Writen by
sadataley
10:42 AM
-
0
Comments
Na Daniel Mjema, Mwananchi
Dodoma. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe amesema ataipa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) jukumu la kuchunguza ufisadi wa mamilioni
ya fedha katika ununuzi wa tiketi za safari za nje za wizara yake.
Ahadi hiyo ilitokana na tishio la Mbunge wa Ole,
Rajab Mbaruku la kutishia kuondoa shilingi endapo Waziri Membe asingetoa
mkakati wa kupambana na ufisadi huo ulioibuliwa kwenye taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo ilifichua
ununuzi wa tiketi kwa bei ya juu zaidi ya mara 16 ya bei halisi ya soko.
Katika taarifa yake alibaini ukiukwaji wa sheria
za ununuzi na kwamba tiketi 56 zilizotakiwa kununuliwa kwa Sh700.9
milioni, zilinunuliwa kwa Sh974.5 milioni ikiwa ni ongezeko la Sh273.6.
milioni jambo ambalo ni kinyume cha mikataba ya Mawakala wa Huduma za
Manunuzi (GPSA).
CAG pia alibaini kuwa katika tiketi 22
zilizochukuliwa zikiwakilisha safari 239 za maofisa wa wizara,
zilionyesha kuwa tiketi hizo zilitozwa zaidi ya kiwango kilichokubaliwa.
Juzi, Mbaruku ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), alimbana Waziri Membe
akitaka atoe ahadi ya jinsi wizara yake itakavyoshughulikia suala hilo
na asipofanya hivyo, angeondoa shilingi kwenye mshahara wake, hatua
ambayo ingesababisha kukwama bajeti hiyo.
Hata hivyo, katika majibu yake Waziri Membe
alijikita zaidi katika kutetea misafara ya Rais, baada ya wabunge
kulalamikia kuwa inatumia fedha nyingi za serikali kwa kuwa inakuwa na
watu wengi, jibu ambalo halikumlidhisha Mbaruku.
“Sijaridhika na majibu ya waziri amejielekeza
zaidi kwenye safari za Rais. Nilichokizungumza mimi ni kuzingatia kanuni
za ununuzi wa umma kwamba inakiukwa,” alisema Mbaruku.
“Pia nimetoa mifano miwili ya safari ambazo
zimefanywa na maofisa wake na hazikuwa za kushtukiza ambazo zimetumia
fedha nyingi tofauti na zile zilizotakiwa kutumiwa katika uhalisia
wake.”
“Kwa hiyo bado nashikilia shilingi ya mshahara wa
waziri hadi atoe commitment (hakikisho) namna ya kushughulikia ufisadi
unaofanywa na maofisa wake.”
Ndipo Membe aliposema: “Mimi nilikuwa nataka tu
nimshauri mwenzangu... kwa kuwa ni kitu specific cha watu... Kwa nini
asitupe muda sisi twende tukalifanyie kazi kwa sababu siyo jambo kubwa.
“Siyo suala la sera ni watu mafisadi kama
anavyowaita. Wako mle, tutakwenda kuchunguza na tutaomba wenzetu wa
Takukuru waliangalie halafu mambo yakienda vizuri nitaleta taarifa hapa
bungeni,” alisema.
Kauli ya Membe ilionekana kumgusa Naibu Spika, Job
Ndugai, ambaye alimsihi Mbaruku alichukue jambo hilo ili
likashughulikiwe na kamati za Bunge hasa ikizingatiwa yeye ni mwenyekiti
wa LAAC.
Kwa habari ziadi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Membe-aikaribisha-Takukuru-wizarani/-/1597296/2329916/-/wnc526z/-/index.html
Kwa habari ziadi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Membe-aikaribisha-Takukuru-wizarani/-/1597296/2329916/-/wnc526z/-/index.html
No comments
Post a Comment