Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Wednesday, August 14, 2013

Wageni hawa wanafuata nini bara la giza?

Rais Mstaafu wa Marekani akisalimiana na wananchi wa Vingunguti alipotembelea Dar es Salaam hivi karibuni. Picha ya Maktaba 
Na Elias Msuya, Mwananchi 
Mgeni njoo mwenyeji apone. Huu ni msemo wa siku nyingi wa Kiswahili. Msemo huu ndio mtazamo wa Watanzania na waafrika kwa ujumla kwa wageni wanaotumbelea kutoka ng’ambo – waje tunufaike na sio kinyume chake. 
Huko wanakotoka wageni hawa, miaka ya nyuma katika karne ya 19 waliita Afrika bara la giza. Siyo kwamba bara hili halikuwa na jua wala mwezi, bali ni kwa sababu hawakulijua, na hivyo pamoja na utajiri wa bara hili, ukiwamo ule waliouchota na kujinufaisha, hawakulithamini.
Katika kitabu chake cha “Dr. Livingstone I presume?” alichokiandika baada ya kumfuatilia Dk Livingstone Kaskazini mwa Tanzania Novemba 10,1871, mwandishi na mpagazi wa wakati huo, Henry Stanley alitumia maneno, ‘Nilipita katika bara la giza’ akimaanisha kuwa bara hilo halikuwa likifahamika kwa Wazungu kwa muda mrefu.
Wakati huo mataifa ya Ulaya yalijikita kwenye mabara mengine kama vile Marekani, Asia na Australia. Afrika lilikuwa bara la mwisho kufikiwa na kuambukizwa ustaarabu wa Ulaya, ndiyo maana wengi wanaona liko nyuma kimaendeleo.
Bara la Afrika lilikuja kufikiwa na kutawaliwa katika karne ya 19.
Baada ya Wazungu kugundua utajiri ulioko Afrika walivutwa kiasi cha kuligawana vipande katika mkutano wa Berlin wa mwaka 1884/85.
Hata baada ya kuligawa na kulitawala, bado hawakuweza kuyafikia maeneo mengi. Ndiyo maana hata baada ya nchi za Afrika kupata uhuru miaka ya 1960, bado mataifa ya Ulaya yameendelea kuitazama Afrika kwa jicho la tamaa kutokana na wingi wa rasilimali zinazopatikana.
Mbali na mataifa ya Ulaya, baadhi ya mataifa ya Asia hasa China na Marekani nayo sasa yamekuja kwa kasi kusaka rasilimali hizo.
Hivi karibuni, kumekuwa na ziara za viongozi wa mataifa hayo nchini Tanzania huku ikielezwa kuwa yanavutiwa na hali ya utulivu na amani kuliko mataifa mengineyo yanayozunguka Afrika Mashariki na Kati.
Mwezi Machi mwaka huu, Rais wa China Xi Jingping aliitembelea Tanzania ambapo alihutubia dunia akiwa hapa nchini.
China imewekeza karibu katika kila sekta nchini kuanzia kilimo, viwanda na hata biashara ndogo ndogo.
Katika kile kinachoonyesha kujibu mapigo, Julai Rais wa Marekani, Barack Obama naye akatua Tanzania akiwa na msafara wa wafanyabiashara wapatao 700.
Wakati Obama akiwa nchini, Rais mstaafu wa nchi hiyo, George Bush naye alikuja akimsindikiza mkewe Laura kuhudhuria mkutano wa masuala ya wanawake uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Wakati huo huo kulikuwa pia na mkutano wa ‘Smart partnership uliowahusisha viongozi kadhaa wa Afrika, akiwemo Mfalme wa Swaziland Mswati, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na wengineo.
Mwezi huu Tanzania imepata ugeni mwingine mzito tena, baada ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza, Tony Blair na mkewe Cherrie kuzuru nchini. Hata hivyo ziara yao ilikuwa ya kimya kimya.
Ziara hiyo ilifuatiwa na Waziri wa Thailand, Yingluck Shinawatra kuja nchini ambapo pamoja na mambo mengine alitia saini mkataba wa kubadilishana wafungwa kati ya nchi hizo mbili.
Ziara hiyo nayo ilifuatiwa na ujio wa Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton ambaye alikuja kutembelea miradi midogomodogo ya wananchi iliyo chini ya mfuko wake ikiratibiwa na kutekelezwa na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Plan) pamoja na Benki ya Barclays kupitia Vikoba.
Mfululizo wa ziara hizo kwa kipindi kifupi, unaelezwa na wasomi kadhaa kuwa mataifa makubwa yanaimulika Afrika na hasa Tanzania kwa lengo la kufaidika na rasilimali ambazo ndiyo kwanza zinagunduliwa. Sisi tunasema acha waje tu, ilimradi, iwe “mgeni njoo mwenyeji apone.”
Akizungumzia ziara hizo, mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humphrey Moshi anasema kuwa ziara hizo zinaonyesha jinsi mataifa makubwa yanavyopigania rasilimali za Afrika.
“Mengi yanasemwa, lakini hili na kupigania rasilimali ni la kweli. Nchi yetu kwa sasa ina rasilimali nyingi kama gesi, mafuta na madini na China imeshawekeza barani Afrika karibu katika kila sekta. Marekani nayo inaona imeshachelewa, ndiyo maana inakuja kwa kasi,” anasema Profesa Moshi na kuongeza:
“Zamani Marekani haikuona umuhimu wowote Afrika, ndiyo maana uwekezaji wake ni asilimia moja tu, huku bidhaa inazouza huku ni asilimia mbili. Hata ukiangalia Obama alipokuja alizindua mradi mdogo wa umeme wa Symbion wa Megawati 100. Kwa sababu hawana uwekezaji mkubwa kwetu. Lakini sasa imeshtushwa na China ndiyo maana anakuja kwa kasi.”
Huku akizitaja nchi za Tanzania, Afrika Kusini, Nigeria na Senegal zinazopata misaada mikubwa kutoka Marekani, Profesa Moshi anasema kuwa nchi hizo zimechaguliwa kuwa kianzio cha nchi hiyo kujikita Afrika.
“Msaada mkubwa uliokuwa ukitolewa na Marekani ni soko la bidhaa za Afrika kupitia Mpango wa ushirikiano wa kibiashara baina ya Marekani na nchi za Afrika (Agoa). Walitoa kati ya nafasi za bidhaa 3,000 hadi 4,000, lakini nchi za Afrika zilipeleka bidhaa 300 tu. Hatujafanya vizuri hadi mwisho wa awamu ya kwanza itakayokwisha 2015. Sasa wanataka watumie awamu ya pili ya Agoa kuwekeza zaidi Afrika,” anasema.
Naye mhadhiri wa sayansi ya siasa wa chuo hicho, Dk Alexander Makulilo anapinga dhana ya kuwepo kwa amani kama kigezo cha nchi tajiri kuvutiwa na Tanzania.
“Haya ni mapambano kati ya Marekani na China katika rasilimali na kuweka kambi za kijeshi. Marekani inataka kudhibiti eneo la maziwa makuu kama vile Congo na Rwanda kupitia Tanzania kwa sababu wenyewe wako mbali,” anasema Dk Makulilo na kuongeza:
“Haya masuala ya kisiwa cha amani yanazua maswali mengi hasa ukiangalia jinsi uhalifu ulivyozidi huku kukiwa na makongamano ya kusisitiza amani ambayo hayakuwepo zamani.”
Hata hivyo, Dk Makulilo anasema kuwa Tanzania inaweza kufaidika na uwekezaji wa nchi hizo iwapo kutakuwa na makubaliano yenye faida.
“Hatuwezi kuzikatalia nchi hizi moja kwa moja kuwekeza katika rasilimali. Ndiyo, yanaweza kutokea kama ya Libya ambapo kiongozi wao Muammar Gaddafi aliuawa. Shida ni kwamba, tunakubaliana nao vipi kwenye mikataba? Tunatakiwa tuwe na ‘win win situation’ (wote tunufaike),” anasema.
Kwa upande wake mhadhiri mstaafu wa chuo hicho, Profesa Ruth Meena anasema kuwa kinachotokea si uporaji wa rasilimali bali tatizo ni sisi kuzigawa hizo rasilimali bure.
“Bara la Afrika lililoonekana kuwa la giza, sasa lina nuru, ndiyo maana viongozi hao wanakuja maana kuna faida. Siku zote uwekezaji wa kibepari una unyonyaji mwishoni, lkini kinachofanyika hapa si uporaji maana kuna mikataba ambayo viongozi wetu wanasaini,” anasema Profesa Meena.
Kwa ujumla wasomi hao wanasema hakuna namna ya kuwazuia wageni, kinachotakiwa ni kuhakikisha kila upande unanufaika na uwekezaji wao.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment