Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Tuesday, December 31, 2013

Serikali ya Tanganyika yaibuliwa katika Rasimu ya pili

Jambo jingine jipya ni kupunguzwa kwa madaraka ya uteuzi ya Rais kwa kuweka vyombo vya kupendekeza majina ya watu wa kuteuliwa na baadhi ya vyeo kuhitaji kuthibitishwa na Bunge.PICHA|MAKTABA 
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Dar es Salaam.Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa Rasimu ya Pili ya Katiba ikiwa na mambo sita mpya, huku ikiendelea kupendekeza Muungano wa Serikali tatu na kurejea kwa nchi ya Tanganyika.
Rasimu hiyo ya Pili ambayo imetolewa miezi saba baada ya Rasimu ya Kwanza, ilikabidhiwa jana kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba katika hafla iliyofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam. Akizungumza kabla ya kukabidhi rasimu hiyo, Jaji Warioba alisema ina Ibara 271, tofauti na ile ya kwanza iliyokuwa na Ibara 240.
Alisema ripoti ya rasimu hiyo pia ina maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba, sera, sheria na utekelezaji maoni ya Mabaraza ya Katiba, takwimu za ukusanyaji wa maoni ya wananchi, makala za utafiti kuhusu mabadiliko ya Katiba na viambatanisho vya ripoti ya mabadiliko ya Katiba.
Mambo mapya
Maeneo yaliyofanyiwa marekebisho baada ya mchakato wa Mabaraza ya Katiba yaliyokutana kuanzia Julai 12 hadi Septemba 2 mwaka huu ni kuongezwa kwa vipengele kuhusu haki za binadamu.
Miongoni mwao ni haki ya kutoa na kupata habari. Pia imetaja haki za makundi maalumu yakiwamo ya watoto, vijana, wazee, walemavu na wanawake.
Kuhusu uraia, Jaji Warioba alisema imependekezwa uraia wa Tanzania kuwa mmoja tu na kutambuliwa kwa uraia wa kuzaliwa na wa kujiandikisha wa nchi moja. Alisema imependekeza pia kutoa fursa kwa uraia wa nchi mbili.
Jambo jingine jipya ni kupunguzwa kwa madaraka ya uteuzi ya Rais kwa kuweka vyombo vya kupendekeza majina ya watu wa kuteuliwa na baadhi ya vyeo kuhitaji kuthibitishwa na Bunge.
Aidha, alisema rasimu hiyo imependekeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iwe taasisi inayojitegemea badala ya kuwa sehemu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kama ilivyokuwa katika Rasimu ya Kwanza.
“Rasimu inapendekeza kuwepo na Jeshi moja la polisi na Idara moja ya Usalama kwa taifa zima, siyo kama tulivyokuwa imependekezwa katika rasimu ya kwanza kwamba kila upande unaweza kuanzisha jeshi lake la polisi,” alisema.
Muungano
Akizungumzia Muungano na jinsi Tume ilivyofanya uchambuzi wa pendekezo lake la Serikali tatu alisema: “Katika Rasimu ya Kwanza tulieleza kuwa kuendelea kwa Serikali mbili kulihitaji ukarabati mkubwa ambao tuliona hautawezekana.
“Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilieleza Tume itaongozwa na msingi mkuu wa kitaifa na maadili ya jamii ya kuhifadhi na kudumisha mambo kadhaa muhimu, moja ya mambo hayo ilikuwa ni kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano. Tume ilianza kazi kwa madhumuni ya kupata maoni ya kuboresha Muungano.”
Alisema watu wengi walizungumzia Muungano, lakini wengi wao walijikita katika muundo wake. Kwa Tanzania Bara, wananchi zaidi ya 39,000 walitoa maoni yao kuhusu muungano, kati yao 27,000 walizungumzia muundo wake. Kwa upande wa Zanzibar, kati ya wananchi 38,000 waliotoa maoni 19,000 walizungumzia muundo wa Muungano.
“Tanzania Bara asilimia 13 walitaka Serikali moja, asilimia 24 walipendekeza Serikali mbili, asilimia 61 walipendekeza Serikali tatu. Kwa upande wa Zanzibar, asilimia 34 walipendekeza Serikali mbili na asilimia 60 walipendekeza Muungano wa mkataba na watu 25 sawa na asilimia 0.1 walitaka Serikali moja,” alisema.
Alisema vyama vya siasa, taasisi za kidini, asasi za kiraia na baadhi ya taasisi za Serikali zilipendekeza muundo wa Serikali tatu, huku akitolea mfano wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Baraza la Katiba Ofisi ya Waziri Mkuu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Malalamiko Muungano
Alisema kila upande wa Muungano una malalamiko mengi kuhusu muundo na kwamba tume hiyo imeorodhesha malalamiko 10 kwa upande wa Zanzibar na manane kwa upande wa Tanzania Bara.
Alisema kwa upande wa Zanzibar, malalamiko matatu makubwa ni Serikali ya Tanganyika kuvaa koti la Serikali ya Muungano ambalo linaisaidia zaidi Tanganyika kuliko Zanzibar na kuifanya Tanganyika kuwa Tanzania.
Pili, mambo ya Muungano kuongezeka na kuathiri madaraka na kuishusha hadhi Zanzibar na tatu ni kumuondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Alisema kwa Tanzania Bara, malalamiko makubwa ni Zanzibar kuwa nchi huru yenye bendera yake, wimbo wa taifa, serikali yake na imebadili Katiba yake ili ijitambue kama nchi, wakati Tanzania Bara imepoteza utambulisho wake. Katiba ya Jamhuri inasema Tanzania ni nchi moja lakini Katiba ya Zanzibar inasema ni nchi mbili.
Pili, Zanzibar imebadili Katiba yake na kuchukua madaraka ya Jamhuri ya Muungano, kuelekeza sheria za Muungano zinazopitishwa na Bunge la Muungano zipelekwe kwanza kwenye Baraza la Wawakilishi kabla ya kutumika.
Tatu, wananchi wa Tanzania bara kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi Zanzibar, wakati wenzao wana haki hiyo Tanzania bara.
Muundo wa Muungano
Alisema katika kuchambua malalamiko ya Zanzibar, Tume imebaini kuwa muundo wa Muungano wa Serikali mbili umeifanya Serikali ya Muungano kushughulikia zaidi mambo ya Tanzania bara, hasa maendeleo na uchumi.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977, Serikali ya Muungano ina mamlaka ya kusimamia mambo ya Muungano na yasiyo na muungano kwa upande wa bara... “Kwa msingi huo, Serikali ya Muungano inashughulikia sana kilimo, elimu, afya, maji, nishati na madini, ujenzi, uchukuzi, maliasili na utalii na mengine ya Tanzania bara yasiyo ya Muungano.”
Alisema kutokana na hali hiyo, Tume haikuwa na njia nyingine kwa sababu Serikali ya Muungano haina madaraka ya kutosha juu ya mambo ya maendeleo na uchumi kwa upande wa Zanzibar na kwamba hata utafutaji wa rasilimali zaidi ni kwa ajili ya Tanzania bara kuliko Zanzibar.
Alisema Zanzibar inafanya mipango yake ya maendeleo, kwamba ili ipate rasilimali, kama mikopo na misaada, ni lazima ipitie Serikali ya Muungano jambo ambalo utekelezaji wake umesababisha matatizo mengi.
“Njia pekee ambayo ingeiwezesha Zanzibar kufaidi shughuli za Serikali ya Muungano wa maendeleo ya Zanzibar ni mambo yote kuwa chini ya Muungano kwa maana ya kuwa na Serikali moja, lakini hilo likifanyika kuna hofu ya Zanzibar kumezwa,” alisema.
Alisema tume hiyo imefanya uchambuzi wa mambo 22 ya Muungano ili kubaini kama yanaingilia hadhi ya uhuru wa Zanzibar na kubaini kuwa siyo yote yanayotekelezeka. Mengi yamebadilishwa bila kubadili Katiba au kwa makubaliano ya pande mbili.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni kodi, bandari, viwanda, usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, posta na simu, uraia, takwimu, mafuta na gesi na Mahakama ya Rufaa.
“Kama Katiba ya Zanzibar ikibaki kutakuwa na nchi mbili; zikiwa nchi mbili haitawezekana nchi moja iwe na hadhi na uhuru na nchi nyingine isiwe na hadhi na uhuru, kwa tathmini yetu, tunaona ukarabati huu ni mgumu. Serikali tatu ndiyo suluhisho,” alisema.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment