Writen by
sadataley
5:33 AM
-
0
Comments
Dar es Salaam. Mkutano wa Matokeo Makubwa Sasa ya Maendeleo (BRN), katika sekta ya elimu unafanyika leo jijini Dar es Salaam huku mambo muhimu tisa yanatarajiwa kujadiliwa, ikiwa ni pamoja na ubora wa elimu na masilahi ya walimu.
Akizungumza jana kwenye warsha ya utangulizi wa mkutano huo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, aliyataja mambo yaliyo katika mpango huo kuwa ni upangaji wa shule kwa ubora wa matokeo ya mtihani kuanzia shule iliyoongoza hadi ya mwisho, uratibu wa utoaji wa tuzo kwa shule zilizofanya vizuri na kuwa na kiongozi cha usimamizi wa shule.
Mambo mengine ni upimaji wa kitaifa wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu, kujenga uwezo wa walimu na wanafunzi katika ufundishaji na ufundishwaji, ujenzi wa miundombinu ya shule, utoaji wa ruzuku ya uendeshaji wa shule na utoaji wa motisha kwa walimu.
Kuhusu upangaji wa shule kwa ubora wa matokeo, Kawambwa alisema kuwa utaratibu huo unalenga kuwezesha kila mkoa kujitathmini na kupanga ubora wa elimu katika sehemu husika.
“Aidha, mosi, Utatumika upangaji wa shule kwa ubora wa matokeo ya mtihani kama kigezo cha uteuzi na kuwabakisha walimu wakuu na wakuu wa shule kwenye nafasi zao; pili, kiwe ni kigezo cha kuainisha shule ambazo zitafuatiliwa zaidi ili kuboresha uwajibikaji, kupanda daraja na kuongeza kiwango cha ufaulu,” alisema Kawambwa.
Alisema maofisa elimu wa mikoa na wilaya ambao watashindwa kusimamia shule na kuzifanya zifanye vibaya katika matokeo watawajibishwa na kwamba kushindwa kwa wanafunzi wengi kutoka wilaya au shule moja kitatumika kuwa ni kigezo cha wao kushindwa kazi.
Mkutano huo ulihudhuliwa na maofisa elimu mikoa, wilaya, wakaguzi wa elimu na wakuu vya vyuo vya ualimu vya umma na binafsi.
Kiwango cha ufaulu
Katika hatua nyingine Waziri Kawambwa amewataka walimu nchini kuhakikisha kuwa wanapandisha kiwango cha ufaulu wa mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne hadi kufikia asilimia 60.
Kauli hiyo ya Kawambwa imekuja wakati ukiwa umebaki mwezi mmoja kwa wanafunzi wa darasa la saba na miezi mitatu kwa kidato cha nne kufanya mtihani yao.
Katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2012 wanafunzi walifaulu kwa asilimia 31, huku kidato cha nne wakifaulu kwa asilimia 43 na Kawambwa anasema matokeo mapya yanatakiwa kufikiwa kuanzia mwaka huu.
Kawambwa alisema katika kutekeleza vipaumbele tisa vilivyowekwa na mpango wa BRN, kila mtendaji katika sekta ya elimu atapimwa kutokana na utekelezaji katika eneo lake na kwamba mambo makuu matatu yanapaswa kuanza mwaka huu.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuongeza ufaulu katika elimu ya msingi kutoka asilimia 31 mwaka 2012 hadi 60, kuongeza ufaulu katika shule za sekondari kutoka asilimia 43 mwaka 2012 hadi 60 mwaka 2013 na kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi wa darasa la pili ataingia darasa la tatu akiwa anajua kusoma, kuandika na kuhesabu.
“Ili kufikia azma hiyo inabidi kila mmoja wetu ajipange katika kuangalia upya majukumu yake,” alisema Dk Kawambwa.
No comments
Post a Comment