Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Tuesday, April 29, 2014

Ushirikiano huu wa ‘Ukawa’ uwe endelevu


Hakuna ubishi kwamba upinzani wenye nguvu huisukuma serikali ichape kazi na kuwatumikia wananchi kwa kutambua kwamba ikiboronga itaondolewa madarakani na serikali kivuli ambayo ni vyama vya upinzani. 
Na Mwananchi
Bila shaka kila mwananchi anayeitakia mema nchi yetu amevutiwa na habari zilizochapishwa katika gazeti hili jana kwamba vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimeamua kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani.
Viongozi wakuu wa vyama hivyo tayari wamekubaliana kuanza mchakato huo na wameandika mapendekezo na kuyapeleka katika sekretarieti za vyama vyao kwa ajili ya kufanyiwa uchambuzi.
Sisi tunaona kitendo hicho cha vyama vinavyounda Ukawa kuwa ni hatua muhimu ya kuongeza nguvu ili kuongeza ushindani ambao ni muhimu katika mustakabali wa nchi yetu kisiasa na hivyo kusaidia nyanja nyingine za kiuchumi na kijamii.
Tangu kuruhusiwa tena kwa siasa huru karibu miaka 22 sasa, bado nchi haijashuhudia ushindani wa kweli unaoweza kuwafanya watawala kuwajibika kwa wananchi kutokana na kuona hatari ya kuondolewa madarakani na vyama pinzani.
Hii imetokana na vyama shindani katika siasa kukumbwa na mifarakano ya kisiasa ambayo imekuwa ikiwagawa na hivyo kuingia kwenye chaguzi vikiwa dhaifu na hivyo kushindwa vibaya na chama tawala na matokeo yake yamekuwa ni wananchi wengi kukata tamaa na hivyo kusababisha idadi ya wanaoshiriki kupiga kura kupungua mwaka hadi mwaka kutokana na kutoona faida ya siasa za ushindani.
Pengine hiyo ndiyo sababu iliyofanya wananchi wapendekeze kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba vyama viruhusiwe kuunganisha nguvu wakati wa chaguzi kwa kuwa wameona bila ya nguvu ya vyama shindani, watawala wawataendelea kuongoza kwa mazoea na matokeo yake ni wananchi kuendelea na umaskini wao na kuona uhuru wa vyama vya kisiasa hausaidii kuwa kuboresha maisha yao.
Si nia yetu kuona chama tawala kikiondolewa madarakani na vyama shindani, lakini tunachotaka kuona na ushindani wa dhati, makini na wa kweli ambao, kwa taifa lolote lile, ni afya kwa ustawi wa wa taifa kwa kuwa huongeza uwajibikaji kwa watawala.
Hakuna ubishi kwamba upinzani wenye nguvu huisukuma serikali ichape kazi na kuwatumikia wananchi kwa kutambua kwamba ikiboronga itaondolewa madarakani na serikali kivuli ambayo ni vyama vya upinzani.
Vyama legelege vya upinzani huogopa kivuli cha serikali na kufifisha maendeleo na kuzima matumaini ya wananchi wanaotaka kuona uwajibikaji serikalini, kwani huwa chachu ya kuendeleza tawala za kiimla zisizothamini demokrasia na zisizowajibika kwa wananchi.
Ndiyo maana tunawapongeza viongozi wa Ukawa kwa kuona umuhimu wa kuunganisha nguvu na kuwa wamoja ili kuweka ushindani wa kweli katika mazingira ya kisiasa tuliyomo.
Tunachoweza kuwashauri viongozi wa Ukawa ni kuwa makini na kuondoa tofauti zinazowatenganisha. Ukawa isitarajie kwamba kila kitu kitakuwa mteremko, kwani bado sheria kandamizi ambazo zimekuwa zikikwaza shughuli za upinzani bado hazijafutwa.
Ni matarajio yetu kwamba serikali na chama tawala kitachukulia hatua hiyo ya Ukawa kuwa changamoto ya kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi na si kuanza kujenga chuki na kutafuta mbinu za kuikwamisha.
Serikali haina budi kuhakikisha kuwa vyama vyote vinapewa nafasi sawa ya ushindani na kujengewa mazingira ya kukua ili kukifanya chama chochote kinachopewa madaraka kiwajibike kwa wananchi na kuwaletea maendeleo.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment