Writen by
sadataley
6:32 PM
-
0
Comments
Na Hamida Shariff,MwananchiMtoto huyo aliyefariki akiwa na umri wa miaka minne, alifariki Juni Mosi kwenye Hospitali ya Muhimbili kutokana na maradhi ya homa ya mapafu. Aliishi kwenye boksi tangu alipokuwa na umri wa miezi tisa.
Watu katika mazishi hayo walianza kujitokeza
kwenye Uwanja wa Jamhuri kuanzia saa 1:00 asubuhi na mwili huo
ulifikishwa uwanjani hapo saa moja baadaye.
Baada ya mwili wa marehemu kuingizwa katika uwanja
huo vilio vilisikika kutoka kwa watu mbalimbali zaidi kina mama na
wanafunzi wa shule za msingi wakiimba... “Tuna imani na Mahakama, tuna
imani na sheria.”
Wakati salamu mbalimbali zikitolewa, baba mzazi wa Nasra, Rashid Mvungi alikuwa ameinamisha kichwa huku akitokwa na machozi.
Kabla ya shughuli ya kutoa heshima za mwisho
kuanza, bibi wa marehemu, Asha Abdallah aliingia uwanjani hapo akilia na
kuomba kukaa meza kuu ili ashuhudie shughuli za kumuaga mjukuu wake.
Baada ya mwili wa mjukuu wake kuondolewa kupelekwa
makaburi ya Kola, bibi huyo alianza kueleza namna alivyoupokea msiba
huo akisema kwa kipindi chote Nasra alipochukuliwa na mama yake mkubwa,
hakuwahi kumuona mjukuu wake.
“Mariamu (mama mkubwa wa Nasra) ni mtoto wangu
lakini baada ya kumchukua Nasra nilikuwa nikimwambia kila siku niletee
mjukuu wangu nimuone au njoo unichukue nikamwone mjukuu wangu lakini
alikuwa akiniahidi kesho mara kesho kutwa na mimi nilikuwa sipajui
nyumbani kwake,” alisema bibi huyo.
Hata hivyo, alielezea kusikitishwa na hatua ya
Serikali kuamua kumzika mjukuu wake bila ya kumshirikisha akisema hana
hatia kwani alitamani kumlea lakini Mariamu alimchukua naye aliamini
kuwa angemlea vizuri.
Mazishi hayo yalihudhuriwa pia na kaka wa
marehemu, Nasoro Mahamba aliyekuwa amesindikizwa na shangazi yake, Tatu
Mahamba. Nasoro alisema tangu akiwa na miaka minne alikuwa akiishi na
shangazi yake huyo na alikuwa akienda kumtembelea marehemu mama yake
wakati wa likizo tu.
Nasoro alisema alipoteza mawasiliano na mama yake mkubwa na kushindwa kujua jinsi ya kumwona mdogo wake.
Nasoro alisema siku ambayo Nasra alipelekwa
Muhimbili alikwenda Hospitali ya Morogoro lakini alishindwa kuzungumza
naye kutokana na hali yake kuwa mbaya.
Hata hivyo, Mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu
katika Shule ya Sekondari Kihonda, alishindwa kufika makaburini kumzika
mdogo wake akisema anasumbuliwa na tatizo la moyo hivyo kuhofia
kuanguka.
No comments
Post a Comment