Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Thursday, September 5, 2013

Rais Kikwete aongoza mazishi ya Askofu Kulola

Waziri Mkuu aliyejiuzulu ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akisalimiana na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa jana wakati wa ibada ya mazishi ya Askofu Mkuu, Moses Kulola wa Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT) aliyezikwa nje ya Kanisa la Calvary Bugando jijini Mwanza. Na Mpigapicha Wetu   
Na Frederick Katulanda
Mwanza. Rais Jakaya Kikwete ameongoza maelfu ya waombolezaji kumzika aliyekuwa Askofu Mkuu Moses Kulola wa Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT). Kiongozi huyo alizikwa jana nje ya Kanisa la Calvary Bugando.
Licha ya kuongoza mazishi hayo, Rais Kikwete pia alitoa ushuhuda kwamba licha ya kuwa muumini wa dini ya Kiislamu, Askofu Kulola wakati wa uhai wake mara kadhaa alikwenda Ikulu kumfanyia maombi.
Rais Kikwete katika salamu zake za rambirambi, alisema amekwenda kushiriki msiba huo kuungana na waombolezaji kutokana na kumfahamu Askofu Kulola ambaye alikuwa mtu wa watu.
“Tuzidi kuwaombea kwa Mungu, familia katika kipindi hiki kigumu, kwa jinsi nilivyomfahamu marehemu alikuwa mpenda watu, hakujali kabila wala hali zao, alijali utu na heshima hii ndiyo sababu na mimi alikuwa rafiki yangu,” alieleza Rais Kikwete.
Alibainisha kwamba licha ya kuwa Muislamu mara kadhaa Askofu huyo alifika kumwombea Ikulu na katika maombezi yake alisisitiza kuwa alikuwa akiwaombea Watanzania na nchi nzima kwa ujumla, hivyo aliwahimiza walio hai kumuenzi Askofu kwa vitendo.
Kwa upande wake, Makamu Askofu Mkuu wa EAGT Asumwisye Mwaisabila, akizungumzia msiba huo kuwa marehemu Kulola alikuwa mchungaji wa aina yake na hivyo kuwataka wanaotaka kufanana naye kuomba kwa Mungu awajalie hekima.
“Alikuwa askofu wa ajabu sana, hata kama ungeweza kumtandikia mkeka ili alale, angelala. Jambo hili ni tofauti sana na maaskofu wa kileo ambao ukiwatendea hivyo watanung’unika na kukusema kila siku,” alieleza na kusisitiza wanapaswa kumuenzi kwa vitendo.
Katika Ibada ya maziko ya Askofu Kulola iliyoongozwa na Makamu Askofu Mkuu, Asumwisye Mwaisabila, mbali na Rais Kikwete pia Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibroad Slaa, aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo, Wabunge William Ngeleja (Sengerema), Ezekiel Wenje (Nyamagana), Highness Kiwia (Ilemela) pamoja na Mchungaji Peter Msigwa, ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini.
Wakati huohuo Rais Kikwete jana alisafiri kwenda Kampala, Uganda, kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment