Writen by
sadataley
6:44 PM
-
0
Comments
JUBILII YA
KKKT YA MIAKA 50
NA MAENEO MAPYA YA MISSIONI
KWA MIAKA 50 IJAYO
KWA MIAKA 50 IJAYO
Na Mchungaji Profesa Wilson Niwagila
Nachukua fursa hii kumshukuru
sana Mheshimiwa Askofu Dk. Benson Bagonza kwa kutupanua mawazo na kuona kwa
macho ya ndani maeneo mapya ya Misioni ya Kanisa miaka 50 ijayo. Tukizungumzia maeneo mapya ya
misioni tuelewe kwamba tunalenga mawazo yetu katika maeneo haya.
Kwanza: Misioni ya ndani. Hapa ni kusema kwamba
kanisa linahudumia waumini wake, ili waweze kukua na kuwa na Imani thabiti. Ni
mahali pa kuhamasisha waumini kufahamu wajibu wao kama wafuasi waaminifu wa
Bwana Yesu, wakihudumiana na kuhudumia watu wengine. Askofu Dk. Bagonza ameweka bayana hali ya
sharika zetu kwamba zinatofautiana kitakwimu kimaendeleo na kimapato; kuna
sharika tajiri na sharika maskini lakini sharika tajiri hazisikii deni kusaidia
sharika maskini. Hapa kuna hali ya
kusahau tulikotoka. Mwanzo wa sharika tajiri zilikuwa katika hali ya umaskini,
vyama vya misioni vikatoa fedha kwa kujenga msingi mzuri. Fedha kutoka vyama
vya misioni zilikusanywa kutoka sharika na wakristo wenye moyo wa kuhudumia
watu wa nchi nyingine. Sasa hapa kwetu Tanzania sharika tajiri zinafanya mambo
mengi yenye garama kubwa lakini hazitupii macho kuona sharika zenye mahitaji ya
msingi.
• Dhambi kubwa ya kutajirika, ni kutokuwa na
nidhamu ya kutumia utajiri kwa manufaa ya maskini. Ubinafsi ni tunda la uchoyo. Ikiwa sharika
tajiri haziwezi kutambua hili basi tujue kwamba ndio mwisho wa kukua kiroho. Misioni ya ndani inapaswa kuwa na macho kuona
mahitaji ya watu wa Mungu, inapaswa kuwa na
masikio kusikia kilio cha uumbaji wa Mungu, inapaswa kuwa na miguu
kuondoka pale ilipo na kufika penye tukio, inapaswa kuwa na mikono kutenda yale
yote yaipasayo. Kitabu cha Kutoka SURA ya 3:7-10 ni changa moto kwa kanisa
kuelewa maana ya misioni ya ndani na nje. Kanisa haliwezi kufaulu kama
halifuati sera ya Mungu: KUSIKIA vilio vya watu wa Mungu, KUONA
dhuluma, uonevu na mateso ya uumbaji wa Mungu, KUONDOKA na kuelekea
kwenye matukio na KUWAJIBIKA kwa njia yoyote ile ili watu wa Mungu na
uumbaji wake ufurahie UKOMBOZI wa Mungu.
Pili: Eneo la Misioni linaweza kuwa misioni nje ya
Kanisa.
Hapa yanaweza kuwa maeneo ya
kijografia kufuata tulivyozoea kwa kuanzisha maeneo mapya. Pamoja na hayo
maeneo mapya yanamaanisha pia
kukabiliana na changamoto mpya ambazo hatukuzoea, kwa mfano mfumo mpya wa
mawasiliano, lugha mpya, uhusiano kati ya wasomi na watu ambao si wasomi,
uhusiano kati ya matajiri na maskini, uhusiano kati ya vyama vya siasa vikiwa
na lengo moja la kumhudumia mwananchi bila kupoteza muda mwingi kwa malumbano.
Matabaka haya yote yako ndani ya usharika, mchungaji au mwinjilisti atafauluje
kuwahudumia hawa wote pamoja wakaweza kujisikia kwamba ni familia moja katika usharika
na katika taifa?
Kanisa linakabiliwa na changa moto kubwa
katika kueneza Injili kwa miaka 50 iliyo mbele yetu. Nidhahiri kwamba
changamoto hizi zinaendana na mabadiliko
makubwa na ya kasi kwa mujibu wa uvumbuzi mpya wa mambo ya sayansi, utanda wazi
na mabadiliko ya tabia ya nchi, tamaduni na mapokeo. Kanisa haliwezi kuzuia
mabadiliko haya lakini lazima liwe makini katika kukabiliana na changa moto
hizi. Kanisa lina sura mbili kama shilingi; upande mmoja Kanisa limepewa
mamlaka ya kufundisha, na upande wa pili Kanisa limeambiwa kwamba ni Mwanachuo.
Roho wa Mungu yupo ndani ya Kanisa akielekeza, akiongoza na kufundisha ili
kukabiliana na mabadiliko pamoja na changamoto zake. Kuwa mwana chuo ni
kusikiliza mwalimu, kufanya kazi za mwalimu, kufanya utafiti ili kubaini mambo
muhimu yatakayomsaidia kuwa mwanachuo mahiri wa kuelekeza wengine katika
kufaulu mitihani ya maisha. Hapa napenda kusisitiza kwamba maendeleo mazuri ya
mwanachuo ni kutopoteza muda alionao, tena ni kubaini kila msaada uliopo
kujiendeleza. Bahati nzuri siku hizi mtu unaweza, ukitaka, kujifunza mambo
mengi yenye manufaa kwa njia ya mitandao popote pale. Huna haja ya kwenda
maktaba iliyo mbali.
• Maendeleo ninayozungumzia si kujenga
barabara au kuleta maji na umeme
nyumbani peke yake bali pia maendeleo ya mtu binafsi kujiendeleza
kielimu. Elimu si kwa vijana tu bali pia na kwa sisi wazee. Shoka isiponolewa
kazi inakuwa ngumu sana, na unakosa mwelekeo na hapo unaambiwa na vijana “mzee
umepitwa na wakati”. Miaka 50 iliyo mbele yetu ni miaka ya kunoa akili zetu,
kuwa na mawazo mapya ya kukabiliana na changa moto za Karne hii.
•
• Wakati huu wa mabadiliko ni wakati mgumu
wa kuelewa mambo vizuri yanayokabili watu wa Mungu. Wakati mwingine serikali,
mashirika, Umoja wa Kimataifa hawana majibu sahihi; lakini Kanisa, kama
mwanachuo chini ya mwalimu mkuu Roho Mtakatifu, linafundishwa kukabiliana na
changa moto zinazogusa maisha ya binadamu. KUTOKA sura ya 3 Musa anaonesha
ugumu wa utume wake- Ilikuwa changa moto kali kumkabili Farao, lakini Mungu anamhakikishia
kwamba yuko mbele na nyuma yake.
• Askofu Dr. Bagonza aligusia suala la from
the centre to the periphery.
• Hili ni suala muhimu sana na la kufanyia
kazi hasa tunapoona watu wengi wanakimbia kutoka the periphery to the centre
nikimaanisha kutoka vijijini na mikoani na kukimbilia mijini, jambo ambalo
linaleta msongamano wa watu na msongo wa mawazo.
• Niruhusu nitoe mfano huu. Miaka 100
iliyopita chama cha misioni kutoka Ujerumani kilichoitwa Bethel Mission
kilifanya kazi Usambara, Bukoba na Rwanda. Mbinu yake ya kueneza Injili ili
kukabiliana na upinzani wa Dini ya Kiislamu katika Afrika ya Mashariki ilikuwa
kuanzisha maduka ya biashara katika kila stesheni walizozijenga kwa makusudi
mawili; kwanza waligundua kwamba waislamu ni wafanya biashara wakubwa hivyo
ilikuwa rahisi kuwavutia wananchi kwa biashara yao. Bethel Mission nayo ikaleta
kivutio cha biashara kwa makusudi ya kuwavutia watu na kuwasaidia wakristo
kununua bidhaa kwa maduka ya misioni. Pili ilikuwa njia ya kuwafundisha
wakristo nao kuwa wafanya biashara katika sehemu zao vijijini wakiongozwa na
Roho wa Mungu, ili biashara yao isiwe ya kupunja watu walio maskini. Kwa njia
hii haya maduka sehemu za vijijini yalibadilisha mwelekeo wa mawazo ya
kukimbilia mijini kutafuta maisha. Nakumbuka baada ya kuanza kazi ya ualimu
huko Magoye, sasa Dayosisi ya Kusini
Kati, nilihitaji Transistor Radio, badala ya kwenda Mbeya au Iringa
nilikwenda Bulongwa ambapo mmisionari mmoja alikuwa ameanzisha duka la kuuza bidhaa
muhimu, zikiwemo radio, kwa bei nzuri (poa).
• Ninalotaka kusema hapa ni nini? Changa
moto tuliyonayo wakati huu ni watu kukimbilia mijini eti kutafuta Maisha. Mbaya
zaidi serikali zetu hazifunuliwi kuanzisha miji na kuweka vitega uchumi
vijijini; hivyo watu wote, vijana kwa wazee tunakimbilia mijini na sisi tupate
uhondo wa miundo mbinu ya miji.
• Wajibu wa kanisa hapa ni upi? Kanisa
litake lisitake litakumbana na changa moto hii. Wakristo wengi wataacha vijiji
na kuhamia mijini, makanisa yaliyoko mijini yatasongwa na mambo haya:
• Watu wa tabaka mbalimbali na jinsi ya
kuwahudumia kikamilifu
• Msongamano wa watu kutokana na ukosefu wa
miundo mbinu bora mijini
• Umaskini uliokithiri utaongezeka mijini
• Magonjwa ya kila aina yatalipuka
• Watu wanaohitaji misaada watakuwa wengi na
Kanisa ndilo litafuatwa kutoa msaada.
• Kanisa litakosa watumishi bora vijijini.
• Huko vijijini watabaki wazee ambao
hawatakuwa na msaada wa karibu, hivyo kama mijini mambo hayatakuwa mazuri.
Sharika zitaendelea kudhoofika na sharika za mijini zitaendelea kuimarika
kifedha. Wachungaji wengi watapenda nao kuhamia mijini ili nao wapate mshahara
mkubwa badala ya kupewa posho.
• Watu wanapokuwa wengi mijini matatizo
mengi yanaibuka, utunzaji wa mazingira unakuwa na matatizo. Nimebahatika
kutembelea Indonesia, Sri Lanka na Philipines. Miji hii imekumbwa na utupaji
taka. Pale Jakata Indonesia na Manila Philipines kuna milima ya takataka,kwa
kuwa watu katika miji hii ni wengi sana, kuna shida ya kupata ajira, hivyo
unakuta wakina mama, na watoto wachanga wako kwenye mlima wa takataka
wakichambua kila kitu kuona kama kutapatikana chochote. Afya zao zinahatarishwa
na uchafu wanaoshika, vyakula kutoka mahoteli vilivutupwa vinaokotwa na
kutumiwa kama chakula
• Hali hii imeanza kujitokeza katika miji
yetu ya Tanzania. Taka zinatupwa ovyo tena karibu na mito. Mvua zikinyesha basi
uchafu pamoja na sumu za kila ainazinatiririka kwenye maji yanayotumiwa na
jamii.
• Kazi iliyombele yetu kama Kanisa ni
kufanya yafuatayo:
• Kushauri na kukumbusha serikali kuona
umuhimu wa kuendeleza vijiji kwa kujenga miundo mbinu muhimu kusudi wananchi
nao wafurahie maendeleo na uhuru wao. Hapa nazungumzia shule navyuo, hospitali
nzuri zinazotoa huduma bora, makampuni ya kuwekeza, maji na umeme ili wana
vijiji nao waanzishe miradi midogo na mikubwa.
• Kuelimisha jamii namna ya kuendeleza
mahali walipo huko vijijini wakiungana na serikali.
• Kazi
ya kutetea wanyonge (advocacy).
• Wajibu
mkubwa miaka 50 ijayo ni kukaza nguvu katika utetezi na unabii.
• Ulimwengu tuliomo na unaokuja ni ulimwengu
ambao hauna huruma. Uonevu, ulafi, unyanganyi, dhuluma, mauaji na kujipenda
vitazidi kushamiri. Hapa watuwanyonge ndio watazidi kuteseka na kukosa amani.
Hivyo ni wito wa Kanisa kujiweka sawa sawa kupambana na hali hii.
Ahsante kunisikiliza
Mch. Prof. Wilson Niwagila
Josiah Kibira University College of Tumaini University Makumira
22/06/2013
No comments
Post a Comment