Writen by
sadataley
2:41 PM
-
0
Comments
Dar es Salaam. Pascalina aliyefiwa na baba yake mwaka 1989 na
mama yake mwaka 1996 anasema hata alivyojaribu kuhoji kwa bosi wake
alijibiwa vibaya; “aliniambia ‘wewe hapa ni mfanyakazi wa ndani sasa
kazi yako ni nini ikiwa mtoto wangu afanye kazi mimi nakupa mshahara wa
bure humu ndani’ lile jibu ndilo lililoniondoa katika ile nyumba, miezi
minne niliyoishi ilikuwa mingi sana kwangu, niliona haina haja ni heri
nirudi kijijini,” anasema Pascalina mama wa watoto wawili sasa.
Esther Meshaki kutoka kijiji cha Ibagi, Kata ya
Mang’oto wilayani Makete aliunguzwa kwa maji ya moto baada ya bosi wake
wa kike kumfumania akitaka kubakwa na baba mwenye nyumba.
“Niliunguzwa kwa maji ya moto kifuani mwaka 1987,
nilikuwa nafanya kazi jijini Dar es Salaam, huko nilichukuliwa na baba
mmoja aliyekuja huku Makete kwa shughuli za kikazi, alinichukua nikiwa
mdogo sana kama miaka 16 hivi wakati huo nilikuwa nimetoka kumaliza
elimu ya msingi. Mkewe alinipokea vizuri tu. Nilifanya kazi kwake kwa
miaka 10, nikiwa na miaka sita nyumbani kwake mkewe alifariki dunia,
niliendelea kumlelea watoto wake na baada ya mwaka mmoja yule baba alioa
tena.
“Huyu mke aliyemuoa kilikuwa chanzo, alikuwa
hamtunzi mumewe ananipa majukumu yasiyo na msingi mwishowe yule baba
akaanza kunitaka kimapenzi, nilimkatalia siku moja usiku mkewe
alichelewa kurudi, matokeo yake yule baba aliingia chumbani kwangu na
kuanza kunilazimisha nilikataa wakati akiendelea kutaka kunikamata kwa
nguvu yule mama aliingia, waligombana na mwishowe nilijua yameisha.
Baada ya wiki moja yule mama alichukua sufuria ya
maji ya moto niliyotenga kwa ajili ya ubwabwa na kunimwagia kifuani,”
anasimulia.
Esther anasema alipelekwa hospitali na kutibiwa
ila alivyopona aliondoka na kurudi kwao Ibagi, “niliondoka lakini yule
baba alianza kuwa hanilipi fedha zangu kwa kuwa sikuwa nikikubaliana na
matakwa yake, nilirudi na majeraha yasiyo na fedha ya kujitibia,”
anasema Esther mwenye watoto sita na mjukuu mmoja.
Wapo waliopotezana na familia
Kuna idadi kubwa ya wazazi huwaruhusu watoto wao
kwenda kutafuta kazi za ndani pasipo kujua watakapofikia, hawa mara
nyingi hukosa mawasiliano na ndugu zao na iwapo atapatwa na matatizo ni
ngumu ndugu kujua.
Monica, 54, anayeishi kijiji cha Ivilikinge
Wilayani Makete anasema “Binti yangu aliondoka mwaka 1992 wakati huo
alikuwa na miaka 14 tu tangu hapo hakurudi tena mpaka leo, ilifikia
hatua tulitaka kufanya matanga ‘arobaini’ kwa kuamini kwamba amekufa
baadhi ya ndugu walikataa na kudai kuwa bado wana matumaini kuwa yupo
hai.”
Anasema binti yake aliondoka na kundi la wasichana
wenzake ambao wanasema waliachana Ubungo, baada ya mtu wasiyemfahamu
aliyefika kijijini hapo kutafuta wasichana kwa ajili ya kazi kuwatawanya
kwa watu mbalimbali stendi ya Mnazi Mmoja.
“Wenzake walisharudi siku nyingi sana wana watoto
wakubwa tu, sasa mimi nasema kila siku mwanangu yupo ila harudi, mpaka
sasa nimeshamsahau kabisa machoni mwangu naweza pishana naye
nisimtambue,” anasema Monica.
Agnetha Sanga, 34, anasema; “Mimi nimepotelewa na
mdogo wangu Zawadi Sanga mwaka 2006, tangu hapo mpaka leo hatujawahi
kuonana, kuna kipindi nilisikia kwamba anafanya kazi Mbeya mjini, ila
sina hakika kwani sijawahi kumuona tangu usiku huo alipotoroka huku
nyumbani.”
Kwahabari zaidi ingia
http://www.mwananchi.co.tz/habari/-/1597578/2001644/-/11noy2uz/-/index.html
Kwahabari zaidi ingia
http://www.mwananchi.co.tz/habari/-/1597578/2001644/-/11noy2uz/-/index.html
No comments
Post a Comment