Writen by
sadataley
2:35 PM
-
0
Comments
Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema (kulia) akiagana
na Wenyeviti wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF
(kushoto)Freeman Mbowe wa Chadema (wapili kulia) na James Mbatia wa
NCCR-Mageuzi, jijini Dar es Salaam jana. Picha Fidelis Felix
Dar es Salaam. Vyama vya siasa vya upinzani vya Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi, leo vitafanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya
Jangwani kuhamasisha wananchi wapinge kile wanachodai ni hujuma dhidi ya
Mchakato wa Katiba Mpya.
Hatua ya kufanya mkutano huo, ilifikiwa jana baada
ya wenyeviti wa vyama hivyo kumvamia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini
(IGP), Said Mwema ofisini kwake wakipinga kitendo cha Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Dar es Salaam kupiga marufuku maandamano waliyokuwa wayafanye
leo jijini humo.
Katika mkutano wao na IGP Mwema, viongozi hao
walikubaliana maandamano hayo yasitishwe kwa sababu za kiusalama, lakini
wafanye mkutano huo wa hadhara.
Wenyeviti hao wa vyama vya Upinzani, James Mbatia
wa NCCR-Mageuzi, Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba
(CUF), ambao walikutana na Mwema jana mchana.
Hatua ya viongozi hao ilitokana na tamko
lililotolewa juzi na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam,
Suleiman Kova kusitisha maandamano ya vyama hivyo yasifanyike.
Kova alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kuhofia
yatasababisha kusitishwa kwa shughuli za kiuchumi pamoja na kuwepo
taarifa za kiintelijensia kwamba yatakuwa na vurugu.
Tamko hilo liliwakera viongozi wa vyama hivyo
vitatu vilivyotangaza kushirikiana katika kupinga kile wanachodai ni
uporaji wa haki ya wananchi kutunga Katiba yao.
Mazungumzo wenyeviti hao na IGP yalianza saa 6
mchana na kumalizika saa 11 jioni, ambapo walitoa taarifa ya pamoja
kuhusu waliyokubaliana.
Akitangulia kutoa taarifa hiyo, kwa niaba ya
wenzake, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba alisema: “Tumekubaliana
kesho tutafanya mkutano Viwanja vya Jangwani. Tumekubaliana kusitisha
maandamano hadi Oktoba 5, (mwaka huu).”
Aliongeza kuwa wamekubaliana pia kwamba watafanya mkutano mwingine wa hadhara Visiwani Zanzibar, Jumatano ijayo.
Hata hivyo, katika taarifa ya pamoja, ulitokea kuhitilafiana kwa kauli, pale IGP Mwema alipokuwa akitoa ya upande wake.
Hali hiyo ilitokana na kauli ya Profesa Lipumba
kusisitiza kuwa mikutano na maandamano ni haki ya msingi kwa vyama vya
siasa na kwamba wanachopaswa ni kutoa taarifa kwa polisi na wala siyo
kuomba kibali.
Awali, wakati Mwema akihitimisha taarifa hiyo ya pamoja alisema
kuwa wanasiasa hao wanapaswa kuomba kibali cha maandamano hayo ya Oktoba
5.
Alisisitiza kuwa kazi ya polisi ni kuhakikisha
usalama wa raia na mali zao, hivyo wanasiasa hao wanapaswa kuomba kibali
na baada ya polisi kuchunguza watakuwa na mamlaka ya kuridhia au
kukataa ombi lao.
Mwema alisema haoni haja ya kuwepo malumbano na
wanasiasa hao katika suala hilo kwa sababu lengo lao ni moja nalo ni
kudumisha ustawi wa jamii.
“Wote tunajenga nyumba moja, sioni sababu ya kugombania fito,” alisema Mwema.
Mzozo wa Katiba
Mzozo wa vyama vya siasa vya upinzani ulianzia
kwenye Mkutano wa 12 wa Bunge uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma,
lakini sasa umehamia nje ya Bunge na vyama hivyo vimetangaza azma ya
kuanza kampeni ya kuuhamasisha umma kudai maridhiano kabla ya kuendelea
na mchakato wa Katiba Mpya.
Viongozi hao wa upinzani wanadai kwamba wabunge wa CCM waliongeza baadhi ya mambo kupitia majedwali ya marekebisho.
Wanadai kuwa hali hiyo inatoa mwanya kwa Serikali
inayoongozwa na CCM kupitia kwa rais kuwa na mamlaka zaidi ya uteuzi wa
wajumbe husika.
Vyama hivyo viliazimia kuanza rasmi leo harakati za kuhamasisha umma kupitia maandamano na mikutano ya hadhara.
Ndoa hiyo ya wapinzani waliifunga, Septemba 15,
kwa kuandika historia nyingine mpya kwenye tasnia ya siasa za Tanzania
wakipinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa
mwaka 2013.
Wanadai mapendekezo mengi yaliyomo katika Rasimu
ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yalipendekezwa na
vyama hivyo, hivyo havitakuwa tayari kuona maoni hayo pamoja na ya
Watanzania wengi yakichakachuliwa.
Wanasema muungano wao ni mwanzo wa kuunganisha
umma wa Watanzania kufanya uamuzi wa kunusuru utekaji madaraka na
mamlaka ya nchi kutoka kwa wananchi.
Kwa habari zaidi ingia www.mwananchi.co.tz
Kwa habari zaidi ingia www.mwananchi.co.tz
No comments
Post a Comment