SERIKALI inaendelea kuchunguza wamiliki wa Makontena matano ya magogo yaliyokamatwa bandarini mwaka juzi, kuwafikisha mahakamani.
Shehena hiyo ya magogo ya mti aina ya Mkulungu ilikamatwa Novemba 5, 2015 yakionyesha yanatokea Zambia kwa ajili ya kusafirishwa nchi za Mashariki ya Mbali.
Akizungumza na Nipashe jana kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi ya Rasilimali za Misitu, Mohamed Kilango, alisema makontena hayo yalikamatwa baada ya kukosekana kwa nyaraka za mzigo huo.
“Wale wahusika tuliwaambia watuletee ‘documents’ (nyaraka) wakashindwa. Sasa tulichokifanya ni kuendelea na taratibu za kiserikali ili watu hao wapelekwe kwenye mkondo wa sheria. Uchunguzi bado unaendelea siwezi kusema ulipofikia,” alisema.
“Nyaraka zimeshaletwa lakini zinahitajika kuthibitishwa. Lazima tukubaliane na serikali ya nchi ambazo zimetoka kwani utaratibu wa kimataifa upo ili kujiridhisha. Kwa sasa tuko kwenye hatua nyingine,” aliongeza.
Kilango alisema suala hilo limechukua muda mrefu kwa kuwa linahusisha nchi mbili, hivyo uchunguzi unafanyika kwa nchi zote ili kujiridhisha.
Kilongo alisema kama mtu anasafirisha magogo kwenda nje ya nchi, kuna vitu vitatu ambavyo mhusika anatakiwa kuwa navyo. Alivitaja vitu hivyo kuwa ni cheti cha ubora wa mazao ya nchi, cheti cha kuruhusiwa kusafirisha mazao katika nchi anayotoka na kibali halisi cha nyaraka.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, alisema nchi hairuhusiwi kusafirisha magogo kwenda nje na kilichoruhusiwa ni mbao kwa kibali maalumu
No comments
Post a Comment