Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya wateule wake akiwemo kiongozi mkuu wa idara ya usalama wa taifa Diwani Athuman ambaye amebadilishiwa majukumu yake na kuwa katibu mkuu wa Ikulu huku nafasi yake ikichukuliwa na Said Hussein Nassoro. Awali, Nassoro alikuwa naibu mkurugenzi mkuu na mkurugenzi wa shughuli za ndani wa idara hiyo.


Diwani Athuman ambaye ni Kamishana wa Jeshi la Polisi, amehudumu katika nafasi hiyo kwa takribani siku 1,210, tangu alipoteuliwa na Rais wa wakati huo, Hayati John Magufuli Septemba 12 mwaka 2019.


Kabla ya Athumani kushika wadhifa huo wa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa alihudumu kama mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).


Hata hivyo ,Rais Samia amefanya mabadiliko mengine kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga ambaye ameteuliwa kwenda New York nchini Marekani kuwa Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa (UN).


Balozi Kattanga ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa katibu mkuu kiongozi Machi 31, 2021, alichukua nafasi ya Dk Bashiru Ali ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Kuteuliwa.


Kattanga aliteuliwa kushika wadhifa huo kutoka kuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan na sasa anakwenda kuchukua nafasi ya Profesa Kennedy Gaston.


Akitoa sababu za kumrejesha nchini Profesa Kennedy, Rais Samia amesema katika mkutano wa Bunge wa Novemba mwaka jana kulikuwa na mjadala mzito wa matumizi ya fedha na madaraka katika ofisi mbalimbali za kibalozi na ulimwenguni na Serikali inazifanyia kazi dosari hizo.

MUUNGWANA BLOG