001, amesema kuwa zoezi hilo litafanyika kama ilivyopangwa na Tume ya Uchaguzi CENI.
Aidha, amewataka mataifa ya nje ya nchi kuacha kuingilia maswala ya nchi hiyo na kuongeza kuwa hawatakubali kuchochewa kisiasa.
Mkataba wa kisiasa uliotiwa saini kati ya upinzani na serikali mwezi Desemba mwaka 2016 unataka kuwepo kwa serikali ya mpito, Waziri Mkuu akitokea upinzani na kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwisho wa mwaka.
Muda wa rais Kabila kukaa madarakani ulikamilika mwaka uliopita lakini kwa sababu ya mzozo wa kisiasa nchini humo, baada ya serikali kusema haina fedha za kuandaa Uchaguzi huo.
Maaskofu wa Kanisa Katoliki waliongoza mazungumzo haya na kusaidia kupata mwafaka lakini wamekuwa wakiwalaumu wanasiasa wa upinzani na serikali kutoonesha nia ya kutekeleza mkataba huo.RFI
No comments
Post a Comment