Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema sera za nchi hiyo kuhusiana na masuala ya fedha hazitabadilika na kuwa watu nchini humo watapaswa kuendelea kuwa watulivu baada ya uwezo wake wa kukopesheka kushushwa.
Hatua hiyo inafuatia tathimini iliyofanywa na taasisi ya Standard and Poor inayoangalia uwezo wa nchi kulipa mikopo yake.
Tathimini ya taasisi hiyo ya Standard and Poor imetolewa ikiwa ni siku chache baada ya Rais Jacob Zuma kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri ambapo amemuweka kando aliyekuwa waziri wa fedha wa nchi hiyo Pravin Gordhan.
Rais Jacob Zuma hii leo amelitaka baraza lake la mawaziri kuwahakikishia wawekezaji wa kimataifa kuwa mabadiliko aliyofanya ya kumfuta kazi waziri wa fedha Pravin Gordhan hayatakuwa na athari kwa wawekezaji nchini humo na kusisitiza kuwa kilichobadilika ni uteuzi wa nafasi ya kisiasa pekee bali sera za nchi hiyo kuhusiana na uwekezaji zinabaki kuwa kama zilivyo.
Amesema mabadiliko hayo yanalengo la kuongeza ufanisi katika serikali ya nchi hiyo kwani ameteua mawaziri vijana wenye uwezo.
Hata hivyo wakati Rais Zuma akitoa kauli hiyo shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini humo Cosatu limemtaka Rais Zuma ajiuzulu mara moja kufuatia mabadiliko aliyoyafanya katika baraza lake la mawaziri kushusha kiwango cha nchi hiyo kukopesheka.
Katibu Mkuu wa shirikisho hilo la Cosatu Bheki Ntshalintshali amesema ni wakati muafaka Rais Zuma kujiuzulu kutokana na mabadiliko aliyoyafanya kuonekana kutokuungwa mkono ambapo katika mabadiliko hayo amemuweka kando aliyekuwa waziri wa fedha ambaye shirikisho hilo limesema ni waziri aliyekuwa mwenye uwezo na anayeheshimika zaidi.
No comments
Post a Comment