Writen by
sadataley
1:22 PM
-
0
Comments
Na Waandishi Wetu, MwananchiDar es Salaam. Kikao cha mashauriano kilichoitishwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta kinatarajiwa kuanza leo lakini wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wamesisitiza kuwa hawatashiriki.
Wakati Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe akitoa
msimamo huo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif
Hamad amesema haoni dalili za kupatikana Katiba hiyo kutokana na makundi
mawili yaliyopo katika Bunge hilo kuendelea kugawanyika kuhusu idadi ya
Serikali katika Muungano, jambo ambalo linaweka njiapanda uwezekano wa
kupatikana Katiba Mpya.
Akizungumza jana, Mbowe alisema wajumbe wa umoja
huo hawatashiriki kikao cha siku mbili kilichoitishwa na Sitta kwa
sababu ni sehemu ya Bunge la Katiba ambalo wajumbe wa Ukawa walisusia
vikao vyake tangu Aprili 16.
“Hatutahudhuria wala hatutakwenda katika kikao
chochote kinachohusiana na Bunge la Katiba, huo ndiyo msimamo wetu,”
alisema Mbowe kwa simu akiwa safarini kwenda Arusha.
Alisema Ukawa wapo katika vikao vya mazungumzo
vinavyoratibiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
ambavyo alisema ndivyo vitawapa mwelekeo kama watarejea katika Bunge la
Katiba au la... “Msimamo wetu ni kuwa hatutashiriki katika Bunge la
Katiba mpaka hapo utakapopatikana mwafaka.”
Mbowe alisema Ukawa inaamini kuwa
kitakachojadiliwa katika kikao hicho cha Sitta hakitakuwa tofauti na
kilichojitokeza katika Bunge la Katiba.
Sitta aliitisha kikao hicho cha wajumbe 30
wakiwamo viongozi wa Ukawa, kwa lengo la kutathmini mwenendo wa vikao
vya Bunge hilo na kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuondokana na
mgawanyiko.
Maalim Seif
Akiwa katika ziara ya kutembelea wanachama wa
chama hicho ambao ni wagonjwa katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani,
Maalim Seif alimweleza mwandishi wetu kuwa: “Sioni matumaini ya
kupatikana kwa Katiba Mpya kwani makundi mawili yaliyomo katika Bunge
hilo yanatofautiana sana, jambo linalonipa shaka endapo Katiba Mpya
itapatikana,” alisema na kuongeza:
“Kuna kundi lenye wajumbe wengi la CCM linataka
serikali mbili na kundi jingine linajiita Ukawa linatetea maoni ya
wananchi lakini makundi haya yanatofautiana sana, kila kundi lina
misimamo yake lakini kinachotakiwa ni kuheshimiwa kwa maoni ya
wananchi.”
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF,
alisema ili Katiba Mpya ipatikane, lazima maoni yaliyotolewa na wananchi
yaheshimiwe na mjadala ujikite katika rasimu iliyoandaliwa na Tume ya
Jaji Warioba.
Kuhusu Ukawa kuhudhuria kikao cha mashauriano,
Maalim Seif alisema: “Ninachojua hawatakwenda kwani wakienda ni sawa
wamerejea katika Bunge hilo. Walichokipinga ni kutetea uvunjifu wa
utaratibu lakini huyo aliyeitisha kamati hiyo ndiye huyohuyo aliyeongoza
Bunge, sasa ukihudhuria kamati hiyo inamaanisha kwamba umerejea
bungeni.”
Kauli ya Sitta
Akizungumza baada ya misa ya mazishi ya Profesa na
mtafiti wa tiba asilia katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Afya Muhimbili
(MUHAS), Zacharia Mbwambo iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kimara Dar es Salaam juzi, Sitta
alisema kikao kinachoanza leo si cha upatanishi kama ambavyo watu wengi
wamekuwa wakikichukulia bali, ni kwa ajili ya kuweka wazi tofauti
zilizopo miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo kabla vikao rasmi havijaanza
Agosti 5, mwaka huu.
“Watu wametafsiri vibaya, kikao hiki hakitarajii
kufanya usuluhishi wowote kwa kuwa hakuna ugomvi, isipokuwa kujadili na
kuweka wazi baadhi ya mambo yanayoonekana kuwa yanakanganya miongoni mwa
wajumbe 621 wa Bunge hili,” alisema Sitta.
Akizungumzia msimamo wa Ukawa wa kususia vikao,
Sitta alisema aliwataka kufikiria vizuri kwa kuwa kuna vipengele ambavyo
havina tatizo kwao, hivyo ni vyema wakarudi bungeni na kuvijadili huku
wakivipinga vile wanavyoona haviko sawa kwao.
Kuhusu madai ya kubadili rasimu iliyowasilishwa na
Jaji Warioba iliyotokana na mapendekezo ya wananchi, Sitta alisema
mchakato wa Katiba Mpya unapitia hatua nyingi na kila moja inaangalia
namna ya kuboresha hatua iliyotangulia.
“Rasimu ya Warioba si msahafu ambao hauhitaji
kubadilishwa. Kuna baadhi ya vipengele vinataka hivyo na ndiyo maana
tunaijadili ili kufika kule tutakako. Kama tume peke yake ingekuwa
imemaliza kila kitu kusingekuwa na umuhimu wa Bunge hili. Ni vizuri kila
mjumbe akatambua hilo. Iwapo kuna tofauti kama wanavyodai Ukawa,
sidhani kama kususia vikao ni jambo mwafaka litakalosaidia kuipata
Katiba bora,” alifafanua.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Julius Mathias na Ibrahim Yamola.
No comments
Post a Comment