Writen by
sadataley
9:22 PM
-
0
Comments
Kwa uchache watu wawili wamejeruhiwa baada ya jeshi la polisi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujaribu kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wanamshinikiza Rais Joseph Kabila akabidhi madaraka.
Rais Joseph Kabila ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akizungumza na waandishi wa habari mjini Kinshasa, Januari 26, 2018. (Picha na AFP)
Leo Jumapili machafuko yamezuka katika mji wa Kisangani ambao ni wa tatu kwa ukubwa nchini humo baada ya askari polisi kujaribu kuwatawanya waandamanaji. Kuna ripoti zinazosema kuwa polisi walitumia risasi hai na mabomu ya kutoa machozi katika juhudi za kuvunja maandamano hayo.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, kwa uchache watu wawili wamejeruhiwa kwa risasi na wahubiri watatu wa Kikristo wametiwa mbaroni kwa kosa la kuongoza maandamano hayo katika wilaya ya Saint Pierre de Wagenia mashariki mwa Kisangani.
Maandamano hayo yaliyoitishwa na Kanisa yamefanyika kupinga uamuzi wa Rais Joseph Kabila wa kukataa kuondoka madarakani.
Maandamano mengine yaliyofanyika katika mkesha wa mwaka mpya mwezi uliopita wa Januari yalikuwa ya umwagaji damu baada ya polisi kuwashambulia kwa risasi waandamanaji.
Takwimu zilizotolewa na waandaaji wa maandamano hayo pamoja na Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa watu 15 wameuliwa na polisi katika machafuko ya huko nyuma, ingawa takwimu hizo zinapingwa na serikali ambayo inasema ni watu wawili tu waliouawa kwenye maandamano hadi hivi sasa.
Rais Joseph Kabila yuko madarakani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwaka 2001 akiongoza serikali inayolaumiwa sana kwa ufisadi, ukandamizaji na kutowajibika ipasavyo.
Muda wa kikatiba wa urais Joseph Kabila (46) ulimalizika mwezi Disemba 2016 lakini ameendelea kubakia madarakani chini ya sheria yenye utata ya kumruhusu kubakia madarakani hadi atakapopatikana mtu wa kurithi kiti chake.
Parstoday

No comments
Post a Comment