Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Tuesday, April 29, 2014

Jaji Samatta, Prof Lumumba kutumika kuwarejesha Ukawa bungeni

Huwezi kuwalazimisha watu kuamua jambo ambalo hawalitaki kama ni muundo wa Muungano tunaomba wananchi ndiyo waamue, lakini yote hayo Katiba yetu inatakiwa kubainisha mambo mbalimbali yanayohusu watu wenye ulemavu na haki zao zote,”PICHA|MAKTABA 
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Wiki hii Bunge Maalumu la Katiba limeahirishwa, kupisha Bunge la Bajeti kuanza vikao vyake vya bajeti kwa mwaka mpya wa fedha wa 2014/15.
Hata hivyo, Bunge hilo limeahirishwa likiwa limegawanyika vipande, baada ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya Bunge hilo Aprili 16, wakipinga kejeli, matusi na mambo mengine ya ukiukwaji wa taratibu yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya mawaziri nje ya Bunge.
Kutoka kwa Ukawa nje unaojumuisha vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, DP na wajumbe 25 kutoka kundi la 201 hakukuzuia Bunge hilo kuendelea na vikao vyake. Bunge hilo limeahirishwa Agosti 5, litakapokutana tena mjini Dodoma kuendelea na majadala wa kuijadili Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba.
Kundi la Tanzania Kwanza linalojumuisha wajumbe wengi wa CCM, wamekuwa wakiwapiga vijembe kuwa warudi bungeni kuendelea na mjadala huo kwani Katiba haitengenezwi nje ya Bunge.
Jukata yasaka suluhu
Kutokana na mgawanyiko huo kuonyesha kuligawa taifa na kuwaacha wananchi wakiwa njiapanda juu ya hatima ya kupata Katiba Mpya, Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) linajipambanua kutaka kusaka suluhu ya mvutano huo.
Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba anasema, Jukwaa hilo linajitolea kusaka suluhu kwa kuratibu maridhiano ya makundi yanayovutana ya Ukawa na la Tanzania Kwanza.
Anasema lengo la kusaka maridhiano hayo ni kuhakikisha kabla ya Bunge hilo kuanza Agosti 5, kunakuwapo maridhiano, yatakayowezesha wajumbe wote wanakuwa kitu kimoja katika kujadili maudhui ya rasimu, licha ya tofauti zao za kiitikadi na kimisimamo.
Kibamba anasema wameamua kuwaalika wataalamu ambao wana uzoefu wa siku nyingi katika masuala ya sheria kusimamia maridhiano hayo, yatakayojenga umoja na mshikamano katika taifa.
Wataalamu hao kwa mujibu wa Kibamba ni Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Barnabas Samatta anayekuwa mwenyekiti, Profesa Patrice Lumumba kutoka nchini Kenya ambaye atakuwa msuluhishi mwenza sambamba na uwepo wa makundi ya viongozi kutoka Ukawa, Tanzania Kwanza, vyama vya siasa, asasi za wananchi na taasisi zote muhimu zilizoguswa na mchakato huu.
“Katika kujenga Katiba yenye kuwajali wananchi, tunaomba kila upande kuridhia kukutana na kutokuwa na misimamo mikali ili kuhakikisha tunawaunganisha na kuendelea na mchakato huo kama kawaida,” anasema Kimbamba.
Kuhusu uhalali wa Bunge hilo kuendelea na mijadala licha ya Ukawa kutoka nje, anasema sheria za Jumuiya ya Madola kwa mabunge ya Katiba kundi moja linapotoka nje kwa tamko, Bunge hilo hutakiwa kusitishwa.
“Ukawa wametoka nje tena wakiwa zaidi ya 190, Bunge lilitakiwa kusitishwa na kupata maridhiano kwanza si kama wanavyotumia akidi vibaya kuliendesha Bunge hilo,” anasema Kibamba.
Aliongeza: “Jukata bado inaamini kwamba mwaka 2014 Katiba Mpya haitapatikana, hivyo kunahitajika kufanyiwa marekebisho makubwa Katiba ya sasa hasa vifungu vinavyohusu uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi ujao unafanyika kwa amani.”
Maoni ya wadau
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania, Felician Mkude anasema, maridhiano yanahitajika ili kuweza kupata uwakilishi ndani ya Bunge hilo kwa ufasaha.
Anasema, kuendelea na mvutano kuhusu aina gani ya Muungano, si jambo la maana na kinachotakiwa kufanyika ni wananchi kupiga kura ya muundo gani unaostahili.
“Huwezi kuwalazimisha watu kuamua jambo ambalo hawalitaki kama ni muundo wa Muungano tunaomba wananchi ndiyo waamue, lakini yote hayo Katiba yetu inatakiwa kubainisha mambo mbalimbali yanayohusu watu wenye ulemavu na haki zao zote,” anasema Mkude.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Idd Makombe anasema mvutano uliokuwa ukiendelea bungeni kuhusu muundo wa Muungano haukuuimarisha bali unauvuruga.
Dk Makombe anasema, uwazi na maridhiano ndio utakaowezesha kuipata Katiba Mpya yenye kuwajali Watanzania wote.
“Kunahitajika kufanyika kwa kura ya maoni kuhusiana aina gani ya Muungano wananchi wanataka, kwani hivi sasa watu hatuaminiani na huwezi kumlazimisha mtu jambo ambalo halitaki, hivyo pande zote mbili zifikie maridhiano kwa amani,” anasema Dk Makombe.
Mhadhiri wa Chuo Kiuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi na Utawala, Richard Mbunda anasema nchi inapitia katika kipindi kigumu kutokana na kauli na mienendo mbalimbali inayoendelea kujitokeza.
Mbunda anasema viongozi wa kidini na Serikali wanapotoa kauli wanatakiwa kuwa makini, kwani zinaweza kuliingiza taifa katika vurugu za kidini au za kisiasa.
Kauli ya Rais Kikwete
Akizungumza na Vijana na Wazee wa Chama Cha Mapinduzi kutoka Tanzania Bara na Visiwani juzi kwenye Ukumbi wa PTA Sabasaba, Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete amewataka Ukawa kurejea bungeni kuendelea na mjadala wa kutunga Katiba.
Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), limeingilia kati mpasuko uliojitokeza katika Bunge Maalumu la Katiba kwa kusaka wasuluhishi watakaorejesha maridhiano ya pande mbili zinazokinzana.
Rais Kikwete anasema, katika kuandika Katiba ya Watanzania kunahitajika kufanya maridhiano ili kuhakikisha mchakato huo unamalizika salama kwa wananchi kupata Katiba yenye kujali masilahi yao.
MWISHO
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment