Writen by
sadataley
11:07 AM
-
0
Comments

Na Beatrice Moses,
Dar es Salaam. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi amesema wizara yake imeagiza wahusika kukagua na kuwachukulia hatua wanaouza dawa za mseto zaidi ya Sh 1,000 ambayo ni bei elekezi ya Serikali.
Dk Mwinyi aliyasema hayo jana baada ya kuzindua kipimo cha malaria kinachotoa majibu haraka kiitwacho Malaria Rapid Diagnostic Test (mRDT), ambavyo vitatumika kwenye vituo binafsi vya kutolea huduma za afya nchini.
“Bei ya dawa mseto ni changamoto, Serikali iliagiza ziuzwe kwa Sh1,000 lakini kuna taarifa kuwa baadhi wanauza hadi Sh2,500 tumeshaagiza mamlaka husika kufanya ukaguzi na kuwachukulia hatua za kisheria wale watakaobainika kukiuka bei hiyo,” alisema.
Akizungumzia kuhusu kipimo cha mRDT alisema Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NIMR) kwa kushirikiana na Taasisi ya Clinton Health Access Intiative (CHAI), wamewezesha upatikanaji wa kipimo hicho kwa bei nafuu katika sekta binafsi.
Dk Mwinyi alisema katika kutofautisha vipimo vya mRDT vinavyotumika Serikalini visitumike ama kuuzwa vile vya vituo binafsi vimewekwa alama ya ‘tiki’ yenye rangi ya bluu, ambayo ina kiwango cha ubora imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Dk Mwinyi amesema kipimo hicho sasa kimepunguzwa bei na kitauzwa kwa bei ya Sh1,100 au chini ya hapo ili wengi waweze kumudu gharama hiyo.
Chanzo:
No comments
Post a Comment